KINAYA: Eti wazee Mlimani wamtukana Ruto kumfurahisha ‘Kamwana’!
Na DOUGLAS MUTUA
JE, Kenya kuna ‘mama-mboga’ au mwanamke mzee?
Na mchoma-mahindi mzee? Na, je, yule bwana aliyepewa msimbo wa jina ‘Githeriman’ amezeeka? Mbona hakuhudhuria mkutano wa baraza la wazee wa Agikuyu ulioandaliwa Nyeri juzi?
Nauliza kwa kuwa sijaelewa anachohitaji mtu kuwa nacho ili aruhusiwe kujiunga na baraza hilo hatari na la kutishatisha.
Mambo gani haya tena? Kila shughuli za kisiasa zinaponoga, mimi husikia kundi hili au lile la wazee likimuonya mwanasiasa huyu au yule dhidi ya kufanya hili au lile.
Katika Karne hii ya 21, vuguvugu lolote linalodai kuwa imara ilhali halina hata mwanamke mmoja, ni kundi la wahuni wanaojitakia makuu kwa kuendeleza ubabe-dume na mfumodume.
Pia, vikongwe kuhudhuria mikutano huku wakijikongoja kwa mikongojo badala ya kutembea na wake zao ni mwendelezo wa uzembe uliokithiri katika jamii.
Uliza wanawake wengi, hususan wa mlimani, utapata ndio huzilisha familia zao kwa maana waume wamekuwa ovyo, hulewa mchana kutwa.
Vijiweni
Anayeraukia staftahi ya pombe hawezi kufanya kazi, ndio maana unawapata vijiweni wakizungumza mambo ya kitoto na kujichekea ovyo.
Hao ni waume wachanga. Waliokula chumvi kuwazidi ndio hao wanaoshika mikongojo na kuhudhuria mikutano ya kutukana watoto waliokuzwa vizuri wakawa viongozi wao kitaifa.
Na sarafu mpya zinatoka kutoka hadi 2022 ifike kwa maana mlimani wapo matajiri wengi wanaosubiri mtu tu azuke na kumtukana Daktari Samoei Ruto, pake pakavu watie mchuzi!
Tatizo, pesa hizo hazifiki nyumbani kwani wanaozipata hupitia kwa ‘mama-pima’ wakanywa kikombe cha ‘muratina’ na kula robo ya mbuzi, kabla wafike nyumbani mifuko imetoka nje kwa kuishiwa.
Kumbuka wake zao wamezeeka, lakini kwa kuwa hawaruhusiwi kuhudhuria mikutano ya wazee, wao hukaa nyumbani wakitafuta chakula ili wazee wakirejea wapate angalau kikombe cha uji.
Sasa niambie: Kizazi kichanga kinapokitizama kilichokitangulia kikilaza damu na kurejea nyumbani jioni kulishwa, kitakuwa na sababu gani ya kufanya kazi kwa bidii?
Ni kama kumwambia mtu asubiri kustarehe akizeeka ilhali akitaka anaweza kuanza starehe zake sasa hivi. Hata sifuati ushauri wa mtu kama huyo, nitafuata nyayo zake.
Tunajua Mlimani kuna shida; ukiwauliza vijana watakwambia jongoo hapandi mtungi.
Siwaonei, umewaona wanawake wakiandamana kwa matawi kudai haki yao ya nyuma ya pazia.
Badala ya wazee waliowazaa vijana wasiojiweza kuwawezesha kwa maarifa – mathalan kuwaelekeza ziliko ‘kukumanga’ – wamekuwa viguu na njia.
Nimekuwa nikishangaa iwapo wazee maskini hawazeeki kwa maana sijawahi kumsikia yeyote kijijini kwetu amejiunga na baraza la wazee.
Baraza hilo – ambalo halijachaguliwa na yeyote ila hujifanya kana kwamba ndilo mmiliki wa Kenya, wengine ni wapangaji – hujumuisha wazee walio na vyao, japo vichache.
Wasio navyo hubaki nyumbani kama watoto, nao huungana na hao waliolemaa kunywa pombe haramu na kulaza damu kwa jumla.
Nimeuliza iwapo wauza mahindi wakizeeka hujiunga na baraza la wazee kwa sababu kila wakati humpata wa kwetu anapouzia.
Hata juzi hakuhudhuria mkutano ulioandaliwa Nyeri kumtukana Dkt Samoei, mteja mkubwa wa mahindi-choma.
Ukimtukana Dkt Samoei kumfurahisha ‘Kamwana’, kumbuka mwenyewe alimtukana ‘Baba’ kumfurahisha ‘Kamwana’ pia.