KIPATO: Biashara ya maji inavyoinua vijana
Na SAMMY WAWERU
NI mwendo wa saa tano hivi za asubuhi tunampata Samuel Ng’ang’a akiwa katika harakati za kupanga mitungi ya maji.
Ana zaidi ya mitungi 60, pembezoni akiwa na ‘kijigari’ maalum cha kuisafirisha, maarufu kama mkokoteni.
Ni shughuli anayoiendeshea eneo la Toezz, Progressive, Mwiki na Chuma Mbili, mitaa hiyo ikiwa kaunti ya Kiambu na Nairobi.
“Uchuuzi wa maji umenifaa na kuniinua kimaisha,” asema Samuel.
Upungufu wa maji kaunti ya Nairobi, Kiambu na katika baadhi ya maeneo nchini, unaendelea kuwa kero.
Ili kunusuru wananchi haswa wenye shughuli tele kuzimbulia familia zao riziki, baadhi ya vijana wamejituma katika gange ya uuzaji wa maji. Aidha, wanapelekea wakazi au wapangaji raslimali hii muhimu katika makazi yao kwa ada.
Ni muhimu kutaja suala la ukosefu wa ajira nchini limeendelea kuhangaisha vijana. Kila mwaka katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya vijana, mamia na maelfu wanafuzu kwa vyeti mbalimbali vya elimu.
Licha ya serikali kuahidi kubuni zaidi ya nafasi milioni moja kwa mwaka nchini, hilo limekuwa kitendawili kinachokosa wa kukitegua.
Hivyo basi, vijana wenye maono hawana budi ila kujituma kufanya kazi halali zinazojiri badala ya kujihusisha na uhalifu.
Katika hilohilo, Samuel Ng’ang’a hajutii uamuzi wake kuchuuza maji Nairobi na Kiambu. Isitoshe, anadhihirishia serikali kwamba si lazima iajiri kila mmoja kwani nafasi zenyewe ni finyu, hazipatikani na zinazopatikana zinaendea wachache.
Kijana huyu alifanya mtihani wa kitaifa kidato cha nne, KCSE mnamo 2014. Samuel ambaye ni mzaliwa wa Nyeri, anasema kwa kuwa wazazi wake hawakuwa na uwezo kifedha kumsomesha chuo kikuu au taasisi ya juu ya elimu alihamia Nairobi kusukuma gurudumu la maisha.
Uuzaji wa maji ndiyo kazi iliyomkaribisha, na kwamba aliajiriwa kwa muda wa miezi sita pekee akafanikiwa kujisimamia.
Kulingana na Samuel 25, ilimgharimu mtaji wa Sh1,500 pekee kuwekeza katika biashara hii ambayo imenoga. Aidha, alinunua mitungi ipatayo 15 ya lita 20 kwa Sh80 kila moja.
“Fedha zilizosalia nilizitumia kununua nazo maji na kazi ikaanza hadi wa leo,” asema barobaro huyu. Anaendelea kueleza kwamba kando na kumfungulia awamu nyingine ya maisha, hatua ya kuajiriwa ilimuwezesha kupata wateja.
Uaminifu kwa wateja ndiyo hulka iliyochangia kazi yake kuimarika.
“Katika biashara yoyote ile, wateja wakikosa imani nawe, watakutoroka mmoja baada ya mwingine. Hiyo ndiyo sababu biashara nyingi hufifia na kufilisika,” ashauri Bw Samuel.
Mtungi mmoja haupungui Sh20, msimu wa kiangazi ukipanda hadi Sh50. Anasema huuziwa Sh5, kila mmoja kutoka kwa wenye mabomba au mifereji ya maji.
Ukizuru mitaa mbalimbali Nairobi na Kiambu, hutakosa kutazama mikokoteni yenye mitungi ya maji, na licha ya ukosefu wa raslimali hii muhimu kuwa changamoto kuu, vijana wameweza kujiajiri na kujaribu kuitatua.
Michael Muriuki, mhasibu na mchanganuzi wa masuala ya kiuchumi, anasema inachopaswa kufanya serikali ni kuyafanya mazingira ya biashara nchini kuwa bora. Anasema vijana wengi wamelemewa kuwekeza katika biashara kwa sababu ya mazingira yenye pandashuka chungu nzima zinazohusishwa na idara husika.
“Kwa mfano, kupata leseni au cheti cha kuweka biashara imekumbwa na ufisadi. Halmashauri ya jiji, inahangaisha wafanyabiashara hususan wale wadogo na wanaojaribu kupulizia biashara zao kuimarika,” aeleza Bw Muriuki.
Isitoshe, serikali hiyohiyo inategemea ushuru kutoka kwa wafanyabiashara wadogo, wale wakubwa wakikwepa.
Kijana Samuel anasema kila siku hulipia ada ya Sh20, ushuru, na kwa mujibu wa mtaalamu Muriuki mkondo huohuo unapaswa kufuatwa na mabwanyenye wenye makasri ya biashara.
Mdau huyu hata hivyo, anashauri Samuel kuwa na malengo makuu katika siku za usoni, akimhimiza apanie kuwekeza katika upakiaji wa maji kwenye chupa. “Ni muhimu ajue itawadia wakati upungufu wa maji utatatuliwa. Alenge kufungua kiwanda cha kupakia maji ya chupa,” asema.