Lugha, Fasihi na Elimu

KCSE 2025: Jinsi ukabila umeangaziwa katika riwaya ‘Nguu za Jadi’

Na JOYCE NEKESA, Kapsabet Boys High School October 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

JUMA hili tutajadili athari za ukabila tukirejelea maswali kutokana na dondoo hili.

“Siasa za majina zikashamiri katika utawala wa Mtemi Lesulia. Hata wale waliobahatika kuitwa katika mahojiano
ili wapate kazi walisumbuliwa sana. Waketwa walipitishwa katika msururu wa maswali yasiyokuwa na uhusiano wowote na kazi walizotuma maombi. Wengine walivunjika moyo, wakakataa hata kutuma maombi ya kazi serikalini. Baadhi ya wale waliobahatika waliajiriwa kwenye kampuni za watu binafsi au hata kuanzisha biashara za kibinafsi. Aidha, idadi kubwa ya wale waliomaliza shule waliajiriwa katika viwanda na mashamba ya matajiri. Wengine walihudumu katika mashamba ya maua ilhali wengine walizalisha bidhaa mbalimbali viwandani wakiwa
kama vibarua.” (Uk.45)

(a) Bainisha mbinu za kimtindo zilizotumika katika dondoo.

Tashihisi – Siasa kupewa uwezo wa kushamiri.
Nahau – …walivunjika moyo.
Takriri – Maneno “hata” na “binafsi” yamerudiwa.
Taswira – Waketwa walipitishwa…
Tashbiha – Wakiwa kama vibarua.

(b) Jadili namna ambavyo ukabila umejitokeza katika riwaya ya ‘Nguu za Jadi’

Wakule na Waketwa walikuwa na uhasama tangu jadi kwani walipigana vijembe na kuzua mabishano kila walipokongamana.
Uongozi wa Lesulia uliwaajiri Wakule pekee katika biashara zao. (Uk.17).
Chifu Mshabaha alimwambia Mangwasha kuwa Waketwa hawakuwa na akili hata ya kuchagua wachumba na ndio sababu walibaki nyuma kama makoti. (Uk.20).

Ubaguzi katika uajiri kwa misingi ya kikabila, wengi walifanya kazi ambazo hawakuzisomea. Matokeo yake yakawa vifo vingi kwani karani aliajiriwa kama daktari wa meno na muuguzi akafanya kazi ya upasuaji. (Uk.44).

Jeshi la nchi lilisheheni vijana kutoka katika jamii ya Wakule kwani Mtemi Lesulia hakuamini uongozi wa kijeshi utoke katika jamii nyingine. (Uk44).

Siasa za majina zilishamiri katika utawala wa mtemi huku Waketwa wakisumbuliwa katika mahojiano.

Wanawake Waketwa waliobahatika kuajiriwa kwa sababu ya kuolewa na Wakule walifutwa kazi walipogundulika kuwa ni Waketwa.

Vyama vya kisiasa vilivyokuwepo nchini Matuo vilicheua hisia za ubaguzi wa kijamii. Kila chama kilikuwa na idadi kubwa ya wanachama kutoka katika jamii yao. (Uk.52).

Sagilu na Sihaba walimshawishi Mbaji kuhujumu biashara za Lonare kwa sababu Mbaji alikuwa Mkule ilihali Lonare alikuwa Mketwa.

Mashauri alipomtema Sagilu na kumuunga mkono Lonare, alilazimika kuhama Mtaa wa Majuu walikoishi Wakule wengi na kwenda kuishi katika Mtaa wa Matango.

Mangwasha alimueleza Chifu Mshabaha kuwa ofisi yake ilikuwa imejazwa Wakule. (Uk.136).

Mbali na ubaguzi wa kikabila tuliojadili, kuna ubaguzi wa kitabaka na wa kijinsia.

Tathmini: Jadili athari za ukabila katika maendeleo ya taifa ukirejelea riwaya ya ‘Nguu za Jadi’.