Makala

KINAYA: Ng’ombe sasa watapata vyeti vya kuzaliwa kabla ya Wakenya wengi!

July 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na DOUGLAS MUTUA

WEWE kaa hapo ukidai hujui ulizaliwa tarehe ngapi; kuna ng’ombe wanaojua siku zao za kuzaliwa!

Endelea kuduwaa hapo, utasikia kunaandaliwa sherehe za ‘mazazi’ ya ng’ombe!

Hivi nikuulize, siku ya mwisho ulipofanyiwa sherehe za mazazi ni lini? Mwaka gani? Ama hujawahi kuwa na sherehe za ukumbusho wa siku uliyozaliwa?

Najua umeanza kusonya, kunitusi na kusema eti hiyo si desturi ya Mwafrika, mara ni ubadhirifu wa matajiri, sijui ni maringo ya watu wa Nairobi, na mambo kama hayo.

Ajabu, mtoto wako au wa jamaa zako alifanyiwa sherehe hivi majuzi ilhali yeye wala wazazi wake si wazungu na hawaishi Nairobi. Unachekesha.

Samahani ikiwa nimekuchokoza. Lakini visingizio vya Wakenya waliokula chumvi vinaudhi. Wengi wanalipuuzilia mbali suala hilo la siku ya kuzaliwa.

Wengi hawajui haswa walizaliwa lini; ithibati ya pekee kwamba walizaliwa ni kuwa wangali nasi, wanapumua.

Hoja kuu hapa si kuzaliwa au kutozaliwa bali ni ile ithibati ya serikali – cheti cha kuzaliwa – ambayo mtu hupewa kuthibitisha kweli mazazi yake yalirekodiwa rasmi.

Miaka kadhaa iliyopita hakuna aliyejali kuhusu cheti hicho kwa kuwa hakikuhitajika mahali kwingi isipokuwa ofisi ya kuchukua pasi ya kusafiria.

Waliosoma kabla ya cheti hicho kuwa miongoni mwa vitu vinavyohitajika ili mtu asajiliwe kufanya mtihani, watakwambia hawakukihitaji, kitambulisho cha kitaifa kilitosha.

Ni kwa sababu hii ambapo utapata watu wengi hawajui siku hasa walizozaliwa. Kumbuka hilo ni rika ambalo liko hai kwa mapenzi ya Mungu.

Naam, kwa sababu mpaka sasa sielewi watu ambao walizaliwa vijijini bila msaada wa madaktari wala wauguzi waliponea kivipi.

Ni kwa kudura za Mwenyezi Mungu na bahati za wakunga wasiojua kusoma na kuandika waliowasaidia wajawazito kuutua mzigo mzito – wewe!

Kumwambia mkunga wa siku hizo akukumbushe siku uliyozaliwa, kana kwamba wewe pekee ndiwe waliyezalisha, ni kutumia akili kizembe.

Na bila shaka mama yako hakuwa na msukumo wa kuijulisha serikali eti umezaliwa; hangemwongezewa sufuria ya ugali.

Tena, mwakilishi wa serikali ambaye mama yako angejulisha kuhusu mazazi yako ni chifu, maskini mwingine wa Mungu asiyejua alizaliwa lini.

Uganda

Huku Kenya ikiwa na mamilioni ya watu wasio na vyeti vya kuzaliwa, jirani yetu ameanza kuwapa ng’ombe wote vyeti hivyo.

Mambo yakiendelea yanavyokwenda, labda hivi karibuni utawasikia ng’ombe wa Uganda wakiitana kwa majina.

Museveni, mwana wa Esitari, ameamua ng’ombe wote wapewe vyeti hivyo, kila mmoja ajulikane alizaliwa lini.

Hataki kubahatisha eti.

Kwa manufaa gani? Mwana wa Esitari anataka awanogeshee Waganda biashara ya kuuza ng’ombe wa nyama nje ya nchi.

Wateja wa ng’ambo wamesema hawawezi kula ng’ombe aliyezidi umri wa mwaka mmoja. Huyo kwetu si ni ndama?

Hao achana nao, mahitaji yao ni ya ajabu na huzidi kila wakikutana na kibaraka kama mwana wa Esitari.

Huku kwetu nasikia walimwambia mwana wa Jomo eti tusilime kwa mbolea ya mifugo, watatuuzia ya dukani.

Akikubaliana nao nitamwita kibaraka.

Tunapaswa kuishi maisha yetu, si kuishi kama vinyago vya waliotutawala na kutuacha pabaya.

[email protected]