KWA KIFUPI: Kulala kwa dakika kadhaa mchana kuna manufaa kiafya
Na LEONARD ONYANGO
UNAPENDA kulala mchana angalau mara mbili au tatu kwa wiki? Wataalamu wa afya wana habari njema kwako.
Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Hospitali ya Lausanne, Uswizi, ulibaini kwamba watu wanaolala mchana angalau mara tatu kwa wiki wanapunguza uwezekano wa kupatwa na maradhi ya moyo au kiharusi
Watafiti hao walihusisha watu 3,462 wa kati ya umri wa miaka 35 na 75 kwa kipindi cha miaka mitano.
Walibaini kuwa watu waliokuwa na mazoea ya kulala mchana kwa kati ya dakika tano na saa moja, walipunguza uwezekano wa kupatwa na maradhi ya mshtuko wa moyo kwa asilimia 48.
Lakini watafiti hao walionya kuwa watu wazembe wanaolala kwa zaidi ya saa moja mchana hawapati manufaa yoyote ya kiafya.