Makala

KINAYA: Wanaojigamba kuhusu Kibra wataambia nini watu Alhamisi?

November 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na DOUGLAS MUTUA

ALHAMISI ijayo nitacheka nusura niteguke mbavu!

Naam, nitaangua kicheko kikuu kuwacheka makabwela na mabwana wanaowatumia kaka viko ambavyo hupakua mchuzi wala havili kamwe.

Lakini kicheko hicho kitaongezeka zaidi nikiwakumbuka wanasiasa na wakuu wa vyama vya kisiasa, watu ambao hujibeba kamna walioshuka duniani kutoka mbinguni ili mimi nawe tuwatumikie.

Lakini, kwa nini kicheko hicho kisubiri siku nne? Mbona nisicheke hata sasa hivi ikiwa ni raha hivyo kuwacheka watu hao?

Huna habari? Kwani unaishi dunia gani? Mbichi na mbivu kuhusu mshindi na mshinde wa uchaguzi mdogo wa Kibra zitajulikana Alhamisi!

Siku hiyo, kabla hujalala – na hili ni sahihi ikiwa hulali mapema kama kuku – utakuwa umejua mshindi ni mwanasoka wa zamani McDonald Mariga au Imran Okoth.

Nimewataja hao kwanza kwa maana ndio wanaoibeba mienge ya Jubilee na ODM katika sanjari hiyo, na bila shaka unajua vyama hivyo viwili vilivyotukosesha usingizi.

Najua pia yupo Eliud Owalo wa chama cha African National Congress (ANC) kinachoongozwa na ‘MaDVD’, na kwa hakika hata yeye anaweza kushinda, ila simjali.

Lakini kwa nini nisimjali Bw Owalo, mtu ambaye aliwahi kuwa msaidizi wa karibu wa ‘Baba’ aliyekuwa na ushawishi wa kupigiwa mfano siku hizo?

Nimeamua kumopuuzilia mbali kwa kuwa mkuu wake, Bw MaDVD, hazidishi hapunguzi chochote kwenye siasda za Kenya. Awepo, asiwepo, tutapiga siasa tu. Hatumkumbuki!

Hata hivyo, siwezi kusema hivyo kuwahusu masogora wakuu wa siasa nchini – Dkt Bill Kipchirchir Samoei na ‘Baba’ – ambao wakipiga chafya tu sote hupata mafua ya kisiasa.

Ama kweli, kicheko ninachonuia kuangua kinawalenga wawili hawa. Bila shaka nitamcheka mshinde kati ya Mariga na Imran au woteb wawili wakibwagwa na Owalo.

Lakini nitawacheka Dkt Kipchirchir na ‘Baba’ zaidi kwa kuwa wametuapia eti matokeo ya Kibra yataashiria mambo yatakavyokuwa kwenye uchaguzi wa urais ifikapo 2022.

Je, wawaniaji wao hao, Mariga na Imran, wakibwagwa na Owalo, nitawacheka Dkt Kipchirchir na ‘Baba’ nikidhani watafyekwa na MaDVD hapo 2022?

La hasha! Hilo haliiwezekani! Kwa maoni yangu, MaDVD bado hajaiva. Hata alipodhani kaiva, akajaribisha kwenda Ikulu, ‘Baba’ alimshinda kwao magharibi. Nitampuuza.

Alhamisi nitaangalia ni nani aliyepata kura ngapi kati ya wawaniaji wa Jubilee na ODM kisha nimcheke aliyepungukiwa, nimpe changamoto ya kutueleza utabiri wakwe.

Hakuna kitu kibaya kama kutanua kifua kwenye ulingo wa siasa, ambao huwa kama kamari hatari ambayo matokeo yake hayajulikani.

Anayejitapa atakavyomshinda mwenzake, hata kwa kutishia tu, hujiweka katika hali hatari ya kufedheheshwa na kuchekwa mambo yakimwendea sivyo.

Juzi ‘Baba’ amewaambia wafuasi wake walioko Kibra kwamba, hata kama hawampendi Imran, wampe kura zao kwa kuwa wanampenda ‘Baba’ mwenyewe. Sijui ana hakika gani.

Aliwaambia hiyo ya kumshinda Mariga ni kazi rahisi wanayoweza kufanya peke yao huku yeye akiendelea kumsaidia Ouru kutawala nchi. Uchokozi dhidi ya Dkt Kipchirchir huo!

Dkt Kipchirchir mwenyewe ametangaza kuwa Mariga ni mwaniaji wa Serikali, kumaanisha hata Ouru anamuunga mkono, hivyo kuhatarisha urafiki wa Ouru na ‘Baba’. Wazichape kwa raha zao ila watuachie nchi bora kuliko walivyoipata.

 

[email protected]