• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 3:31 PM
KONOKONO: Ngonjera inayotetea haki za mtoto wa kiume

KONOKONO: Ngonjera inayotetea haki za mtoto wa kiume

Na PATRICK KILAVUKA

Haki za watoto zinapaswa kuzingatiwa pasi na kubaguliwa kijinsia kwani, mtoto ni mtoto awe wa kike au wa kiume!

Ni kutokana na haki za mtoto wa kiume kukiukwa katika jamii, wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Makutano SA kutoka Kaunti Bungoma waliwasilisha ngonjera yenye kichwa Konokono ambayo ilirejelea kauli mbiu ya kuzingatia haki zake katika mashindano ya Kitaifa ya Magizo na Filamu.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Makutano SA, Kaunti ya Bungoma wakifanya mazoezi ya kukariri ngonjera Konokono ambalo ilikuwa inaashiria unyanyasaji wa mtoto mvulana huteseka na kuteswa kupitia vichapo na hamaki au vita pasipo wa kumtetea katika mashindano ya Maigizo na Filamu yaliyoandaliwa Shule ya Upili ya Lenena,Nairobi. Picha/Patrick Kilavuka

Mada ya Konokono ilidhihirisha vile mtoto mvulana anateseka au kuteswa katika jamii na haki zake za kimsingi au kibinadamu kukandamizwa bila kuongelewa hadharani.

Ngonjera hiyo ilisisimua kuanzia mashinani hadi mashindano ya kitaifa ambayo yaliandaliwa Shule ya Upili ya Lenena, Kaunti ya Nairobi na hata kutawazwa kuwa wasilisho bora la mwaka 2018. Pia, walipokea kombe la wasilisho bora kuhusu uhamasisho wa Uwiano wa Kitaifa na Utangamano kupitia sanaa na filamu.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Makutano SA, Kaunti ya Bungoma wakionesha vile umoja watu wanaweza simama kidete kutetea haki za mtoto wa kiume wakati wa mazoezi katika mashindano ya Maigizo na Filamu yaliyoandaliwa Shule ya Upili ya Lenana, Nairobi. Picha/Patrick Kilavuka

Vikombe na vyeti vingine ambavyo vilivunwa kutokana na wasilisho hilo ni; Ngonjera bora la Kiswahili, utunzi bora, ulimbwende na jezi bora, uelekezi bora na utayarishi bora chini ya mwalimu mkuu Josephine Masinde.

Hata hivyo, Wasilisho lao lilianza kutamalaki kitengo cha Ngonjera kuanzia mashindano ya Kauntindogo ambayo yalifanyiwa Chuo cha Ualimu cha Nabongo na kwa kuwa bora kisha wasanii hawa wakapewa fursa ya kupeperusha bendera katika mashindano ya Kaunti ambayo yaliandaliwa chuoni humo tena na kuwa bora.

Wanafunzi wa kike wa Shule ya Msingi ya Makutano SA, Kaunti ya Bungoma wakariri ngonjera Konokono ambayo ilikuwa inaangazia namna haki za mvulana zinakandamizwa mfano kupokea vichapo katika mashindano ya Maigizo na Filamu yaliyoandaliwa Shule ya Upili ya Lenena,Nairobi. Picha/Patrick Kilavuka

Wasanii hawa waliendelea kutia fora zaidi katika mashindano ya Kanda ya Magharibi ambayo yalifanyiwa Shule ya Upili ya Vihiga na kuibuka katika nafasi ya kwanza halafu wakapokea mwenge wa kutua katika ya mashindano ya kitaifa mwaka huu baada ya kutawazwa malikia wa ngonjera.

Kando na kuonesha ubabe mwaka huu, miaka mingine ambayo shule hii ilikuwa pia na matokeo bora katika mashindano hayo ilikuwa 2014, walipofika katika mashindano ya kitaifa na wasilisho Vidude na hata wakumtumbuiza Rais.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Makutano SA, Kaunti ya Bungoma wakikariri ngonjera Konokono ambayo ilikuwa inaangazia haki za mvulana zinavyokandamzwa pole pasipo wa kumtetea katika mashindano ya Maigizo na Filamu yaliyoandaliwa Shule ya Upili ya Lenena,Nairobi. Picha/Patrick Kilavuka

Mwaka 2015, ilifika katika kingang’anyiro cha Kanda ya Magharibi na hoja ya Fuski( lengo likiwa kuzima unyakuzi wa ardhi za mashule), mwaka 2016, walikuwa na wasilisho lenye mada ya Ufagio ambalo lilifika kiwango cha Kanda katika mashindano yaliyoandaliwa Shule ya Upili ya Friends School Kamusinga.

Mwaka 2017 wasilisho lao la Remote lilifika tena katika mashindano ya kitaifa yaliyoandaliwa Kisumu na kupokea tuzo la Uwiano wa Kitaifa na Umoja.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Makutano SA, Kaunti ya Bungoma wakikariri ngonjera ya Konokono wakiashiria kutamauka kuhusu vile haki za mvulana zinakiuka bila kuangazia katika mashindano ya Maigizo na Filamu yaliyoandaliwa Shule ya Upili ya Lenena,Nairobi. Picha/Patrick Kilavuka

Changamoto? Ni kuwianisha mazoezi na masomo darasani, wazazi wengine kutotambua vipaji vya watoto wao na kutaka kuwazuia kushiriki katika kufanya zoezi na gharama ya juu ya matayarisho kiujumla.

Wasanii hawa kumi na watano, wanaushukuru uongozi wa shule kwa kuwashika mkono na kuwaamini huku wakitazamia kufanya vyema tena mwaka ujao kadri ya kudura za Maulana mwenye uwezo na maarifa ndiposa wafikie hatima ya mashindano hayo kumtumbuiza Rais.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Makutano SA, Kaunti ya Bungoma wakionyesha tuzo zao baada ya kuibuka washindi katika mashindano ya Maigizo na Filamu yaliyoandaliwa Shule ya Upili ya Lenena,Nairobi. Picha/Patrick Kilavuka

 

You can share this post!

Tutapunguza ada ya umeme mradi wa Olkaria ukikamilika...

ERIC MALANDA: Aanzisha timu yenye makali ligini licha ya...

adminleo