KINAYA: 'Tangatanga' wamebwagwa sasa wakubali yaishe tufuate mengine!
Na DOUGLAS MUTUA
WATU wa ‘Tangatanga’ wameanza kutumia akili kama kofia!
Sijui ushindi wa Kibra umewakaaje. Labda hawakutarajia kichapo cha namna hiyo, lakini hiyo si hoja.
Na niliwaonya tangu zamani, nikawaambia wadumishe ushindani wa kisiasa wenye upeo wa juu si kucheza mchezo wa pata potea ambao ‘Baba’ hupenda kushiriki mara nyingi.
Juzi nimejipata kwenye njia panda, sijui niudhike au nicheke kuhusu kelele walizotoka nazo Kibra wafuasi wa ngazi ya juu wa kinara wa mrengo wa ‘Tangatanga’, Dkt Samoei.
Baada ya kushindwa vibaya na kuandamwa kwa matusi na dhihaka na lile kundi kali la ‘Baba’ lenye wabunge ‘wachanga’ na watundu, ‘Tangatanga’ walilia kuhusu maridhiano.
Yepi hayo? Yaleyale tu unayoyajua, chimbuko la mkono wa maridhiano waliopokezana ‘Baba’ na Jomo mdogo, wakamshtua kila mtu, ila zaidi Dkt Samoei.
Kilio cha ‘Tangatanga’ – ambacho hakikutoa machozi yoyote kwa sababu ni cha kiume na mwanamume Mwafrika anayelia angali anatamani titi la mama – kilielekezewa ‘Ouru’.
Walimshinikiza mwenyeji huyo wa Ikulu atafakari sana kuhusu uhusiano wake na ‘Baba’, zinakotupeleka juhudi za maridhiano zilizobatizwa BBI, kisha aamue iwapo bado anataka kuendelea kuwa rafiki wa ‘Baba’ na ODM yake.
Kilichowaudhi zaidi wafuasi wa ‘Tangatanga’ ni kwamba vijibwa wa ‘Baba’ vilibweka sana, tena kwa sauti kuu na ukali wa kupigiwa mfano, vikamsihi mkuu wao akae macho.
Eti nini? Akae macho aone nini? Eti asiyapepese wala kusinzia hata kidogo amkabili ‘Ouru’ kisawasawa hadi 2022 ili awape kitu ambacho wametafuta tangu jadi; Ikulu.
Na akiwacheza? Liwe liwalo eti, chochote kitokee, wakosane naye papo hapo, urafiki wake na ‘Baba’ uishie hapo! Kisha? Labda uwe mwisho wa dunia, Yesu aturudie.
Mengine yaliyobwekwa na vijibwa wa ‘Baba’, hasa mwanamke fulani ambaye jina lake nimelibana nisimkweze na kutukuza uozo wa kinywa, hayaandikiki yakachapishika.
Hata hivyo, mimi hayakuniudhi. Yaliniburudisha, hasa kwa maana sikuwa na mwanangu nikiyatizama kwenye runinga au kuyasoma magazetini.
Mengi yaliaibisha, hivyo nilijifungia chumbani peke yangu. Hiyo ni mbinu yangu ya kuwalinda wanangu dhidi ya watu wazima walio na tabia za kitoto.
Nilicheka tu kama nilivyokuahidi. Naam, niliwacheka mibabe wa ‘Tangatanga’ wakilialia na kushinikiza urafiki wa ‘Baba’ na Ouru uchunguzwe upya. Utadhani waliushabikia tangu mwanzo.
Nimekwambia nusura niudhike kwa kuona hoja za malalamiko walizotoa Tangatanga. Mwanasiasa mwenye uzoefu wa kutosha halalamiki eti ametukanwa.
Ukiwa mwanasiasa, ushindwe na matusi ya hadhara, heri urudi kwako nyumbani ukakae na mkeo.
Na nakuhakikishia hata huko utatukanwa tu. matusi yako kila mahali.
Tangatanga wana hakika gani kwamba vijibwa wa ‘Baba’ hawakupata baraka za Ouru kuwatukana? Kumbuka ‘Baba’ na ODM yake waliingia serikalini kimyakimya, hatuna upinzani.
Huenda Tangatanga wakiungulika kwa kutukanwa, Ouru akijichekea ovyo ndani ya Ikulu na kujipongeza kwa kuwachapa kwa mbali na kuficha ushahidi kwamba alihusika.
Unahitaji kuwa na hakika sana ukimwambia mwanasiasa akutetee kwa kuchezewa visivyo na mwanasiasa mwingine; labda hiyo ni njama yake.
‘Tangatanga’ wajifute machozi, wajipanguse vumbi walilotifuliwa, warejee uwanjani na kuzichapa tena na ODM na, ikibidi, Ouru. Machozi ni ya wanawake. Namnukuu babu.