• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 1:14 PM
KIPWANI: Usistaajabu wasanii tele wa injili, ni Neno

KIPWANI: Usistaajabu wasanii tele wa injili, ni Neno

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

KUNGELIKUWA na wasanii wengi wenye vipaji mkoani Pwani endapo vyombo vya habari vingelikuwa vikiwaangazia wasanii wa nyumbani kwao.

Ndiyo kauli ya msanii Flora Makumbi ambaye ni miongoni mwa wasanii wa Pwani.

Anaamini kama wangelipata usaidizi wa kuandika, kupiga na kuonyesha nyimbo zao, mkoa huo ungeliongoza kwa wingi wa wasanii wenye vipaji.

Flora anasema karibu aache kuimba lakini mumewe alimpa moyo mkubwa wa kuendelea kuinua kipaji cha uimbaji wa nyimbo za Injili kwani alikuwa na uhakika iko siku atakuwa miongoni mwa waimbaji wenye tajriba kubwa ya nyimbo za kumsifu Bwana.

“Kutokana na moyo na usaidizi ninaoupata kutoka kwa mume wangu, nina matumaini makubwa kuwa utafika wakati nitaweza kuwa mwanamuziki mwenye kutajika na kuwa maarufu katika nyimbo za kumsifu Mungu,” asema.

Hebu tupashe ulianza kupenda muziki lini na wapi na nini hasa kilichokufanya ujitose huko?

Flora: Hakika sikuwa natambua kama nitajitosa katika fani ya muziki ila nilianza kuimba tangu nikiwa mdogo nikiwa pamoja na familia yangu ambayo ilikuwa ikiimba nyimbo za Injili kanisani. Hapo ndipo nilikutana na binamu yangu Huston Mwakio ambaye ndiye aliyenipa motisha wa kuanza kuandika na kuimba nyimbo ambazo zitaweza kusambaa zikiwa na ujumbe wa kumsifu Mungu.

Ulianza kutoa kibao chako cha kwanza lini na kiliitikiwaje?

Flora: Nilitoa album yangu ya kwanza ya Mwite Yesu yenye nyimbo nane mnamo mwaka 2013 lakini hizi hazikutamba kwa kuwa nilikuwa ndio mwanzo naanza na sikutambua njia mwafaka na nzuri ya kuzisambaza. Nilijaribu kupeleka kwenye stesheni za radio lakini niliyokuta huko, yalinishinda nikarudi kuimba kanisani.

Hebu tutajie nyimbo hizo nane zilizokuwa kwenye album ya ‘Mwite Yesu’?

Flora: Haya, nyimbo hizo ni Unanipenda, Mwite Yesu, Nakutegemea, Nakuabudu, Nakuamini, Aba Mlungu, Nifundishe na Maker of the Universe.
Ni lipi hasa lililokufanya ukarudi tena kuimba wakati tayari ulipata ugumu wa nyimbo zako kutumika kwenye stesheni za redio?

Flora: Ilikuwa mwaka 2015 ndipo nilipompata kitulizo cha moyo wangu ambaye alisisitiza kuwa ni muhimu nirudi kwenye sanaa hiyo ya muziki huku akinipa moyo kuwa nitaendelea na hilo naanza kulishuhudia.

Hebu tufahamishe hiyo album yako ya pili ni ipi, ina nyimbo zipi na uliitoa lini na yaendeleaje?

Flora: Albamu yangu mpya inaitwa ‘Mwaminifu’ ambayo ina nyimbo tano, Mwaminifu, Praise Him, Baba Oshe, Maskani na Have your way. Baadhi ya nyimbo hizo tumeziandika pamoja na mume wangu na niliitoa album hiyo wiki moja iliyopita.

Kitu gani katika muziki unatamani ama ulitamani kukitekeleza kikuridhishe moyo wako?

Flora: Jambo ambalo nilikuwa nataka kulitekeleza ni kuimba live na wakati huo huo kurekodi. Hilo nimefanikiwa kutekeleza na ndiyo hiyo album niliyoizindua wiki moja iliyopita.

Unatumia mitindo gani kwa nyimbo zako?

Flora: Mimi hutumia mtindo wa Gospel sababu ndio unaoshabikiwa na waumini wengi.

Kwa nini siku hizi kuna wanamuziki wengi wa Injili?

Flora: Ninavyofahamu ni kuwa wasanii wengi wameamua kurudi na kumtumikia Mungu. Pia ni njia mojawapo nzuri ya kuwapa mawaidha waumini watekeleze mazuri anayopenda Bwana.

You can share this post!

Wanasoka wa Gor Mahia kutemwa kwa utundu wao

Mhadhiri katika chuo kikuu cha MKU ashinda tuzo nyingine

adminleo