• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 5:50 AM
LEONARD ONYANGO: Viongozi wasiwatumie wanabodaboda, wanahatarisha usalama wao

LEONARD ONYANGO: Viongozi wasiwatumie wanabodaboda, wanahatarisha usalama wao

Na LEONARD ONYANGO

TAKWIMU za Mamlaka ya Usalama Barabarani (NTSA) zinazoonyesha idadi ya wahudumu wa bodaboda walioangamia katika ajali za barabarani imeongezeka kwa karibu asilimia 50 mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana, zinaogofya.

Kwa mujibu NTSA, wahudumu wa bodaboda 884 walifariki katika ajali za barabarani kati ya Januari 1 na Oktoba 31, mwaka huu.

Hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 48 ikilinganishwa na 594 waliofariki barabarani mwaka jana.

Idadi ya abiria wa bodaboda ambao waliangamia barabarani kati ya Januari 1 na Oktoba 31 mwaka huu, imeongezeka kwa asilimia 26 hadi 360 kutoka 277 mwaka jana.

Iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa, idadi ya wahudumu wa bodaboda watakaoangamia barabarani itaongezeka maradufu mwaka huu, haswa ikizingatiwa kuwa ajali nyingi hutokea Desemba.

Ongezeko la ajali za bodaboda linasababishwa na hatua ya serikali kuonekana kulemewa kudhibiti sekta hiyo.

Wahudumu wa bodaboda wanaendesha pikipiki kiholela bila kuzingatia sheria za barabarani.

Hii ni kwa sababu wahudumu wa bodaboda wamegeuka mboni ya macho ya wanasiasa – hawaguswi.

Wahudumu wa bodaboda – ambao wanakadiriwa kuwa milioni 1.2 – husaidia pakubwa wanasiasa kupata kura. Baadhi ya wanasiasa wanakodisha wahudumu wa bodaboda wawasindikize katika mikutano ya kisiasa ili waonekane kwamba wanapendwa.

Bodaboda pia wanaweza kukodishwa kuzua vurugu dhidi ya wapinzani wa mwanasiasa aliyewakodisha.

Wagombeaji wa kisiasa; kuanzia udiwani, ubunge, useneta na ugavana, hutumia wahudumu wa bodaboda wakati wa kusaka kura.

Katika siku za hivi karibuni, Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto wamekuwa waking’ang’ania wahudumu wa bodaboda kwa malengo ya kisiasa.

Masharti makali ambayo yamekuwa yakiwekwa na serikali ili kudhibiti sekta ya bodaboda, yamekuwa yakilegezwa au kutupiliwa mbali ili kuepuka kuwakwaza wahudumu hao.

Wanasiasa wanahitaji kura kutoka kwa wahudumu wa bodaboda na wala hawana haja na usalama wao.

Serikali imegeuka kuwa jibwa linalobweka tu bila kung’ata wahudumu wa bodaboda wanaovunja sheria za barabarani.

Mwaka jana, serikali ilitishia kuwakamata wahudumu wa bodaboda wanaobeba abiria bila kuwa na helimeti, bima, mavazi ya kuaksi mwangaza, nakadhalika. Lakini masharti hayo yalilegezwa baadaye.

Mwezi uliopita, serikali ilitangaza kuwa inalenga kutoa mafunzo ya wiki moja kwa wahudumu wa bodaboda ambao watakiwa kulipia Sh750.

Kwa mujibu wa serikali, hakuna bodaboda ataruhusiwa kuhudumu bila cheti cha mafunzo hayo yatakayotolewa na Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS).

Mpango huo pia huenda ukasambaratika kabla ya kutekelezwa.

Wahudumu wa bodaboda wataendelea kuangamia barabarani mpaka lini?

You can share this post!

Anafuga nguruwe jijini Nairobi, mapato ni ya kuridhisha

LUCY DAISY: Serikali ielewe uchumi umezorota, iwaruhusu...