• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 12:44 PM
Kufunga baa ‘kiholela’ kunawafungia wachuuzi na wasanii riziki, adai Kioni

Kufunga baa ‘kiholela’ kunawafungia wachuuzi na wasanii riziki, adai Kioni

NA MWANGI MUIRURI

MRENGO wa Azimio La Umoja-One Kenya eneo la Mlima Kenya sasa umeitaka serikali ya Rais William Ruto ielewe kwamba ndani ya baa hakuuzwi pombe peke yake, bali pia huwa ni soko kubwa linalowapa wachuuzi na mahasla wengine riziki.

Aliyekuwa mbunge wa Ndaragwa Jeremiah Kioni amedai kwamba serikali inaenda kinyume na ahadi ambazo ilitoa.

“Walidai kwamba utawala wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta ulikuwa ukidhulumu watu wa chini katika biashara. Wakatuambia kwamba hakuna riziki ya mtu itawahi kufungwa lakini sasa wanapiga vita riziki za wengi,” akasema Bw Kioni.

Katibu huyo mkuu wa chama cha Jubilee alisema Naibu Rais Rigathi Gachagua ambaye amezindua vita dhidi ya pombe haramu na kulenga utundu wa wamiliki wa baadhi ya baa, anafaa kujifahamisha kwamba biashara ya baa huwa ni soko kwa wachuuzi chungu nzima na ambao sasa wanaumizwa kwa msingi wa kupambana na ulevi.

“Sisi watu wa Azimio tunaunga mkono vita dhidi ya pombe haramu lakini hatuungi mkono kufungwa hata kwa baa moja isipokuwa ile ambayo imedhihirisha ukosefu wa maadili kabisa hasa kwa kuuzia watoto pombe,” akasema.

Alimtaka Rais Ruto na Bw Gachagua wajumuike mashinani na wajifahamishe na hali halisi ya mahasla wakiwa ndani ya baa kuchuuza bidhaa zao wala sio kunywa pombe.

“Ile dhana ambayo serikali iko nayo kwamba pombe itaisha kupitia kufunga baa na kuwakamata walevi, ni mtazamo usio na mashiko. Kile ambacho inafaa kufanya ni kuweka mikakati ya kuhakikisha upishi wa pombe au utengenezaji wake unafanywa kwa kuzingatia usafi na ubora wa hali ya juu ili bidhaa inayofika sokoni iwe salama,” akasema.

Aliongeza kwamba mkakati mwingine ni serikali kuzima mianya ya baa kupata pombe haramu.

“Waache kuja tu na kuamuru wafanyabiashara kufunga baa,” akasema.

Naye aliyekuwa Waziri Msaidizi (CAS) katika wizara za Spoti na Elimu Bw Zack Kinuthia alisema kwamba ukifunga baa, unamfungia riziki mwekezaji na wahudumu wake.

“Isitoshe, utakuwa umewafungia wengine wengi ambao hutegemea kufunguliwa kwa milango ya baa ndipo wapate chakula cha kila siku,” akasema.

Bw Kinuthia alisema baa moja ya kiwango cha chini kabisa hutoa nafasi tano za kazi, zikiwa ni mwekezaji, mhudumu wa kaunta, mhudumu wa wateja, soja na mtekelezaji usafi.

“Hii ina maana kwamba kila baa inayoamrishwa ifungwe kuna kazi zisizopungua tano ambazo serikali inaua,” akasema.

Mwenyekiti wa muungano wa baraza la wazee Wachira Kiago ameteta kwamba vita hivyo vya kufungisha baa zinaathiri uchumi mashinani kwa kiwango kikuu.

“Baa ikiwa haiko karibu na shule, hospitali au eneo la ibada, haifai kuambiwa ifungwe. Ukipokonya mhudumu wa baa leseni yake kwa msingi kwamba watu wanakunywa pombe haujasuluhisha lolote,” akasema.

Alisema wazee wanaunga mkono vita dhidi ya pombe ya mauti “na ni msimamo wetu kwamba taka hizo za kukera hazitengenezewi ndani ya baa”.

Soma Pia: Wakazi wa Kangai wateketeza baa ya mauti

Bw Kiago aliteta kwamba wachuuzi wa mayai ‘boilo’, njugu, nguo, viatu, bidhaa vya ujumla, madalali wa kushirikisha dili, wauzaji kahawa, samosa, matunda, dawa za mitishamba, vitabu, mifugo kama sungura na kuku, samaki na kadhalika huwa wanategemea pakubwa biashara ya baa kujishindia wateja.

Wengine hasa katika baa zilizo na lojing’i huwa wanachuuza bidhaa muhimu za matumizi ndani ya baa.

Mwenyekiti wa muungano wa wasanii Mlima Kenya Epha Maina alisema Kuna baa ambazo zimefungwa na zilikuwa zinaandaa shoo ambazo huwapa wasanii husika riziki yao bila kusahau waandalizi wa nyama nje ya vilabu hivyo.

“Unafunga baa na kwa mpigo unamnyima msanii nafasi ya kuandaa shoo. Hivi vita vya pombe vinafaa vipigwe msasa na ieleweke kwamba kufunga baa sio kumaliza pombe ya mauti. Pombe hii hata inaweza ikaandaliwa kwa boma la mtu binafsi au kwa vichaka. Katika hali hiyo pia utasema tufunge maboma yetu na pia vichaka?” awaza msanii Ben Githae.

Bw Githae alisema kwamba “kila mtu aliyeenda shule anasema kwamba kuzima pombe ya mauti kutafaulu tu iwapo serikali itazima kupatikana kwa malighafi na viwanda haramu wala sio kupitia kufunga baa”.

Bw Maina alisema kwamba “sisi kama wasanii tunaenzi sheria na pia usalama wa watu katika hali zote na kamwe hatuungi mkono ulevi kiholela…lakini tutilie maanani kwamba biashara ya baa sio haramu nchini”.

Wahudumu wa bodaboda, teksi na tuk tuk pia wanasema kila baa huwa ni mwanya wa kupata wateja hasa kuanzia masaa ya usiku.

“Walevi wengi hutafuta huduma za uchukuzi kufika kwao nyumbani. Kufunga baa ni sawa na kumalizia watu wa bodaboda nafasi za kuhudumu. Ni kama hii serikali iko kwa vita na wanaojitafutia katika mitaa kama mahasola,” akasema Bw Kamande Ngoru, mhudumu wa teksi Mjini Murang’a.

Kwa upande wao, vibiritingoma mitaani walisema kwamba baa ndizo shamba lao la kuvuna wateja huku nao baadhi ya wachungaji wa kuhamahama wakisema huwa wanahubiri ndani ya baa kuponya nyoyo za wanaohangaika na mengi ya dunia na kupata sadaka.

Aidha, ombaomba walioongea na Taifa Leo walihofia kwamba vita vya baa ni sawa na kuwafungia milango ya kugongagonga wakisaka wahisani.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Raila akienda AUC Kenya itakosa upinzani wa nguvu –...

OKA yafufuka kuipa nguvu Azimio – Kalonzo

T L