Kwa nini Kiswahili kinafaa zaidi kuwa lugha ya mawasiliano mapana barani Afrika?
NILIWAHI kudai kwamba Afrika haijakaa tutwe kuhusiana na masuala ya lugha, utamaduni, maendeleo na ukoloni mamboleo.
Wanaharakati wa lugha na wasomi, wakiwemo Wole Soyinka, Chinua Achebe (Afrika Magharibi), Mohammed Hassan Abdulaziz, Ngugi wa Thiong’o, Ali Mazrui (Afrika Mashariki), Joseph Malema (Afrika Kusini) miongoni mwa wengine, wamependekeza Kiswahili kuwa lingua franca ya Afrika.
Kwa nini Kiswahili ilihali Afrika ina lugha nyingi na ‘kubwa’, zenye wazungumzaji wengi? Je, Kiswahili kina wasemaji wangapi Afrika Mashariki na ulimwenguni?
Haiyumkiniki kutaja kwa uhakika idadi ya wasemaji wa lugha yoyote iwayo. Jambo tulilo na uhakika nalo ni kwamba, ikiwa tunajua idadi ya wasemaji wa Kiswahili Afrika ya Mashariki na Kati, tunaweza kukisia idadi ya wazungumzaji wa Kiswahili ulimwenguni.
Lugha ya Kiswahili ni mojawapo ya lugha za Kiafrika ambayo imevutia mashabiki wengi Afrika ya Mashariki na Kati na maeneo ya Maziwa Makuu, barani Afrika na ulimwenguni kwa jumla. Siwezi kusema kwa uyakinifu ni kwa nini Kiswahili kimepata ufuasi huu kiasi cha kupigiwa kura kuwa lingua franca barani Afrika.
Ikumbukwe kwamba umaarufu wa lugha mara nyingi huendana na idadi ya wazungumzaji wake. Bara la Afrika si ‘maskini’ kulingana na ramani ya lugha na idadi ya wazungumzaji wake.
Mbali na Kiswahili, Afrika pia ina lugha nyingine zenye wazungumzaji wengi ajabu. Ingawa Kiswahili ni lingua franca ya Afrika Mashariki, wanenaji asilia au watu wanaozungumza Kiswahili kama lugha yao ya ‘mama’ ni kati ya takriban milioni 5 hadi 15.