KINA CHA FIKIRA: Ubora wa mtu daima huwa ni mtu mwenyewe
Na WALLAH BIN WALLAH
KATIKA maisha ubora wa mtu umo ndani ya mtu mwenyewe.
Mtu akitaka kuwa bora au akitaka kuwa mtaalamu katika kazi au taaluma yoyote ama katika lugha ya Kiswahili, anapaswa kujitolea kwa ari na nia kujifunza mpaka awe mtaalamu kamili.
Mtu hawezi kutaalamika kwa kudhania tu au kwa kutamani tu kuwa mtaalamu; kwa kuwaigaiga watu fulani waliobobea! La, hasha! Fulani ni fulani!
Kila mtu ana ubora wake na kipawa chake asilia ambacho akikikuza na kukilea vyema, anaweza akawa bora zaidi ya wengine wengi.
Nimeamua kuleta kauli hii kuhusu kujiboresha kwenye ukurasa huu wa gazeti letu tulipendalo la Taifa Leo baada ya kushuhudia minong’ono mingi kuwa ni kwa nini baadhi ya wataalamu na wapenzi wa Kiswahili hutumia lugha bila ya kuzingatia kanuni za sarufi na ufasaha?
Mbona wengine hupotoka mpaka wakayatumia maneno ya Kiswahili Ndivyo Sivyo chambilecho Ndugu Enock Nyariki katika makala yake ya Taifa Leo kila Jumatano?
Katika udadisi wangu, nimewasikia wengine wanaokitumia Kiswahili upogoupogo wakijitetea kwa kutoa vijisababu vyao vingi tu! Wapo wanaosema ati nia yao ni kuifanya lugha ya Kiswahili iwe nyepesi ili kwamba waelewane kwa urahisi na watu ambao wanalenga kuwasiliana nao!
Wengine hudai kwamba walipokuwa shuleni au chuoni hawakufundishwa vizuri! Ati waling’ang’ana kujifunza Kiswahili wenyewe kwa wenyewe tu bila walimu! Wapo wanaotoa hoja kwa ukakamavu kabisa kwamba hivyo wanavyoitumia lugha ya Kiswahili ndivyo walivyofunzwa walipokuwa masomoni! Walilelewa hivyo wakaelewa hivyo!
Pia wapo wanaojitetea kwamba wanayatumia maneno ya Kiswahili jinsi walivyowasikia wazungumzaji wengine wakiyatumia. Nao wakawaiga hivyo hivyo wakidhani ni lugha sahihi! Hao ni miongoni mwa wale waliozoea kutamka *panguza, guza, masaa, masiku, manyumbani, vuruta badala ya vuta, mazingara badala ya mazingira. Ndio hao hao wanaotumia kivumishi mingi kuvumisha nomino zote za kila ngeli wakisema: chakula mingi, siku mingi, pesa mingi, vitu mingi, mambo mingi, ugali mingi, maneno mingi; kila kitu kwao ni mingi tu!
Wapo wanaoyatumia maneno kwa makosa bila kujua kuwa wanakosea! Hapo ndipo pana umuhimu wa kujifunza ili mtu awe na hakika ya jinsi ya kuyatumia maneno kwa usahihi na mantiki katika lugha yoyote.
Vitabu vya kujifunzia Kiswahili vipo tele! Kamusi za kumwongoza mtu kujua matumizi sahihi ya kila neno kuhusu maana na kubainisha nomino katika ngeli sahihi zipo nyingi! Ubora wa mtu umo ndani ya mtu mwenyewe! Kujifunza ndiko kuelewa!!