Lugha, Fasihi na Elimu

LUGHA: Neno ‘siyuko’ si la Kiswahili ijapokuwa limezagaa kwenye matumizi

Na ENOCK NYARIKI October 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

BAADHI ya wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili hutatizika wanapotumia vitenzi vishirikishi katika mawasiliano.

Kwa mfano, huwa rahisi kwa mzungumzaji mmoja kusema: ‘Wewe haupo’ badala ya ‘Wewe hupo’.

Hata hivyo, kosa moja ambalo limesheheni mno katika mazungumzo ya watu ni matumizi ya ‘siyuko’ kurejelea hali ya kutokuwepo au kutoshiriki katika shughuli fulani.

Waama, baadhi ya wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili hutamka kauli ‘mimi siyuko’ bila kufahamu kuwa ina kasoro.

Miaka michache iliyopita, katika kipindi kimojawapo cha kuigiza kwenye runinga ya Citizen, chale fulani alikuwa na mazoea ya kutumia ‘siyuko’ kwa maana tuliyoirejelea katika makala haya.

Lengo la chale mwenyewe kulitumia neno hilo kwa namna hiyo lilikuwa kuchekesha, basi.

Hata hivyo, watazamaji wa kipindi chenyewe bila kufahamu kuwa neno lenyewe lilikusudiwa kuikosoa jamii fulani ambayo hutumia Kiswahili uchwara, nao wakawepo katika kulitumia hivyo.

Hata hivyo, ni muhimu kufahamu kuwa ‘siyuko’ si neno sanifu la Kiswahili ijapokuwa limezagaa katika matumizi ya kila siku. Ukanushaji wa vitenzi vishirikishi ambavyo kimsingi huonesha ‘uwepo’ hufuata kanuni fulani maalumu.

Hakika, kiambishi {yu} hujitokeza tu katika nafsi ya tatu umoja. Ukanushaji wa ‘nipo’ au ‘niko’ unapaswa kuwa ‘sipo’ au ‘siko’.

Kwa hivyo, iwapo lengo la mzungumzaji ni kumfahamisha mwenzake kuwa hatapatikana mahali fulani wakati fulani, basi anapaswa kusema: Kesho sipo ofisini.

Ukanushaji wa ‘upo’ au ‘uko’; vitenzi ambavyo hutumiwa kurejelea nafsi ya pili umoja ni ‘hupo’ au ‘huko’.

…YATAENDELEA