Maandamano Saba saba: Sarakasi waandamanaji wakigeuza Thika Road uga wa picha
HUKU zaidi ya kaunti 17 nchini zikishiriki maandamano Jumatatu, Julai 7 kuadhimisha siku ya Saba Saba 2025 baadhi ya washirika waligeuza barabara kuwa ukumbi wa sarakasi.
Siku ya Saba Saba, huadhimishwa kila mwaka Kenya kama kumbukumbu ya kuzinduliwa kwa utawala wa vyama vingi – mnamo Julai 7, 1990.
Maafisa wa kukabiliana na ghasia wakipambana na waandamanaji, Thika Road baadhi ya waliojitokeza walishiriki vitendo vya uchesi na sarakasi.

Katika kisa kimoja, wanadada kadha Taifa Dijitali ilikutana nao eneo la Carwash karibu na Kasarani, Nairobi wakiwa katika harakati za kunaswa picha katikati mwa barabara kuu inayounganisha jiji la Nairobi na Thika, maarufu kama Thika Super Highway.
Cha kushangaza ni kwamba wasichana hao walikuwa na mpiga rasmi, paparazzi, ambaye hakusita kuvuna hela.
“Hii ni mojawapo ya barabara ambayo ni vugumu sana kupata nafasi kupigia picha katikati na hii leo maandamano yametupa jukwaa,” akasema mmoja wa wasichana hao.

Wakiwa watatu kwa jumla, walipigwa picha ya kundi kisha kila mmoja akanaswa nyingine akiwa pekee.
Kando na tukio hilo, mabarobaro walionekana wakifanya mazoezi katika barabara ambayo utulivu ukiwa huwa yenye shughuli chungu nzima za usafiri na uchukuzi.
Magari hupita kwa mwendo wa kasi, na siku ya maandamano ya Saba Saba, Thika Road ilisalia mahame wahudumu wa bodaboda na ambulensi wakiwa ndio pekee walionekana wakipita.

Polisi walikabiliwa na kibarua kigumu kuondoa waandamanaji kwa gesi ya vitoza machozi, maandamano hayo yakifanyika kipindi ambacho Wakenya wanaelezea kukerwa kwao na ukatili wa polisi na serikali kukosa kuwapa sikio kufuatia ugumu wa maisha.
Barabara kuu zinazoingia jijini Nairobi, ziliwekwa vizuizi na polisi ili kuzuia waandamanaji kuingia katika kitovu cha jiji.
Mitaa ya ndani Thika Road, ilisalia tulivu licha ya barabara hiyo kuu kufungwa kutwa nzima.
