Makala

KUMBUKUMBU 2019: Magavana watatu waanza mwaka mpya wakiwa nje ya ofisi

January 1st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

MAGAVANA watatu wanauanza mwaka huu wakiwa hawawezi kukanyanga afisini kutokana na kesi za ufisadi wa mamia ya mamilioni.

Magavana hao Ferdinand Waititu Baba Yao (Kiambu), Mike Sonko (Nairobi) na Moses Kasaine ole Lenolkulal (Samburu) hawajui hatima zao, kesi hizo zinapotarajiwa kuangaziwa upya huu mwezi wa Januari ambao leo Jumatano umeanza rasmi.

Waititu anakabiliwa na kesi ya ufisadi wa zaidi ya Sh580 milioni, Sonko naye alikana kushiriki katika ufisadi wa Sh381 milioni ilhali Lenolkulal alishtakiwa kwa kupokea kwa njia ya ufisadi zaidi ya Sh80 milioni.

Kaunti hizi tatu zimejikuta katika lindi la suitafahamu baada ya Mahakama kuu kuamuru wasalie nyumbani hadi kesi zinazowakabili ziamuliwe.

Wote watatu walishtakiwa mbele ya hakimu mkuu mahakama ya kuamua mizozo ya ufisadi (ACC) Douglas Ogoti.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Bw Noordin Haji aliwafungulia mashtaka magavana hao watatu na kumsihi Bw Ogoti aamuru washtakiwa hao wasiruhusiwe kurudi afisini hadi kesi zinazowakabili ziamuliwe.

Bw Haji aliomba mahakama itegemee maamuzi ya Jaji Mumbi Ngugi na Ngenye Macharia ambayo walikubaliana kuwa magavana ni watumishi wa umma na Kifungu nambari 10 cha Katiba kinaashiria kila “mtumishi wa umma anapasa kuiletea afisi anayohudumu heshima.”

Pia kifungu hiki pamoja na kile cha Sura ya 6 vinasema watumishi wa umma hawapasi kushiriki katika vitendo ambavyo vitashusha hadhi yao, kuvunjia umma heshima na pia kufedhehesha nchi hii.

Katika lingo za kimataifa nchi hii imepata sifa mbaya kwa sababu ya visa vya ufisadi.

Katika mwaka wa 2019, Bw Haji amewafungulia mashtaka ya ufisadi wakuu serikalini na wengine wanaendelea kupigwa darubini.

Baadhi ya wakuu walioshtakiwa ni Magavana hao Waititu, Sonko, Lenolkulal, Waziri wa Hazina Kuu Henry Rotich na Katibu wake Kamau Thuge wanaokabiliwa na shtaka la ufujaji wa zaidi ya Sh63 bilioni katika mabwawa ya Kamweror na Aror.

Kufuatia maamuzi ya Majaji Ngugi na Macharia, washukiwa hao wa ufisadi wanatakiwa kukaa manyumbani mwao hadi kesi zinazowakabili zisikizwe na ziamuliwe.

Katika kesi hizo dhidi ya magavana hao watatu mahakama ilifahamishwa walijifaidi na pesa za umma kutokana na kandarasi zilizopewa baadhi ya makampuni.

Bw Waititu pamoja na mkewe Susan Wangari walikanusha mashtaka ya kufaidi kutokana na kandarasi ya ujenzi wa barabara ambazo kaunti hiyo ilitoa ikambaratiwe kwa bei ya Sh588 milioni.

Kandarasi hiyo ya ujenzi wa barabara ilipewa kampuni ya Testimony Enterprises Limited.

Katika kesi ya Sh381 milioni inayomkabili Sonko, kampuni za ROG Securities Limited (inayomiliki matatu za ROG-River of God) Web Tribe Limited, Hardi Enterprises Limited, Toddy Civil Engineering Ltd, Arbab Ltd na High Energy Petroleum ndizo zilitajwa na tume ya kupambana na ufisadi (EACC) kuhusika katika ufujaji wa pesa za kaunti ya Nairobi.

DPP na EACC walisema kuwa pesa kutoka kwa kampuni hizo, ziliwekwa kwenye akaunti za Sonko katika Benki ya Equity (EBL) zilizoko kaunti za Nairobi, Kwale na Mombasa.

Sonko pamoja na wengine 24 walikanusha jumla ya mashtaka 38.

Aliachiliwa kwa dhamana ya pesa tasilimu Sh15 milioni katika kesi mbili zinazomkabili.

Ngoma za kisheria zitachezwa katika kesi dhidi ya Gavana Lenolkulal wakati mashahidi 235 watakapofika kortini kueleza jinsi kinara huyo wa kaunti alivyohusika na ufujaji wa Sh84 milioni anazodaiwa alipokea kutoka kwa kaunti hiyo kwa kuuzia magari mafuta na bidhaa za petroli kutoka kwa kampuni ijulikanayo Oryx Service Station.

Kwa jumla Bw Lenolkulal adaiwa alipokea Sh84,695,995 kwa kutumia mamlaka ya afisi yake vibaya.

Bw Ogoti alielezwa DPP atatumia saa 130 kukamilisha kuwaita mashahidi hao.

Mahakama ilielezwa na kiongozi wa mashtaka unaongozwa na naibu wa mkurugenzi wa mashtaka ya umma Bw Alexander Muteti.

Kesi hizi zitaanza kusikizwa Januari 2020.