KWA KIFUPI: Kususia mboga za majani hufanya wazee kushindwa kutembea
Na LEONARD ONYANGO
WAZEE wanaokwepa kula mboga za majani kama vile sukumawiki au spinachi, basi wako katika hatari ya kushindwa kutembea.
Utafiti uliofanywa na wanasayansi umebaini kuwa ukosefu wa vitamini K mwilini unasababisha wazee kupata maradhi ambayo huwasababisha kushindwa kutembea.
Matokeo ya utafiti huo uliochapishwa katika jarida la kisayansi la Journal of Gerontology: Medical Sciences, ulibaini kuwa ukosefu wa vitamini K kwa wazee wa umri wa zaidi ya miaka 70, huwasababishia ulemavu.
Wanasayansi hao walibaini kuwa wazee wasio na vitamini K wako katika hatari ya kushindwa kutembea maradufu ikilinganishwa na wenzao walio nayo.
Watafiti hao walichunguza wazee 635 na ajuza 688 wa kati ya umri wa miaka 70 na 79.
Washiriki hao walichunguzwa kwa kati ya miezi sita na miaka 10.
Wanasayansi waligundua kuwa wazee ambao hawakupenda kula mboga walishindwa kutembea na wengine hawakuweza hata kusimama.
Idadi kubwa ya wazee wanaopenda kula mboga waliweza kutembea umbali mrefu na hata kufanya kazi za nyumbani.
Sukumawiki hutoa asilimia 400 ya vitamini K.
Aina nyingine za mboga zilizo na kiasi kikubwa cha vitamini K ni brokoli, maharagwe na kabichi.
Vyakula vingine vilivyo na chini ya asimilia 10 ya vitamini K ni maini, kuku, parachichi(avocado), nyama ya ng’ombe, maziwa, mayai na nyanya iliyokaushwa.