• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Leah Wangui: Mtafiti wa afya anayetukuza Mungu kupitia uimbaji

Leah Wangui: Mtafiti wa afya anayetukuza Mungu kupitia uimbaji

Na JOHN KIMWERE, NAIROBI

ALIANZA kughani nyimbo za kumtukuza Mungu akiwa na umri wa miaka 12 akisoma darasa la sita kwenye Shule ya Msingi ya Kisulisuli mjini Nakuru.

Katika mpango mzima anaorodheshwa kati ya wasanii chipukizi wanaoeneza injili ya Mungu kupitia tambo za mitindo ya kizazi kipya hapa nchini. Amehitimu kwa shahada ya digrii kutoka Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta (JKUAT) katika masuala ya utafiti wa Afya ya binadamu.

Hata hivyo, Leah Wangui Waweru maarufu Zaqen anasema tangia akiwa mtoto alitamani kuhitimu kuwa daktari ndoto ambayo haikutimia.

”Nimelelewa kanisani jambo lililonivutia zaidi kuanza kueneza injili ya Mungu kupitia nyimbo,” anasema na kuongeza kuwa amepania kuibuka miongoni mwa wanamuziki watajika miaka ijayo.

Mapema mwaka huu aliachia audio ya nyimbo inayofahamika kama ‘Jangwani’ inayoshauri wanadamu wafuate mtindo wa Ayubu hasa wakome kunung’unika bali wazidi kumwabudu Mungu hata wakijikuta katika hali ngumu kimaisha.

”Ningependa kuwaambia wafuasi wangu kuwa wasubirie video ya fataki hiyo ifikapo mwezi Mei mwaka huu,” alisema na kuongeza kuwa analenga kuendelea kusambaza injili ya Mungu kupitia uimbaji.

Mwimbaji huyu anawashukuru wazazi wake, Simon Waweru na Loice Wanjiru kwa kumwelewa na kumruhusu kuendeleza wito wake katika usanii.

”Bila shaka natoa mwito kwa wazazi wawe wakiwaunga mkono wanao katika talanta zao,” alisema na kuongeza kuwa nyakati zingine hatua ya wazazi huvuruga maisha ya wanao.

ALBAMU YA KWANZA

Licha ya pandashuka za kifedha kugharamia ada ya kurekodi tugho zake anajivunia kuachia albamu ya kwanza mwaka uliyopita iitwayo ‘Hitha’ inayosheni nyimbo sita. Nyimbo hizo ni: ‘Hitha,’ ‘Wape Neno,’ ‘ Your Presence,’ ‘Nibadilishe,’ ‘Nihuishe,’ na ‘Ningu-ngweterera.’

Mwimbaji huyu anasema anahisi ametunukiwa kipaji tosha katika masuala ya utunzi ambapo analenga kufikia hadhi ya kati ya waimbaji mahiri hapa nchini. Anasema anatamani sana kuwafikia waimbaji kama Ruth Wamuyu na Mercy Masika ambao wametunga nyimbo kama ‘Mambo sawaswa,’ ‘Twakusifu,’ na ‘Mwema,’ ‘Mwambie mtawalia.

Afrika analenga kuwapiku wanamuziki kama Upendo Nkone mtunzi wa teke kama ‘Unastahili kuabudiwa,’ na ‘Kama Mawimbi,’ kati ya zingine.

Kwa wanamuziki wa kimataifa anataka kutinga upeo wao kina Tasha Cobbs na Sinach ambao wametunga vibao kama ‘For Your Glory,’ ‘Fill me up,’ na ‘Great are you Lord,’ ‘Way maker’ miongoni mwa zingine.

MALENGO

Binti huyu aliyezaliwa mwaka 1995 anasema amepania kuendelea kuhubiri neno la Mungu ili wanadamu wazidi kumfahamu zaidi na kugeukia njia zake ili waishi maisha mazuri.

Dada huyu ambaye kwa muonekano wake ni mpole anashauri wasanii wenzake kuwa wanastahili kutunga tambo zinazosheheni mawaidha ya kuwasaidia kondoo wake Kristo.

”Wasanii tunahesabiwa kama kioo cha jamii kwa hivyo tunapaswa kuwa mstari wa mbele kuonyesha mienendo mizuri kwa wafuasi wetu,” alisema na kuongeza kuwa baadhi yao wameibuka na mitindo isivyofaa ambayo ni vigumu kuigwa na wengine.

Kadhalika anawataka wasanii wanaokuja wasiwe wepesi wa kuvunjika moyo bali watie bidii na kumwomba Mungu ili awape mwongozo katika kazi ya uimbaji.

You can share this post!

KSG Ogopa yabanwa na Dagoretti Lions

Immaculate Murugi: Serikali ipige jeki filamu nchini

adminleo