Makala

KURUNZI YA PWANI: Changamoto za ulezi kwa wafungwa wa kike gereza la Shimo la Tewa

May 14th, 2018 Kusoma ni dakika: 4

WINNIE ATIENO na DIANA MUTHEU

MNAMO Februari 27 mwaka 2017, Celine Ong’ayo Emali alimwadhibu na kumjeruhi vibaya mwanawe kwa kile anachosisitiza alikuwa jeuri. Lakini kulingana na mama huyo hakukusudia kumjeruhi mwanawe.

Tukio hilo lilimfikia mzee wa kijiji huko Likoni na Bi Emali akakamatwa akiwa na umri wa miaka 22.

Alihukumiwa mahakamani kwa shtaka la kumjeruhi mwanawe.“Nilikuwa mjamzito na mwingi wa hisia. Sikuwa na nia ya kumuumiza mwanangu bali ni hasira za uja uzito. Lakini chifu alikataa kunisamehe.

Nilipelekwa mahakamani, nikashtakiwa na kufungwa kwa miaka mitatu,”alisema Bi Emali kwenye mahojiano na Taifa Leo anakoendeleza kifungo chake katika gereza la Shimo la Tewa.

Mwaka mmoja umesalia mfungwa huyo akamilishe kifungo chake.

Februari 27, mwaka ujao, Bi Emali atamaliza kifungo chake katika gereza la wanawake la Shimo la Tewa.  Bi Emali alihukumiwa kifungo gerezani akiwa na ujazito wa miezi saba.

Anasema kuwa hasira ya ujauzito ulipelekea tukio hilo hadi akamwacha mwanawe na majeraha.

Aprili 2017, alijifungua mtoto wa kike lakini maisha gerezani yamezidi kuwa magumu.

Naibu Mratibu wa Huduma ya Magereza eneo la Pwani Stanley Mbaji awalisha keki mahabusu katika Gereza la Shimo La Tewa. Picha/ Kevin Odit

MAISHA MAGUMU

“Maisha ya jela ni magumu lakini ni magumu zaidi endapo una mtoto mchanga. Watoto wana mahitaji yanayotakiwa kutimizwa ambapo siyawezi nikiwa jela. Wakati mwingine familia zetu hazitutembelei, hivyo inatulazimu kung’ang’ania angalau tupate sabuni na mahitaji muhimu ya watoto wadogo,” Bi Emali alisema.

Hata hivyo anashukuru kuweko kwa vyakula maalum vya watoto wachanga vinavyopeanwa katika kituo hicho cha kurekebishia tabia.

Tangu alipofungwa jela, Bi Emali anasema kuwa hakuna mtu yeyote wa familia yake ikiweko nduguze au wazazi wake ambao wamemtembelea.

“Nihisi kama nimekataliwa na kutelekezwa na jamii. Ni mume wangu tu ambaye hunitembelea mara kwa mara. Lakini sijui ikiwa ameoa tena au atanisubiri nimalize kifungo changu, “Bi Emali aliongezea.

Anasema kuwa watoto katika kituo hicho wanapewa maziwa na uji.

“Ningependa mtoto wangu alelewe katika mazingira mengine badala ya jela ili asiige tabia na lugha mbaya ya humu. Lakini kuna sheria ambayo ukizalia jela ni sharti umlee mtoto hadi afikie umri wa miaka angalau minne” akaongeza.

Mfungwa mwenzake, Mary Marube alikamatwa katika mpaka wa Lunga Lunga Mei 18 mwaka jana kwa kosa la kuuza dawa za kulevya.Bi Marube alikuwa mjamzito, akajifungua mnamo Desemba 18 mwaka huo huo katika gereza hilo huko Mombasa.

“Ningependa mwanangu alelewe nyumbani kwa kuwa mazingira ya jela ni duni. Watoto si wafungwa, kwa nini wafungwe pamoja na waliohukumiwa? Si sawa, “alisema Bi Marube.

Mtoto wake aliye na miezi mitatu anaonekana kuwa mwenye afya kutokana na kunyonyeshwa matiti wanavyoshauri madaktari.

Mahabusu wa kike katika gereza la Shimo La Tewa wabeba bidhaa walizoletewa na kampuni ya Nation Media Group Julai 31, 2015. Picha/ Kevin Odit

“Nitaanza kumpa chakula akiwa na miezi sita. Ningeomba turuhusiwe kuwaacha watoto wetu na jamaa zetu badala ya wao kuishi na sisi gerezani.

Watoto hawapaswi kulipia dhambi za wazazi wao. Gerezani sio mahali pazuri, watoto watajifunza tabia mbaya na matusi, “aliongezea Bi Marube.

Alikiri kuwa hapo zamani aliuza dawa za kulevya lakini alipokamatwa alikuwa ameacha biashara hiyo haramu.

Mama huyu ambaye ana watoto sita anahudumu kifungo cha miaka mitano gerezani. Anasema alikamatwa kutokana na maisha yake ya zamani ya biashara ya kuuza dawa za kulevya.

“Niliuza dawa za kulevya. Lakini nilipokamatwa, waliweka dawa hizo ili kunifanya kuwapa washirika wangu katika biashara.

Wafadhili wanapaswa kutusaidia kuwatunza watoto wetu walio nyumbani, wanaweza kupotoka na hata kuwa wezi. Mtoto bila mama anaweza kupotea, “Bi Marube aliongezea.

Mwanamke huyu mwenye umri wa miaka 42 anasema kuwa mumewe hakufahamu kuwa alikuwa anauza dawa za kulevya.

Bi Marube anasema changamoto katika maisha na umasikini ulimfanya kujihusisha na biashara hiyo.

“Singeweza kumwambia mume wangu waziwazi kuwa nauza dawa za kulevya. Alitambua tu nilipokamatwa na alinisamehe. Ni biashara yenye pesa lakini ninawaonya watu dhidi ya kujihusisha na ulanguzi wa dawa za kulevya. Gerezani sio mahali pazuri,”aliongezea.

Lakini kwa Prisca Mwaka, maisha ni kizungumkuti kwani analea pacha gerezani humo huku ndugu zake wakiendeleza kifungo chao cha miaka 30 katika upande wa pili wa wanaume katika gereza ya Shimo la Tewa.

Pamoja na ndugu zake wawili, Bi Mwaka 34, alihukumiwa kifungo gerezani mnamo Novemba 8 mwaka jana kwa kujaribu kuua.

Januari 8, mwaka huu alijifungua watoto pacha katika kituo cha afya cha gereza hilo.

“Nina pacha na hakuna mtu wa kukusaidia hapa gerezani, maisha ni magumu. Nilihukumiwa na ndugu zangu kutokana na kesi ya mgogoro wa ardhi nyumbani kwetu, Mtwapa. Ninasumbuka sana na ningemuomba Rais Uhuru Kenyatta anisaidie, “alisema huku machozi yakimtiririka.

Aliongeza: “Ni kesi ya kujaribu kuua lakini tumekata rufaa. Tulihukumiwa kifungo cha miaka 30.”

Afisa msimazi wa gereza hilo, Fairbain Ombeva alisema kuwa kina mama na watoto wao wanatunzwa vizuri.

“Tunatunza watoto wa wafungwa wenye umri wa miaka 0 hadi minne. Baada ya watoto hawa kufikia umri wa miaka minne, wanaruhusiwa kwenda kwa jamaa zao au katika vituo vya watoto kwa sababu wanaelewa kuwa wako gerezani.

Hata hivyo, tuna huduma za kuwalinda watoto mchana kutwa, malazi kando na chakula maalum, “alisema.

Mahabusu katika gereza la wanawake la Shimo La Tewa waungana na askari jela kucheza densi. Picha/ Kevin Odit

HAWACHANGANYWI

Alisema watoto hao hawachanganywi na watu wazima.

“Mchana huwa wanapelekwa kwenye kituo chao malaum hapa gerezani ambapo wanacheza na kusoma. Kuna maafisa waliofundishwa kuwatunza watoto hapa. Tuko hapa kurekebisha tabia na watoto hawa hawatajifunza tabia mbaya wakiwa gerezani,” akasema.

Akizungumza siku ambayo familia za wafungwa ziliruhusiwa kutangamana hapo gerezani siku nzima, Bi Ombeva alisema mama huyo aliye na pacha hupokea pakiti nne za maziwa ili kuongeza maziwa ya mtoto.

Aprili 10, kwa mara ya kwanza wafungwa kwenye jela hiyo ya wanawake walipewa muda wa kutangamana na familia zao ili kuhimiza upatanisho na kujua matukio mapya miongoni mwa jamaa zao.

Watoto na waume wa wafungwa hao walimiminika kwenye gereza hilo kujumuika na jamaa wao.

Walibubujikwa na machozi ya furaha baada ya kuona mama zao na wake wao ambao wanahudumia vifungo tofauti, ikiwa ni pamoja na vifungo vya maisha gerezani.

Familia za wafungwa waliotuhumiwa kwa ugaidi, ikiwa ni pamoja na ile ya Hania Sagar, mke Aboud Rogo, walikuwa miongoni mwa wale waliotembelea mama yao wakati wa siku ya familia kutangamana katika gereza hilo.

Kina mama waliofungwa pamoja na watoto wao walielezea maisha yao wakielezea masikitiko yao baada ya kukataliwa, kupuuzwa na kusahauliwa na familia zao wanapoendelea kutumikia vifungo vyao katika jela la Shimo la Tewa la wanawake.

Walisema kuwa ingawa ‘wanalipia’ dhambi zao, watoto waliowazalia gerezani hawapaswi kukaa jela sababu hawana hatia.

Kina mama hawa waliwazaa watoto wao katika hospitali ya Shimo la Tewa baada ya kukamatwa, kushtakiwa na kufungwa wakati walipokuwa wajawazito. Sasa wanaogopa watoto wao ‘watarithi’ tabia za gerezani.

Wakiongea kwa huzuni na majonzi, kina mama hawa walitoa wito kwa serikali iwaokoe watoto wao kutokana na mateso ya jela.