Lugha, Fasihi na Elimu

Sifa bainifu katika uandishi wa Barua Rasmi

January 28th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

JUMA lililopita tulijadili kwa kina kuhusu uandishi wa barua za kirafiki ama za kidugu. Juma hili naomba tuangazie uandishi wa barua rasmi.

Hizi ni aina za barua ambazo huandikwa kwa nia ya kuwasilisha ujumbe rasmi au ujumbe wa kiofisi. Uhusiano rasmi hudumishwa kwa kuwa wanaoandikiana aghalabu huwa hawajuani.

Barua rasmi ni chombo muhimu sana katika mawasiliano ya kiofisi. Kuna aina nyingi sana za barua rasmi. Aidha, barua hizi hutambuliwa kwa majina mbalimbali kutegemea malengo yazo.

Mathalan, wanaotafuta kazi huziita barua za ajira au za kazi; wanaoziandika wakiwa kazini kwa mashirika au taasisi nyingine huziita barua za kiofisi; wanaofanya shughuli za kibiashara nao huzitambua kama barua za kibiashara.

Wanaozituma kwa sababu ya shughuli mbalimbali rasmi huziita barua rasmi; wanaoziandika kwa ajili ya kuomba msamaha huziita barua za kuomba msamaha. Kuna barua za uhamisho zinazoandikwa kumpa mtu uhamisho wa kikazi.

Vilevile, tuna za kuomba ruhusa; za kuomba nyongeza ya mishahara na nyinginezo.

Mada zinazoshughulikiwa na barua hizi ni pana kama shughuli zenyewe.

Kwa mfano kualika kiongozi fulani au watu fulani, kutangaza mkutano, kutoa udhuru na kuomba nafasi ya kazi.

Barua rasmi kimsingi huwa na sehemu sita – anwani, marejeleo, mtajo, mada, utangulizi, mwili na hitimisho. Tutaangalia sehemu hizi juma lijalo.

Zoezi

Wewe ni mkazi wa Kaunti ya Tuonembele. Kaunti yako inapitia changamoto si haba. Umepata nafasi ya kumwandikia gavana wako barua kumweleza mambo ambayo ungependa yaimarishwe ili kuboresha maisha ya wakazi.

Andika barua utakayomtumia.