KIPWANI: Malkia wa Kimaasai aliyetokea Bongo Star Search
Na ABDULRAHMAN SHERIFF
ALIKUWA mmoja wa wasanii waliokuwa tishio kwenye mashindano ya kila mwaka ya Bongo Star Search, ila baadaye aliamua kubadilisha na kujitosa kwenye nyimbo za Injili.
Jina la Karen Kimaren kwa wengine huenda likawa geni lakini kwa wanamuziki wa sehemu karibu zote za Pwani na hasa wa Kaunti ya Taita Taveta, wanamfahamu kama Malkia wa Kimaasai mwenye sauti nyororo na ya kupendeza.
Wengi wanamtambua kwa kibao chake kinachoitwa On fire cover ambacho alikizindua rasmi mapema Januari, mwaka huu; wimbo aliouimba kwa ufundi kiasi cha kumjazia sifa kedekede hadi kusajiliwa miongoni wa wasanii watakaoimba katika Tamasha kubwa la Muziki hapo Aprili linalojulikana kwa jina la Taveta Fiesta.
Karen ametoa wito kwa wadhamini wajitokeze kuwasaidia waimbaji wa nyimbo za Injili kwa sababu wanastahili kuimba nyimbo za kuwavutia wapenda muziki kufuata nyendo zinazofaa.
Safari yako ya kimuziki ulianzia wapi?
Karen: Ilianzia kanisani huko Gilgil nikiwa pamoja na ndugu zangu ambapo tulifanikiwa kuunda kundi lililoitwa The Kimarens ambalo hata hivyo tulitengana kutokana na kila mtu kushika shughuli zake. Wale ambao walikuwa wangali wanafunzi hivi sasa wanapania kulifufua pindi mambo yatakaponyooka.
Ulipoanza kujitosa kwenye fani hii ya muziki, mambo yalikuwaje?
Karen: Kama wahenga walivyosema hakuna kazi bila changamoto, nami licha ya kuwa na kipaji nimepitia changamoto nusura nikate tamaa maana si mara moja nimewahi kufukuzwa studio kwa ukosefu wa pesa za kulipia. Kuna baadhi ya maprodusa walikua wakinitaka kimwili, lakini sikukubali sababu ya kulinda hadhi yangu.
Kuna produsa aliyekukubalia kufanya kazi naye na akakuwekea heshima?
Karen: Namshukuru mtayarishaji wa muziki Kryptonia huku video zangu zikisimamiwa na Mkurugenzi Pitcraizy ambaye tunaheshimiana na kufanya kazi kwa njia mwafaka chini ya Taveta Sanaa Studio inayomilikiwa kwa uangalifu na Deejay Kichi.
Wazazi wako walikuruhusu kujiingiza fani ya muziki?
Karen: Wazazi wangu walinipa radhi na hata kuniunga mkono. Ingawa sijapata mfadhili, namshukuru mjomba wangu mbali na kuwa na majukumu, ananisaidia kwa malipo ya kurekodi nyimbo zangu.
Kwa nini ulikwepa muziki wa kisasa na kuamua kujitosa muziki wa Injili?
Karen: Sababu kubwa iliyonifanya nivuke sakafu hadi muziki wa Gospel ni kuwa nimeona kuwa na wajibu wa kumtumikia Mungu ambaye ndiye aliyenifanya niwe na talanta ya kuimba.
Vibao vyako vya nyimbo za kisasa vilikuwa vipi na umetumia mitindo gani?
Karen: Vibao vyangu vya nyimbo za kisasa ni Romain Virgo niliyotumia mtindo wa Reggea na On fire cover ambayo niliimba nikitumia mtindo wa Slow dance.
Kwa upande wa Injili, umetoa kibao chochote?
Karen: Najitayarisha kutoa kibao changu cha kwanza ambacho nitakipa jina mara nitakapokamilisha kukirekodi na kwa nyimbo zangu za mwanzo, natarajia kutumia mitindo ya Bongo Fleva ambao ndio unpendewa na wapenda muziki.
Unawaambia nini wanamuziki wa Injili?
Karen: Nyimbo za Injili zinahusu na kumsifu Mungu, hivyo tusichanganye na nyimbo za dunia na tusizifanye kuwa za kibiashara bali ni kueneza Neno.
Unawaambia nini mashabiki wa muziki wako?
Karen: Ninawashukuru kuniunga mkono wakati nikiimba nyimbo za kidunia. Sasa wanifuate kwa nyimbo zangu za Injili.