Kutafsiriwa kwa Katiba na Sheria kunafaa kuchukuliwa kama jambo la dharura
JAPO nipo mbali na kuna tofauti kubwa ya wakati, nilifuatilia kesi ya aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua vizuri kupitia teknolojia iliyopo.
Si azima yangu kurejelea masuala ya kisiasa wala kisheria yaliyohusiana na kesi hiyo. Lengo langu ni kutalii mustakabali wa lugha kutokana na yaliyojiri katika kesi yenyewe.
Kila walipokuwa wakizungumza, mawakili kutoka pande zote na majaji walirejelea Katiba na Sheria nyinginezo za nchi mara si haba. Sheria walizozirejelea hazieleweki na wengi kwa sababu mbili.
Kwanza, zimeandikwa kwa Kiingereza ambacho wengi wa Wakenya hawakielewi na pili zimeandikwa kwa lugha ya kitaaluma ambayo inawatatiza hata wanaokielewa Kiingereza.
Maoni yangu ni kwamba masuala ya kisheria yanafaa kuwa rahisi kueleweka kwa kila mtu hasa ikieleweka kwamba kutojua sheria hakukubaliki kama njia ya kujitetea.
Ndiyo sababu naendelea kukariri kwamba kuna haja ya dharura ya kutafsiri Katiba ya Kenya na Sheria zote za Bunge ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaelewa haki zao na mipaka ya haki hizo kikamilifu.
Zaidi ya hayo, itakuwa muhimu kwa wanasheria kuandika machapisho yanayosahilisha lugha ya kitaaluma ili kumwezesha mtu wa kawaida kuelewa sheria zinazomhusu.
Kuendelea kukosa kufanya hivyo ni sawa na kumnyima Mkenya uelewa wa haki zake. Ni hujuma kumhukumu mtu kwa kuvunja sheria ambayo haielewi na labda ambayo hajui kama ipo!
Bunge kama chombo kinachohusika na utunzi wa sheria, na kama mwakilishi wa mwananchi, linafaa kuongoza katika jambo hili. Najua kwamba kuna vyombo vingi vinavyohusika na sheria na vikijitolea kutafuta mtaji wa kuendesha shughuli hii, haitakuwa vigumu kuupata.