KWA KIFUPI: Omega 3 huenda ikahatarisha afya ya wagonjwa wa Kisukari – Watafiti
Na LEONARD ONYANGO
WATAFITI sasa wanaonya kuwa dawa yenye mafuta ya samaki (omega 3) si tiba ya ugonjwa wa kisukari maarufu type 2 diabetes.
Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha East Anglia, Uingereza, wanasema kuwa mafuta hayo huenda yakawa hatari kwa afya ya wagonjwa wa kisukari.
Awali, imekuwa ikiaminika kuwa omega 3 huepushia wagonjwa wa kisukari hatari ya kukumbwa na maradhi ya moyo.
Lakini baada ya watafiti hao kufanya uchunguzi wa kina, walibaini kuwa mafuta hayo ya samaki hayasaidii chochote kuboresha afya ya waathiriwa wa kisukari Type 2.
Dkt Lee Hooper ambaye aliongoza watafiti hao alisema kuwa walifanyia uchunguzi omega 3 baada ya kupokea malalamishi kutoka kwa waathiriwa wa kisukari kwamba hawajasaidika licha ya kutumia mafuta hayo.
“Omega 3 yamekuwa yakidaiwa kupunguza aina fulani ya mafuta yanayopatikana kwenye damu. Lakini tulipopima waathiriwa ambao wamekuwa wakiitumia, tulibaini kwamba mafuta hayo yaliyoko kwenye damu hayakupungua,” akasema Dkt Hooper.
“Kwa ufupi ni kwamba hatukupata faida au madhara ya mafuta ya omega 3,” akaongezea.