KINAYA: Uzalendo wa bendera umeongeza wananchi sufuria ngapi za ugali?
Na DOUGLAS MUTUA
HIVI nikuulize, unawezaje kutetea tambara liitwalo bendera ilhali huna hata kitambaa cha kufutia kamasi?
Na majasho yanayokutoka? Huna hata kitambaa cha shati au suruali kuukuu angaa ukayafuta na kuendelea kutufokea kuhusu uzalendo?
Ngao ya kitaifa, ile sanamu ya kuchongwa kutoka mtini au kuundwa kwa mabati, inakupa fahari gani ikiwa unalala mabandani ambako hujua uko hai ukiamka asubuhi?
Uzuzu tunaoshuhudia nchini Kenya unatia hofu. Naam, kutia hofu hasa, pamoja na kusikitisha.
Kisa na mkasa ni kwamba tukiendelea hivi, utakutana na kiwiliwili cha mtu kikitembea bila kichwa; kuna ishara Kenya kuna watu walio na uwezo wa kuishi bila akili.
Kusikitisha, ndio, kwa sababu ni lazima anayeishi bila akili anapitia maisha magumu kupindukia. Yaani, kuwa na ombwe tupu kichwani, ukalazimika kusubiri hadi watu wakufikirie ni mateso tele, au sio?
Mjadala duni unaendelea, kuhusu heshima kwa bendera ya taifa, ngao yake na sanamu nyingine ambazo tulisoma kuzihusu tukiwa shule za msingi.
Mjadala huo ungeendelea miongoni mwa walalahai singejali kwa maana wao ndio wanaojua manufaa ya kuwa Mkenya.
Maisha kati yetu na matajiri, pamoja na hao unaopenda kuita viongozi, ni tofauti sana. Wao wakitaka hiki wanapata, wewe ukikitaka unafukuziwa mbali kama mbwa koko!
Uzalendo wa bendera ungekuwa kitumbua tungekuwa tumewalisha watoto wetu kitambo sana. Hata watu waliokufa njaa huko Turkana juzi wangekuwa wameutafuna.
Lakini ni hewa tu, hadaa ambayo inatia aibu kwa sababu wanaoieneza washapata, wanaoiamini hawajui ‘be’ wala ‘te, na wote wanazunguka mduara usio na mwisho.
Uzalendo wenye tija ni ule ambao unaenziwa na kila mtu – mtawala na mtawaliwa – si chombo cha kuwanyanyasa watu, kuwaasi kiakili haswa, wala kuwanyonya damu.
Naam, si uzalendo wa watu kujiongezea mishahara na marupurupu ya kila aina huku maskini akiendea miayo kijijini na kufia huko kwa njaa na maradhi.
Ni uzalendo wa kufukuza ujinga, maradhi na umaskini, wananchi wakaishi kwa raha, wakajihisi wana nchi ya kuita yao.
Hebu tuulizane: Ulipokuwa skuli, bendera yenu ilikuwa maridadi kila wakati au ilichakaa na kuchanika kama tambara lililovaliwa na kichaa akachoka?
Mapema
Mwanzoni, bendera yetu ilichujuka rangi kabisa kisha ikachanika kadri ilivyopeperushwa na upepo, hatimaye ikafanana na kamisi iliyovuliwa na kichaa na kutupwa sokoni, akaja kichaa nafuu akaiokota, akaiosha na kuipandisha tena!
Nakumbuka kuna siku ambapo hatukupandisha bendera yoyote siku ya Ijumaa kama ilivyokuwa kawaida kwa sababu tambara lenyewe lilikuwa limekwisha.
Tulibahatika tulipochangiwa na shirika la bahati nasibu, Charity Sweepstake, tukanunua bendera na kuhisi kama tuliopata uraia wa Kenya upya.
Hivyo ndivyo tulivyokorogwa akili na watawala weusi wa nchi hii tukaamini kwamba bila bendera hatutoshi, ndiyo sababu unasikia makabwela wakisisitiza iheshimiwe.
Huko kwa kuheshimu tambara kulitokwa zamani! Ikiwa huwezi kunitimizia mahitaji ya kimsingi niliyokuchagulia, huo wimbo wa bendera kawaimbie walevi wenzako mkishapewa mbili-tatu.
Wamarekani wanashona chupi na soksi, labda hata sodo, kwa bendera yao. Na uzalendo wao haujapungua. Huu utapeli wa kimawazo ni lazima ufike mwisho.