Lugha, Fasihi na Elimu

NDIVYO SIVYO: Neno ‘zuru’ limejikuta likitumika katika miktadha isiyofaa

Na ENOCK NYARIKI November 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WIKI iliyopita niliangazia kosa ambalo baadhi ya wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili hulifanya wanapotumia kitenzi ‘zuru’.

Msukumo wa makala ulitokana na kauli ya mwanahabari fulani katika taarifa ambayo niliinukuu katika makala hayo. Hivi ndivyo alivyosema: “Tulipozuru katika hospitali ya Kisii…” (nimenukuu sehemu ya kauli hiyo).

Kosa – nilivyotaja wiki jana – lipo katika matumizi ya ‘zuru’ na kihusishi ‘katika’. Swali ambalo tuliliibua na ambalo tumelijibu kwa sehemu ni kuhusu neno linalopaswa kufuatishwa na kitenzi hicho. Je, tunazuru ‘katika’ au tunazuru ‘mahali maalumu’ au hata ‘mtu fulani’?

Swali hilo ndilo linalotuelekeza katika dhana ya usoelekezi na uelekezi wa kitenzi ‘zuru’. Tulitamatisha makala kwa kutaja kuwa yamkini kitenzi ‘zuru’ kina sifa ya usoelekezi na uelekezi.

Haya ni maoni niliyoyafikia baada ya kutambua kuwa licha ya toleo la awali kabisa la Kamusi ya Kiswahili Sanifu ambalo halitaji iwapo ‘zuru’ ni kitenzi elekezi au sielekezi, kamusi nyingine zimeonyesha kuwa ni sielekezi. Zipo fasili mbalimbali kuhusu uelekezi na usoelekezi wa kitenzi.

Hata hivyo, nitaazima fasili inayosema kuwa kitenzi elekezi ni kile ambacho hufuatwa na nomino ilhali kitenzi sielekezi ni kile ambacho hakifuatwi na nomino. Pengine maelezo haya yanakusudiwa kufanya makala haya yaeleweke kwa urahisi na msomaji wa kawaida.

Tunaposema kuwa fulani amezuru Nairobi, neno ‘Nairobi’ litachukuliwa kama kielezi cha mahali. Hata hivyo, katika kauli ‘nilimzuru bibi au rafiki’, dhana zinazokifuata kitenzi hicho ni nomino. Hii ndiyo sababu iliyonifanya kudai kuwa kitenzi chenyewe kinaweza kuwa elekezi na sielekezi.