KURUNZI YA PWANI: SUPKEM lawamani kuhusu ilivyosimamia Hija ya 2018
Na CECIL ODONGO
UHASAMA umeibuka kati ya Baraza Kuu la Waislamu nchini (SUPKEM) na maajenti waliotoa huduma za kufanikisha safari za Waislamu kwenda Mecca mwaka huu.
Kulingana na takwimu kutoka SUPKEM, karibu mahujaji 5,000 walihudhuria ibada za mwaka huu lakini kumeibuka madai kutoka kwa mahujaji ya kutopata huduma za thamani ya pesa zao huku maajenti wakikashifu baraza hilo kuhusu madeni ya mamilioni ya fedha.
Kabla ya safari, mahujaji waliwatumia maajenti wanaotambuliwa na SUPKEM kupata stakabadhi muhimu za safari kutoka kwa idara ya uhamiaji na usajili wa watu serikalini kama vile paspoti, kupata chanjo za maradhi mbali mbali na kulipia gharama ya makazi, hema na tiketi za ndege.
Hata hivyo mwezi mmoja baada ya kukamilika kwa ibada hiyo, kampuni husika za maajenti zimeibua madai kuhusu madeni wanayodai baraza hilo huku wengine wakisema kwamba baraza limekuwa likiwapa ahadi hewa kila wanapodai hela hizo.
Madeni hayo yanakadiriwa kuwa mamilioni ya pesa huku ikisemekana pia serikali ya Saudia Arabia vile vile ikiwadai SUPKEM deni la mwaka jana na la mwaka huu.
“Mimi ninadai SUPKEM Sh16milioni na nimekuwa kwa ofisi zao mara kadhaa ili wanilipe pesa zangu lakini hakuna aliye tayari kunisikiza. Nilifanya bidii na nikahakikisha kwamba kila hujaji niliyemsimamia safari zake zinafanikiwa ila sielewi kwa nini nisilipwe haki yangu,” akasema ajenti mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe au linukuliwe kwa kuhofia kuadhibiwa.
Katibu Mkuu wa SUPKEM, Abdullahi Salat, alikanusha madai kwamba kuna deni lolote wanalodaiwa na maajenti akisema anafahamu kuhusu deni la serikali ya Saudia pekee.
Bw Salat aidha alisema huenda maajenti hao wanatumiwa na viongozi wengine wenye kinyongo kwa walio afisini kutatiza shughuli za SUPKEM.
“Ningependa kukwambia wazi wazi kwamba kila ajenti alipewa idadi ya mahujaji aliostahili kuhudumia kisha fedha hizo zikalipwa kwa serikali ya Saudi Arabia. Iwapo walikosa kufikisha idadi hiyo wajilaumu wenyewe wala hakuna deni lolote la ajenti tulilo nalo,” akakanusha Bw Salat.
Vile vile alipuuzilia mbali tetesi za baadhi ya mahujaji kwamba hawakupokezwa huduma nzuri wakati wa hijja na madai yalioyoenea kwamba wengine waliachwa wakiwa wamekwama Saudia Arabia ilhali walikuwa wamekamilisha malipo yao yote.
“Katika histora ya taifa hili hakuna hijja ambayo imekuwa ya ufanisi kama ya mwaka huu. Kila hujaji kutoka Kenya tulihakikisha ameshughulikiwa vizuri sana.
Mara tu walipotoka katika uwanja wa ndege iliwachukua nusu saa kufika kwenye mahema yao na kila siku tulihakikisha wako sawa kinyume na miaka ya nyuma ambapo watu walipotea na wengine kutaabika sana,” akaongeza Bw Salat.
Kando na hili maajenti wengine wanadai kwamba mahujaji waliopanga kusafiri hadi Mecca kwa ibada za hijja lakini zikatibuka dakika za mwisho mwisho wanazidi kuwaandama huku wakisisitiza wanataka kauli ya viongozi wa SUPKEM ndipo wafahamu pesa hizo zitalipwa lini.
Watu wanafikiria kwamba mimi nimekula hela zao ilhali pesa zote niliwasilisha. SUPKEM hawakutupigania wala kusaidia Waislamu kupata stakabadhi muhiimu za safari hizo ndiyo maana safari hizo zilitibuka.
Tunaomba tupewe haki yetu ili nasi tuwarejeshe waliokosa hijja fedha zao,” akasema ajenti mwengine na kufichua kwamba atalazimika kuichukulia baraza hilo hatua za kisheria iwapo hatakuwa amepokea fedha zake kufikia Jumatano wiki hii.
Wengi wa maajenti waliosema na Taifa Leo walidai kwamba wana ushahidi wa kutosha kutetea madai yao ikiwemo risiti na barua mbalimbali kutoka kwa SUPKEM.
Wakati uo huo kiongozi moja mashuhuri aliyehudumu katika uongozi wa baraza uliopita alisema kwamba huenda pesa hizo zilifujwa au kutumika kulipa marupurupu ya viongozi wa sasa akisema hali hiyo inaipaka tope Waislamu machoni pa umma na kimataifa.
“Ni hali ya kusikitisha kwamba hali imekuwa mbaya hivi na huenda hii ikawa mojawapo za sakata iliyosahauliwa. Mtu kama hajaenda hajj anafaa kurejeshewa fedha zake na wasifikiri hatujui kinachoendelea tunafahamu vizuri sana,” akasema kiongozi huyo.