Makala

KIU YA UFANISI: Uuzaji kinywaji cha kahawa humpa zaidi ya milioni kwa mwaka

September 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LUDOVICK MBOGHOLI

SAIDI Mwajoha ni msanii wa ngoma za kitamaduni aliyezaliwa katika eneo la Rabai Kwa Mbadji, Kilifi, takriban miaka 35 iliyopita, aliyetegemea mapato ya usanii kujikimu kimaisha licha ya kupitia changamoto nyingi.

Hata hivyo, kadri maisha yalivyomwendea visivyo, ndivyo alivyofikiria mikakati mipya ya kumwezesha kujikimu kimaisha.

“Nilianza kazi ya usanii wa kitamaduni nikidhani ndiyo tegemeo la pekee maishani mwangu, lakini baada ya kuona mambo si mazuri, nilianza kutafakari upya malengo yangu,” aambia Akilimali alipohojiwa kwenye eneo lake la kazi.

Aligundua kuwa kazi ya usanii haidumu kama kazi nyenginezo, ndipo miaka 18 iliyopita akaamua kuanza shughuli ya kupika kahawa ‘thungu’ na kahawa tamu akichanganya na unga wa tangawizi kama jaribio lake la kwanza kibiashara.

Anasema, alipoanza upishi wa kahawa akitumia sufuria inayoweza kuchemsha lita sita za maji, ambayo ndiyo anayoitumia hadi wa leo, hakuwaza kuachana kabisa na usanii.

“Nilianza kuitumia sufuria hii yenye uwezo wa lita sita za maji, pamoja na gilasi 3 pekee kwa matumizi ya wateja wangu, lakini sikuwaza kabisa kuachana na usanii maana upo ndani ya damu,” Mwajoha apasha zaidi.

Anasema kwa sasa anatayarisha kahawa ‘thungu’ na kahawa tamu zaidi ya mara 10 kila siku kutokana na wingi wa wateja, hasa nyakati za jioni hadi mwendo wa saa nne za usiku.

“Wateja wangu ni wengi na nyakati za msimu wa baridi kali ndio naongeza zaidi viwango vya maandalizi,” aeleza akiwa maskani yake ya Kapelo Base.

Asema biashara yake ilichochewa na jamaa zake awali, walioizingatia ila baadhi walishindwa kuiendeleza. “Chimbuko la biashara hii ni jamaa zangu, walichochea ujuzi nilionao nikiwa nawafanyia kazi,” akiri Saidi.

“Kapelo Base ni maarufu hapa Mazeras, zipo maskani nyingi za kuuza kahawa, lakini hapa ni maarufu zaidi kwani wateja wanaomiminika nyakati za jioni ni wengi mno,” aelezea msanii huyu.

Mapato mazuri kiasi

Kuhusu mapato yake ya uuzaji wa kahawa ‘thungu’ na kahawa tamu, Mwajoha anadai japo hayaridhishi, ni mazuri kiasi kwani si rahisi kwa mfanyabiashara wa kawaida mwenye duka kubwa kuweza kupata.

“Sina budi kukubali hali ilivyo, huwa nauza gilasi moja ya kahawa (thungu na tamu) kwa Sh15 pekee, ambapo sufuria ninayotumia inanipatia jumla ya gilasi 35,” adokeza Mwanjoha.

Anasema sufuria hiyo ya lita sita inamwingizia pato la jumla la Sh525 pindi kahawa inapomalizika kabla ya kuitumia kwa kuchemshia kahawa nyiingine.

“Hii inamaanisha ikiwa natengeneza kahawa ‘thungu’ mara tano kwa siku, nitajiingizia takriban Sh2,625,” anadokeza Mwajoha.

Na endapo atatengeneza kahawa tamu mara tano kama afanyavyo kwa kahawa ‘thungu’, pia anatengeneza Sh2,625.

Kutokana na hesabu hiyo, Akilimali imebaini Saidi Mwanjoha anaweza kujiingizia jumla ya Sh78,750 za kahawa ‘thungu’ kwa mwezi ikiwa anatayarisha sufuria tano pekee za kahawa hiyo kila siku, huku akijiingizia pato sawa na hilo kila mwezi kwa utayarishaji wa sufuria tano za kahawa tamu kila siku na zimalizike.

Aidha, hesabu hiyo yaonyesha Mwajoha anaweza kunufaika kwa pato la hadi Sh1,890,000 kwa mwaka!