Kitendawili cha msitu wa Kirisia Samburu
Na GEOFFREY ONDIEKI
Maafisa wa polisi kutoka idara ya misitu (KFS) wameanza kubomoa nyumba (manyatta) za wakazi wanaoishi katika msitu wa Kirisia katika kaunti ya Samburu ili kupisha shughuli ya kuhifadhi msitu huo.
Taifa Leo Dijitali ilipotembelea msitu huo, ilibaini kuwa nyumba kadhaa za wakazi zimebomolewa na wakazi wengi wanakesha kwenye baridi ikizingatiwa uwepo wa sheria za kafyu na tishio la virusi vya Corona.
Hata hivyo, wakazi hawa wamelaani mbinu ambayo KFS inatumia kuwafurusha kutoka kwa msitu huo unaokisiwa kuwa mkubwa zaidi katika eneo la kaskazini mashariki mwa nchi.
Wanasema kuwa jamii inayoishi katika msitu huo wa Kirisia haikupewa ilani ya kufurushwa inavyihitajika kisheria.
Wanasema kuwa ubomozi wa nyumba zao ulianza ghafla na umeacha mamia ya wakazi bila makao.
Hata hivyo, hakuna visa vya purukushani na vuta nikuvute vimeripotiwa kati ya maafisa KFS na wakazi. Wengi waliozungumza na Taifa Leo walisema kuwa wanahisi kuwa serikali kuu pamoja na ya kaunti imewasaliti.
Sitili Lesingiran, mkazi ambaye boma lake lilibomolewa na maafisa hao, alielezea wasiwasi wake na kukiri kuwa familia yake imekesha kwenye baridi kwa siku tatu. Alitoa wito kwa serikali kuingilia kati na kusimamisha shughuli ya kuwafurusha maskwota mpaka janga la virusi vya Corona litakapoisha.
“Nimeishi kwenye msitu huu kwa miaka 25 sasa na sijui mahali pengine. Serikali ni ya watu wote lakini hii yetu haijali maisha ya watu wake. Tunahisi kusalitiwa na serikali yetu ya kaunti na ile ya kitaifa,” alisema Bw Lesingiran.
Bw Lesingiran, ambaye ni baba wa watoto sita, alikiri kuwa yupo tayari kuondoka msituni wakati janga la virusi vya Corona litakapoisha.
“Tutaenda wapi wakati Kama huu? Serikali inatangaza watu wakae nyumbani lakini sisi tunabomolewa zetu. Huu ni unyama kwa sababu tukianza kuzurura hapa tutaambukizwa virusi vya Corona,” aliongeza.
Alihimiza serikali ya kitaifa kupitia idara ya kutatua migogoro ya mashamba nchini kuingilia kati na kuwatafutia wakazi suluhisho la kudumu.
Mkazi mwingine Loyiamai Lengepei alishutumu serikali kwa kupeana amri ya kufurushwa kwao wakati huu taifa limekumbwa na visa vingi vya Corona. Alisema kuwa jamii zinazoishi katika msitu wa Kirisia zinahitaji muda zaidi kuhamia maeneo salama.
“Hatujakataa kutoka msituni lakini KFS wanatuhujumu Kama sisi sio wakenya. Tunahitaji muda zaidi kujipanga na tutaondoka,” alisema Bw Lengepei.
Hata hivyo, mkuu wa uhifadhi wa Ikolojia katika kaunti ya Samburu Eric Ochieng aliambia Taifa Leo kuwa KFS inawavurusha wakazi ambao wameingia msituni kinyume na sheria na kuishi mahali ambapo wengine walitoka kwa hiari.
Alisema kuwa wakazi wameingia na kujenga msituni miezi miwili tu baada ya serikali kutwaa zaidi ya ekari 1000 ya sehemu ya msitu huo, na kuwa KFS inawalenga wale ambao wameingia msituni bila kibali.
Aliongeza kuwa KFS bado inaendelea kuhamisha familia za wale wanahama kwa hiari.
“Wale ambao wanatolewa msituni kwa lazima ni wale ambao wameingia mahali wengine walitoka miezi miwili iliyopita na hatutakubali,” alisema Bw Ochieng.
Mnamo Disemba mwaka iliyopita, zaidi ya watu 5000 ambao waliingia msituni kinyume na sheria walitoka kwa hiari.