Nafasi ya lugha katika kinyang’anyiro cha kuwania Uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika
ALIYEKUWA Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga, ameibua mdahalo muhimu kuhusu nafasi ya lugha kwenye siasa za kinyang’anyiro cha Uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC).
Ingawa Afrika ina ndimi nyingi, bara bado limegawanyika kwa vigezo na misingi ya lugha za watawala wa kikoloni. Kuna nchi zinazotumia Kiingereza (Anglofoni), Kifaransa (Frankofoni) na Kireno (Lusofoni).
Akizungumza jijini Addis Ababa, Ethiopia mnamo Novemba 10,2024, Bw Odinga alisema, Afrika bado inatatizwa na chembechembe za ukoloni mamboleo unaoendelezwa na lugha za kigeni.
Mataifa mengi ya Afrika bado yanatumia lugha za kikoloni kwa ajili ya mawasiliano, shughuli za kiuchumi na hata ufundishaji katika mifumo ya elimu. Hali hii ni bayana hasa ikizingatiwa kwamba uhuru wa Afrika yamkini ni wa ‘bendera’. Mifumo yetu ya kiuchumi, kiutawala na hata elimu imejengwa kwenye amara za kikoloni.
Je, Afrika imefanya juhudi zozote za kimaksudi kuibomoa miundomsingi ya kikoloni – hasa kuhusiana na lugha? Jibu ni ndio. Mwandishi Ngugi wa Thiong’o, ambaye huziona lugha za kigeni kama nyenzo za kuimarisha ukoloni, ameshiriki sana uanaharakati wa kutetea lugha za kiasili – hasa Gikuyu na Kiswahili.
Falsafa ya Ngugi ni kwamba: “Ikiwa unajua lugha zote ulimwenguni, na ukawa hujui lugha yako ya mama au lugha inayosheheni utamaduni wako, huo ni utumwa.” Katika kitabu chake – Moving the Centre: The Struggle for Cultural Freedoms (James Carrey, 1993), Ngugi anajishughulisha na suala la ‘uhamishaji wa kitovu sumbufu’ (problematic centre) kuwili. Kwanza, baina ya, na ndani ya mataifa.