• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:55 AM
KINAYA: Matajiri watumie noti za Sh1,000 kujitakasa kwa kusaidia maskini

KINAYA: Matajiri watumie noti za Sh1,000 kujitakasa kwa kusaidia maskini

Na DOUGLAS MUTUA

HEBU tutakase pesa jamani!

Kivipi? Si huo ni uvunjaji sheria? Na tukishikwa? Tukienda jela wake na watoto wetu watatunzwa na nani?

Nina jawabu: Wake watapata waume wengine, waishi vyema kuliko walivyoishi nasi waja watundu, nao watoto watakuzwa na Mungu tu.

Kisa na maasa? Tunataka kutakasa pesa zote chafu – kana kwamba kuna pesa safi – zinazoenea nchini na kuharibu uchumi ili zidhibitiwe, kila mmoja apate zake halali.

Samahani msomaji, najua unasikia kama haya ni mambo ya kufikirika tu, yanayoendelea kwenye nchi ya kusadikika.

Hapo nimekuelewa; huwezi kutakasa pesa ambazo huna, hivyo humo kwenye hilo kundi la watakasaji.

Kundi lenyewe lina nyingi, nyingi tu za kuajabiwa ambazo nina hakika ukiziona utazimia kwa mshtuko.

Ni watu walio na pesa za aina hiyo amboa ninarejelea, si makabwela. Hata hivyo, maskini pia ni mtu, tena wa Mungu, na ndiyo sababu hajatoweka duniani.

Wazo langu ni kwamba uamuzi wa Serikali wa hivi majuzi kuondoa noti zote za Sh1000 katika muda wa miezi minne ni fursa safi kwa wezi na walaghai kujitakasa.

Bila shaka wakibeba mabunda ya manoti ya kuyapeleka benki watashikwa na kuishi jela kwa muda mrefu, hivyo ni lazima watumie akili.

Muhimu ni kujitakasa kwa kutakasa pesa zao chafu, wabaki safi kama pamba na wawe na matumaini ya kwenda mbinguni siku ya kiama ikifika.

Kivipi? Badala ya kuzipeleka benki na kuvishwa pingu na sare ya jela, au kuziacha ziozee majumbani kwao, ni heri watugawie kila mtu angaa nusu milioni!

Sisemi watuite kikao cha hadhara eti kila mtu apate zake, la hasha! Wakifanya hivyo tutashikwa sote, wao walipe dhamana na kutoka jela, mimi nawe tufie humo!

Njia rahisi ya kujitakasa pamoja na pesa zao ni kufanya hisani kama vile kujenga shule na kuchimba visima vya maji huko Tseikuru au Turkana, wafadhili na kilimo.

Na wasikome hapo! Wanaweza kuamua kwenda kila kijiji wakijengea maskini nyumba, watu wanaoishi mitaa ya mabanda waache kunyia karatasi za sandarusi na kuzipeperusha hewani hadi katikati ya barabara tunakopitia.

Kwa kufanya hivyo, mazingira yatakuwa yametunzwa vizuri, maskini watakuwa na furaha, nao wahisani hao watakuwa wamerejesha walivyotuibia na hivyo watasamehewa.

Mishahara midogo

Ni fursa nzuri pia ya kujitakasa kwa Wahindi, Waarabu na Wasomali ambao huajiri watu wetu na kuwalipa mishahara ya Sh3,000 kwa mwezi.

Hii ndiyo njia rahisi kabisa kwa maana haichoshi; mwajiri anahitaji kumpa mfanyakazi hundi ya kila mwezi ya Sh3,000 kisha amwongezee bakshihi ya Sh297,000!

Ikiwa wewe hulipwa Sh3,000, tajiri wako akiamua kukulipa laki tatu katika muda wa miezi minne ijayo atakuwa amepunguza umaskini kwenu.

Hata ukiamua kwenda kulewa ni sawa tu, mwenye baa atakuwa amepata mteja mpya, hivyo chupa zake za bia hazitapata vumbi kwa kukosa wateja.

Unaweza kudharau wazo langu la kuwapa fursa ya kujitakasa watu wote walio na mafedha yasiyojulikana, lakini kwanza jiulize kwa nini wanayaficha.

Msamaha wa dhambi ya kuiba ni kurejesha ulichoiba ukaondoka hatiani rafiki yangu. Tuzidi kuombeana.

[email protected]

You can share this post!

DONDOO ZA HAPA NA PALE: Deti na binti ya bosi yamletea balaa

MWANASIASA NGANGARI: Kiongozi aliyetimua Jaramogi kupitia...

adminleo