Makala

Kufa dereva kufa makanga mjeledi wa Gachagua ukimtandika Ruto

Na WAANDISHI WETU October 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

BUNGE la Kitaifa limeongeza gia mchakato wa kumtimua mamlakani Naibu Rais Rigathi Gachagua huku likiziba haraka mianya ya kisheria inayoibuka.

Haya yaliibuka Ijumaa wakati Karani wa Bunge, Bw Samuel Njoroge alipoongeza muda wa ushirikishaji wa umma katika hatua ya kuheshimu agizo la Mahakama kwamba, ufanyike katika maeneo bunge yote 290.

Jaji Richard Mwongo wa Mahakama Kuu mjini Kirinyaga alitoa uamuzi wake Ijumaa akisema ushirikishaji umma kuhusiana na mchakato huo unapaswa kufanyika katika maeneo bunge yote nchini na sio katika kiwango cha kaunti pekee.

Saa chache baada ya uamuzi huo kutolewa, Bw Njoroge alitoa ilani akitangaza kuwa, zoezi la kushirikisha umma limeongezwa muda hadi Jumamosi na litafanyika katika kiwango cha maeneo bunge.

Hii ilionekana kinyume na kawaida ya maafisa wakuu wanaojivuta kutekeleza maagizo ya mahakama.

Haikubainika mara moja iwapo walalamishi waliowasilisha kesi katika Mahakama Kuu ya Kirinyaga walikuwa wamekabidhi rasmi Bunge la Kitaifa agizo hili wakati muda wa ushirikishaji umma ulipoongezwa.

Hatua hiyo iliangazia mikakati iliyosukwa na kuivishwa kuhusiana na mchakato wa kumtimua ofisini Bw Gachagua ikiwemo fedha za kuufanikisha, hasa ikizingatiwa zoezi la ushirikishaji umma linagharimu mamilioni ya pesa.

Kasi ambayo Bunge linaendesha mchakato huo pia inaonyesha kujitolea kwa waandalizi kuhakikisha unafanikiwa.

“Kwa kutambua kuwa, Mahakama Kuu mjini Kerugoya iliagiza Bunge la Kitaifa kuandaa vikao vya ushirikishaji umma karibu zaidi na raia, angalau katika kiwango cha maeneo bunge katika kila eneo bunge nchini Kenya kuwezesha wapigakura wa wabunge wanaohusika na mchakato wa kuondolewa mamlakani kushiriki katika vikao hivyo, zoezi lililoanza Oktoba 4, 2024 limeongezwa muda hadi Oktoba 5 2024,” Bw Njoroge alisema katika tangazo lake.

Alisema vikao hivyo vitafanyika katika ofisi zote za maeneobunge 290 na katika ofisi zote za wawakilishi wa wanawake ambao ni wabunge katika kaunti zote 47.

Katika agizo lake, Jaji Mwongo alisema kushirikisha umma katika kiwango cha kaunti hakutoshi na hivyo akaagiza ushirikishaji huo upanuliwe.

Ghasia

Vikao vya Ijumaa vilikumbwa na ghasia katika maeneo mengi nchini na kufanya shughuli hiyo kusitishwa katika baadhi ya vituo.

Wakazi waliohudhuria kikao cha ushiriki wa umma katika ukumbi wa Bomas of Kenya, Kaunti ya Nairobi walilazimika kusitisha shughuli hiyo kwa muda baada ghasia kuzuka.

Wahuni walimshambulia mwanaharakati Morara Kebaso alipowasili kushiriki zoezi hilo katika ukumbi huo.

Matukio kama hayo yalishuhudiwa katika maeneo ya Murang’a, Nyeri, Kiambu na Nakuru ambako zoezi hilo lilisitishwa.

Ushiriki wa umma katika mchakato wa kumtimua Bw Gachagua ulisitishwa katika uwanja wa Nakuru ASK baada ya ghasia kuzuka.

Baadhi ya wakazi waliingia barabarani, wakipinga kuondolewa ofisini kwa Bw Gachagua wakiimba ‘Bila Rigathi, hakuna Ruto.’

Katika Kaunti ya Nyandarua, wakazi kwa kauli moja walipinga hoja hiyo wakisema kwamba, hakuna ushahidi wa kuunga mkono kuondolewa kwa Gachagua.

Zoezi hilo lililofanyika Kisumu lilivutia idadi kubwa ya watu waliojitokeza kuhudhuria huku wakazi wakiwasilisha maoni yao kuhusu suala hili.

Lakini katika hali ambayo haijawahi kushuhudiwa, hali ya wasiwasi ilitanda pale wananchi walipotaka mchakato wa kumtimua pia uhusishe Rais William Ruto.

‘Tulimpigia kura Mheshimiwa Gachagua kwa sababu ya rais, hakugombea afisi hiyo peke yake kwa hivyo ikiwa naibu wa rais ataondoka basi rais aende pia,’ mmoja wa wakazi alisema.

Mjini Kakamega, mzozo kati ya makundi mawili ulilazimisha hafla hiyo kumalizika katika hali ya kutatanisha.

Mrengo unaopinga kuondolewa kwa Bw Gachagua ulivamia ukumbi wakiimba ‘Ruto lazima aondoke!’ na kuvuruga mjadala uliokuwa ukiendelea.

Kundi hilo linalojumuisha wafanyabiashara wengi kutoka soko la Kakamega lilidai ikiwa Gachagua atalazimika kuondoka, basi lazima Ruto pia aondolewe afisini.

‘Tulimpigia kura Ruto kuwa Rais. Gachagua alikuwa msaidizi wake. Ikiwa Gachagua ataenda lazima waende pamoja,’ akafoka Sammy Imbwaka.

Tofauti zilizuka baina ya wananchi wa Lamu waliojitokeza kwa vikao vya umma kujadili jinsi ya kumng’oa mamlakani Naibu wa Rais Rigathi Gachagua kwenye ukumbi wa KCB mjini Mokowe.

Wananchi walianza kurushiana cheche za maneno punde makarani wa bunge la kitaifa waliposoma baadhi ya mashtaka yanayosababisha kuanzishwa kwa mchakato mzima wa kumng’atua kitini Bw Gachagua kabla ya kuwapa waliojitokeza ukumbini fomu maalumu kujaza.

Kuna wananchi waliosikika wakimtetea Bw Gachagua ilhali wengine wakiunga mkono kubanduliwa kwake.