• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 5:50 AM
KIU YA UFANISI: Wengi hustaajabia kuku wake walao mboga na matunda kama binadamu

KIU YA UFANISI: Wengi hustaajabia kuku wake walao mboga na matunda kama binadamu

Na CHARLES ONGADI

UKISTAAJABU ya Musa utayaona ya Firauni.

Je, umeshawahi kuona kuku wanaokula mboga na matunda kama tu binadamu badala ya nafaka?

Katika kituo cha biashara cha Bushbar, Shanzu, Mombasa kuna kuku wanaokula kwa wingi mboga na matunda kama chakula chao cha kila siku.

“Ili kupata kuku mwenye afya na anayevutia ni bora kumlisha mboga na matunda kama tu anavyokula binadamu,” asema mfanyabiashara maarufu eneo la Shanzu, Benson Mutuku Mbwendwa.

Mbali na biashara ya fanicha, Mutuku pia ni mfugaji maarufu wa kuku wa kienyeji eneo hili ambaye aina ya ufugaji wake umeondokea kuwashangaza wengi. Anafuga zaidi ya kuku 80 wa kienyeji ambao amewahifadhi katika vibanda tofauti katika eneo lake la biashara ya fanicha.

Kila asubuhi, Mutuku anahakikisha amewatafutia kuku wake kiamsha kinywa cha mboga za sukuma wiki na mchicha anazonunua katika soko la karibu na eneo lake la biashara. Kisha inapofika wakati wa chakula cha mchana, anawanunulia matikitimaji anayoyapasuapasua kisha kuwaachia wadone.

Mutuku anaiarifu Akilimali kwamba kama binadamu, mwili wa kuku unahitaji mboga na matunda ili kunawiri na kuepuka magonjwa kila sampuli.

Anasimulia kwamba ni nadra kwa kuku wake kuvamiwa na magonjwa kiholela kwani miili yao ina kinga ya kupambana na magonjwa kutokana na kula mboga na matunda. Ijapo Mutuku anakiri kuwanunulia kuku wake chakula cha dukani lakini siyo chaguo lao la kwanza kama walivyo kuku wengine wa kawaida. Hata hivyo, katika kuhakikisha hapati hasara kutokana na magonjwa hatari kama kideri anahakikisha kwamba anawachanja na kujihami kwa dawa.

“Kila wakati nahakikisha nimejihami kwa dawa kama New Castle, Chickstarter na Combora ambazo ni kiboko ya magonjwa angamizi kwa kuku,” aeleza Mutuku. Anafichua kwamba mwanzoni hakuwa na nia ya kufanya ufugaji wa kuku kwa lengo la kuuza lakini baada ya kubaini kwamba wanalipa vyema ndipo aliamua kuvalia njuga ufugaji kama kitega uchumi. Aongeza kabla ya kuamua kufanya ufugaji miaka kumi iliyopita, alikuwa akiwapatia bure bilashi marafikize waliokuwa wakimtembelea.

Hata hivyo, anafichula kwamba anauza kuku mmoja aliyekomaa kwa kiasi cha Sh1,000 na wateja wengi wamekuwa wakimiminika kununua.

Wengi hutoka maeneo ya mbali kama Mtwapa, Kikambala, Majengo Kanamai na maeneo ya katkati ya mji wa Mombasa kama makande, Tudor na hata Kizingo kununua kuku hawa wa kienyeji.

Kulingana na Mutuku, wafugaji wengi wa kuku wanakumbatia sana ufugaji wa kuku wa gredi wakati Wakenya wengi wameanza kurudia ulaji wa kuku asilia wa kienyeji. Hii imepelekea wafugaji wa kuku wa kienyeji kuanza kupata faida kutokana na bidhaa hii kuanza kupendwa na wengi kila uchao. Mutuku anawashauri wafugaji wa kuku wa gredi kuanza mara moja kwenda na wakati kwa kugeukia ufugaji wa kuku wa kienyeji.

“Ni heri ukawie lakini ufike kuliko haraka haraka ambayo haina baraka. Ijapo mfugaji atahitajika kusubiri kipindi kirefu kabla ya kuanza kupata faida katika ufugaji wa kuku wa kienyeji kuliko wa gredi lakini ukweli wa mambo ni kwamba mafanikio yameanza kuonekana katika ufugaji wa kuku wa kienyeji,” asema Mutuku.

Anawashauri wafugaji wa kuku wa kienyeji kutokuwa na mazoea ya kuwalisha kuku wao nafaka pekee na badala yake wajaribu mbinu ya kuwalisha mboga na matunda na wataona matokeo.

Anawakumbusha vijana wasio na kazi mijini, kujitosa katika ufugaji wa kuku hasa wa kienyeji kwa kuwa inalipa sana kuliko hata kazi ya kuajiriwa. “ Ni kazi ambayo unajipanga bila kupangwa na yeyote ila tu cha muhimu ni kujituma kila wakati kulenga faida nono,” ashauri Mutuku.

You can share this post!

KIU YA UFANISI: Mradi wa maziwa unaonawiri na kunufaisha...

Jericho Allstars msimu huu imeona giza ligi ya S8PL

adminleo