• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 5:01 PM
KIPWANI: Aliota akiwa msanii sasa ndoto imetimia

KIPWANI: Aliota akiwa msanii sasa ndoto imetimia

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

ALIOTA akiwa mwimbaji na sasa imetimia.

Tarsila Rogert al-maarufu Joe Mosha anasema alipenda kuimba tangu alipokuwa mtoto wa umri wa miaka 12 akiwa darasa la sita ambapo mara kwa mara alijikuta akiimba nyimbo za Injili haswa usingizini.

“Ni sababu ya ndoto hizo niliamua nitakuwa mwimbaji, tena nyimbo nitakazoimba ziwe zile za kumtukuza Bwana,” asema Joe Mosha.

Wasaka umaarufu na pesa au lengo tu ni kumtukuza Mungu?

Joe Mosha: La hasha, si pesa. Naimba kwa sababu ni wajibu wangu kumtumikia Mungu na kuongoza waja kwake. Siimbi kwa sababu ya kujitajirisha.

Ikiwa ni hivyo, riziki yako unaipata kwa njia gani?

Joe Mosha: Namshukuru Bwana kwani napata riziki yangu ya kila siku kutokana na biashara yangu ya kuuza chakula ndani ya soko la Majengo, mjini Mombasa.

Una nyimbo ngapi, zipi na zimeitikiwaje?

Joe Mosha: Nina nyimbo nyingi lakini zile ambazo nimezirekodi hadi sasa ni mbili; Unaweza na Nipe Subira. Mashabiki wamezipokea vizuri na Unaweza sasa upo YouTube. Natumai kuachia ngoma zaidi mwaka huu.

Una nia ya kufika wapi kimuziki?

Joe Mosha: Nataka nitambulike Afrika kwa nyimbo zangu lakini si sababu ya kujitajirisha.

Kwa nini hukufikiria kuimba nyimbo za kilimwengu?

Joe Mosha: Kama nilivyokueleza, nilikuwa naota ndoto nikiimba na kumsifu Mola na ndiyo sababu nikajikita kwenye fani hii.

Ni waimbaji gani wa Injili wanakukosha?

Joe Mosha: Kina Jennifer Mghendi, Martha Mwaipaja, Christina Shusho, wote wa Tanzania na Gloria Muliro wa Kenya. Nazipenda nyimbo zao ambazo zinanipa moyo mkubwa wa kujitahidi kuendeleza kipaji changu.

Unawaambia nini wenzako wa Injili na wale wa kilimwengu?

Joe Mosha: Nawaomba waimbaji wa Injili wasikate tamaa kutokana na majaribu mengi wanayoyapata, wajitie moyo na kusonga mbele kwa imani kuwa siku moja watafaulu. Hawa wa kilimwengu nawasihi waangazie jumbe zenye maadili.

Unawaambia nini mashabiki wa nyimbo zako?

Joe Mosha: Nawapenda sana, Mungu awabariki kwa kusikiliza nyimbo zangu na natumai zinawakosha moyo.

Una chochote unachoandaa hivi sasa?

Joe Mosha: Nina kibao cha Amenena Nami ambacho nitakizindua maalum kwa kumuombea Mungu shangazi yangu ambaye ameugua kwa kipindi kirefu.

You can share this post!

DOMO KAYA: Kumbe ni kutuchocha tu!

SHANGAZI AKUJIBU: Baba halisi anadai mtoto niliyelea miaka...

adminleo