Makala

KINAYA: ‘Baba’ bado ni jogoo wa siasa licha ya ‘kusaliti' NASA kupitia handisheki

October 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na DOUGLAS MUTUA

ACHENI ‘Baba’ aitwe ‘Baba’! Ala! Kivipi tena? Sikiza, tena unisikize vizuri. ‘Baba’ ni mwanasiasa mzito asiye na mfano wake, tatizo ni kwamba hajajua kuingia Ikulu.

Sina mazoea ya kumsifu mwana wa Jaramogi, hasa kwa maana tangu mwanzo nimemjua kama kigeugeu.

Naam, kigeugeu haswa, anayeweza kuwaacha wafuasi wake wakizubaa kwenye kingo za Mto Jordan kwa madai ameona mamba hatari! Aliyemwita ‘Joshua Mwitu’ alijua!

Ikiwa kuna mtu aliyeumwa na tendo la kushtukiza la ‘Baba’ kuwaacha watu wa NASA kwenye mataa na kwenda kusalimiana na ‘Ouru’ usiku, mwite mimi.

Kwa nini, ilhali tangu hapo sizijali nyendo za kigogo huyo wa siasa za upinzani? Kisa na maana ni kwamba nampenda sana akiwa kwenye upinzani akiwatetemesha wezi serikalini.

Sasa yumo ndani ya Serikali, tena nakwambia yuko kimya kabisa haneni kitu kwa maana si ustaarabu kuzungumza ukiwa na chakula kinywani. Tutapata taabu sana.

Japo sina mazoea ya kumsifu ‘Baba’, lazima nikubali, hata shingo upande tu, kwamba ana wafuasi wake sugu wasiojali anateuka au anazungumza. Kwake yote mawili ni sawa.

Hao, wafuasi wake, ndio watu ninaonuia kusifu kwa kudumisha uzalendo wao kwake hata baada ya mzee wa watu huyo kuwasaliti vibaya.

Kuwasaliti vipi? Kuungana na ‘Ouru’ usiku na kudai anamsaidia kutawala ila hawajaona manufaa ya hakika, tena dalili zinaonyesha atachezwa shere kishenzi kabla ya 2022.

Ninataka kuwasifu wafuasi wa ‘Baba’ kutokana na tukio la hivi majuzi lililofanyika ninakoishi, kwenye nchi ya watu: Marekani.

MaDVD, yule mwana wa Moses Mudamba Mudavadi ambaye nahisi anaweza kuwa rais mzuri akiombewa kura za kutosha kwa maana hawezi kujiombea, alitutembelea.

Usimcheke MaDVD kwa kusikia hawezi kujiombea kura! Hata Baba Jimmy hakujua kura huombwaje ila alipoombewa na ‘Baba’ zikatosha alituongoza vyema kuliko marais wote.

Acha nikurejeshe kwenye ziara ya MaDVD. Watu walikuja kiasi cha haja. Wapo pia waliofuatilia shughuli zote za ziara hiyo mitandaoni.

Bila shaka wawakilishi wote wa Kenya walio ughaibuni, yaani sisi mabalozi tusio na mishahara, tulifuatilia kwa makini.

Wapo waliofuatilia kwa maana yule mwanasarakasi wa eneobunge la Gichugu, yaani ‘malkia mstaafu’ Martha Wangari Karua, alikuwepo pia.

‘Mstaafu’ huyo alisaidia kujaza chumba tu; wengi tunaomtuhumu kwa kuchakachua kura za urais mnamo 2007 na kumwapisha Baba Jimmy usiku hatuna hamu naye.

Samahani tena kwa kukupoteza kidogo, sasa nakurejesha tena kwenye mkondo mkuu wa kisa cha MaDVD kutuzuru Marekani na kuwavutia watu wengi.

Kilichonishangaza ni jinsi watu walivyomchangamkia na kumkumbatia MaDVD, wakasema atakuwa rais wao kuanzia 2022, ila wakaharibu mambo kwa kutoa sharti kuu.

Sharti lenyewe ni kwamba watamchagua MaDVD tu ikiwa ‘Baba’ hatawania urais, akiwania basi MaDVD asahau kura zao kama alivyolisahau titi la mama yake!

Kwani ‘Baba’ aliwalisha wafuasi wake kiapo cha aina gani? Labda nimwendee usiku nami anipe siri, nikulishe usiwahi kukosa makala ya Kinaya hata siku moja….

Labda ‘Baba’ anaweza kuinusa Ikulu akimchukua MaDVD kama mgombea mwenza, wazichape kiume na Dkt Bill Kipchirchir. Nawaza tu.

 

[email protected]