KCSE 2025: Maudhui na mtindo katika uandishi wa insha
JUMA hili hebu tuangalie maudhui na mtindo katika uandishi wa insha. Maudhui ni hoja kuu ambazo mwandishi amekusudia kuwasilisha.
Kimsingi, mtahiniwa aandike maudhui ya kutosha – aghalabu zaidi ya manane. Aanze na maudhui mazito ya kushawishi.
Yaandikwe kiaya hasa aya za mraba ama za wima. Mstari urukwe kabla ya kuanza aya nyingine ili insha iwe nadhifu na kutenganisha hoja moja na nyingine. Kila aya iwe na maudhui moja japo yanaweza kuchangiana.
Maudhui yajadiliwe kwa kina na kwa undani. Maudhui yajitokeze wazi hasa katika sentensi za mwanzo kwenye kila aya.
Katika swali linalohitaji suluhisho, suluhisho hilo lijitokeze katika kila sentensi ya mwisho kwenye kila aya hata kama swali halikuuliza kutoa suluhisho husika.
Uhalisia na uyakinifu viwepo hasa katika insha ya kwanza na ya pili. Katika swali lililo na sehemu mbili (faida na hasara/athari/ufaafu) zote zifafanuliwe huku msimamo ukitolewa kwa kuegemea sehemu yenye hoja nyingi. Kwa ujumla, hoja ziwe kama nane au zaidi.
Kipengele cha mtindo
Tutaangalia suala la sura ambapo mtahiniwa anastahili afahamu sura za insha zote. La pili tutakaloangalia ni lile la urefu wa maneno mia nne.
La tatu ambalo tutalijadili leo katika mtindo wa insha, ni suala la nyakati na nafsi. Mtahiniwa anastahili kuwa makini sana anapolisoma swali ili kutambua mahitaji ya swali hilo kwa kurejelea wakati unaosisitizwa.
Mbali na nyakati, mtahiniwa anastahili pia kuzingatia nafsi inayosisitizwa katika swali analolijibu.
Kwa mfano swali kama hili; Umealikwa kitongojini mwenu kama mgeni wa heshima katika hafla ya kuzindua Kundi la Wasanii wa Kikwetu.
Andika hotuba utakayotoa ya kuonyesha umuhimu wa sanaa na michezo.
Hapa mtahiniwa ama mwanafunzi anayeandika insha hii amefungwa kinafsi. Itambidi ajihusishe moja kwa moja kwa kutumia nafsi ya kwanza. Hii ni kwa sababu ya kiambishi awali ‘u’ katika kitenzi ‘umealikwa’.
Fauka ya hayo, insha ya hotuba huandikwa kwa kutumia nafsi ya kwanza.