Nafasi ya lugha katika kinyang’anyiro cha Uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC)
MASUALA yanayohusu lugha mara nyingi huzua hisia na mihemko mikali kwa misingi kwamba, lugha ni uti wa mgongo katika shughuli zote za mwanadamu.
Lugha hufungamana na utamaduni. Kuwanyima au kuwapokonya watu lugha yao, ni sawa na kuwavua nguo zinazositiri uchi wao.
Ni katika mkutadha huu ambapo ninatalii suala la lugha katika kinyang’anyiro cha Uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC). Kura za kupigania kiti hiki zitafanyika Februari, 2025.
Mgombea wa Kenya ni Bw Raila Odinga – ambaye tayari amezungumzia suala la migawanyo ya Afrika kwa misingi ya lugha za kikoloni; yaani Anglofoni (Kiingereza), Frankofoni (Kifaransa) na Lusofoni (Kireno).
Kwenye mieleka ya kura hiyo, Bw Odinga atamenyana na Mabw Anil Gayan (Mauritius), Mahamoud Ali Youssouf (Djibouti) na Richard Randriamandrato wa Madagaska au Bukini.
Juma lililopita, nilidai kwamba Waafrika hawajakaa tutwe katika kuangazia masuala ya kuimarisha sera za lugha katika nchi zao.
Wasomi na wanaharakati mbalimbali wamejifunga masombo katika kuzitetea lugha za Kiafrika zinazopembezwa huku wakikabiliana na nguvu za ukoloni mamboleo.
Baadhi ya wanaharakati hawa ni pamoja na Ngugi wa Thiong’o, Ali Mazrui, Alamin Mazrui, Mohamed Hassan Abdulaziz, Grace Ogot, Kimani Njogu (Kenya), Julius Nyerere (Tanzania), Wole Soyinka na Chinua Achebe (Naijeria) na Julius Malema (Afrika Kusini).
Uzi unaounganisha wataalamu hawa ni maandishi na matamshi yao yanayotetea hadhi za lugha za kiasili kupewa nafasi yao stahiki barani Afrika.