Makala

Mabwanyenye wa Kenya Kwanza watemea mate Gen Z

Na WAANDISHI WETU  May 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

ZIARA za mara kwa mara za Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki na viongozi wa Kenya Kwanza katika maeneo mbalimbali ya nchi, hasa katika eneo la Mlima Kenya, huku wakitoa mamilioni ya pesa kwa vikundi vya wakazi, zimezua maswali kuhusu chanzo cha pesa hizo.

Profesa Kindiki amekuwa akifanya ziara za mara kwa mara katika eneo hilo linalochukuliwa kuwa linapinga serikali ya Rais William Ruto akitoa mamilioni ya pesa kupitia kile anachokiita “mipango ya kuwezesha kiuchumi”.

Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, Prof Kindiki ametembelea maeneo ya Naivasha (Kaunti ya Nakuru), Kiambu, Lari, Gatundu Kaskazini, Limuru (Kaunti ya Kiambu), Kirinyaga Central, Mwea (Kaunti ya Kirinyaga), Kipipiri, Ol Kalou (Kaunti ya Nyandarua), Imenti (Meru), Kigumo (Murang’a) na South Mugirango (Kisii), akitoa mamilioni ya fedha kwa wahudumu wa bodaboda, vikundi vya kina mama, na makanisa.

Viongozi wengine wakuu wa Kenya Kwanza kama vile Kiongozi wa Wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot, mwenzake wa Bunge la Taifa Kimani Ichung’wah, Kiranja wa Wengi Sylvanus Osoro na msaidizi wa kibinafsi wa Rais Ruto, Farouk Kibet, pia wamekuwa wakiongoza harambee kote nchini wakitoa michango mikubwa.

Msimamo wa kutojali wa baadhi ya viongozi wa Kenya Kwanza kuhusu hali ngumu ya walipa kodi, na kuanika anasa na utajiri usiofaa, ulizua hasira katika maandamano ya kitaifa ya Gen Z mnamo Juni 2024.

Rais Ruto na baadhi ya washirika wake walionekana kama watu wajeuri, wakianika mavazi ya kifahari, magari ya bei ghali, nyumba za kifahari, na kuchangia kwa wingi katika harambee. Hali hiyo ilimlazimu Rais kupendekeza marufuku ya harambee kwa maafisa wa serikali.

“Tumeagiza Mwanasheria Mkuu kuandaa mswada wa kupiga marufuku harambee kwa maafisa wa serikali na kuanzisha mfumo wa wazi na uliopangiliwa wa michango ya kijamii, misaada na hisani,” alisema Ruto mnamo Julai 5.

Lakini inaonekana kwamba michango mikubwa imerejea. Katika baadhi ya hafla zake, Prof Kindiki huandamana na makatibu wa wizara ambao pia huchangia. Amepewa jina ‘Bw Mapesa’ kutokana na ukarimu wake mkubwa wa kifedha.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa afisa wa mawasiliano wa ofisi yake (aliyeomba kutotajwa), Prof Kindiki alisema kuwa ana marafiki nchini na ughaibuni wanaomuunga mkono katika juhudi hizi. “Amesema ikiwa marafiki wapo tayari kusaidia, kwa nini asiwasaidie wananchi?” alisema afisa huyo.

Katika hafla ya jana huko Etago, South Mugirango, alitoa mchango wa kibinafsi wa Sh2 milioni na Sh3 milioni kwa niaba ya Rais Ruto. Alisafiri kutoka Kakamega hadi Kisii kwa ndege, kabla ya kuelekea Kiambu baadaye siku hiyo hiyo.

Mifano mingine ya michango aliyoshiriki ni Runyenjes, Embu, mnamo Februari 1, 2025 ambapo alitoa Sh3 milioni kwa SACCO za bodaboda. Rais Ruto alituma Sh5 milioni. Serikali ya Embu ilitoa Sh5 milioni, na Gavana Cecily Mbarire Sh1 milioni.

Mnamo Mei 16 2025 huko Kigumo Prof Kindiki alitoa Sh5 milioni kati ya Sh16 milioni zilizotolewa na ujumbe wake. Mwakilishi wa Wanawake Betty Maina alitoa Sh1 milioni.

Katika Kaunti ya Naivasha, walitoa zaidi ya Sh15 milioni kwa wanawake na vijana.

Hata hivyo, Mbunge wa Naivasha Jane Kihara ambaye ni mshirika wa Gachagua alipinga michango hiyo akiitaja kama ‘wizi wa fedha za umma kwa kampeni za mapema’.

Katika Kirinyaga, zaidi ya vikundi 40 vya wanawake vilinufaika, huku zaidi ya Sh20 milioni zikitolewa na Prof Kindiki na viongozi waliokuwa naye.

Prof Kindiki amekuwa akizungumza sana kuhusu uboreshaji wa sekta za kahawa, chai, na maziwa nguzo kuu za uchumi wa Mlima Kenya akisema “Nikizuru sehemu zingine za Kenya mara moja, hapa nitakuja mara mbili. Nitakuwa nikirudi mara kwa mara kwa sababu kazi yangu ni kumsaidia Rais kupeleka maendeleo kote nchini.”

Wadadisi wa siasa wanasema Prof Kindiki anaendeleza mikakati ya kisiasa kujaribu kupunguza mvutano ndani ya serikali huku akikabiliana na mashambulizi ya kisiasa kutoka kwa Rigathi Gachagua na upinzani. Prof Tom Nyamache wa Chuo Kikuu cha Turkana alisema ziara za Prof Kindiki ni mkakati wa kujaribu kurejesha maeneo ambayo yanaegemea upinzani. Anajaribu kuwavutia wapiga kura.

Mchambuzi wa siasa Steve Kabita alisema:“Ziara hizi ni njia ya kutuliza upinzani dhidi ya serikali ya Kenya Kwanza, hasa baada ya mpasuko kati ya Rais Ruto na Gachagua.”

Lakini viongozi wa upinzani na baadhi ya washirika wa Gachagua wamehoji chanzo cha mamilioni hayo ya fedha.

Mbunge Edward Muriu wa Gatanga alisema: “Fedha hizi ni hongo kwa wananchi ili waunge mkono serikali badala ya kushughulikia barabara, afya, elimu ya juu, maji safi, umeme, na kupunguza ushuru mzito unaowakandamiza wananchi.”

Zack Kinuthia, mshirika wa Gachagua, alitaja zoezi hilo kama ‘aibu na dharau kwa Gen Z na wakazi wa Mlima Kenya’:

“Kuwapa chakula kwa watu wetu ni kuwadhalilisha. Hawa ni watu wanaofanya kazi kwa bidii.”

Lakini Mbunge wa Mathira Eric Wamumbi alisema:“Kupitia mpango huu tumesaidia zaidi ya vikundi 60 vya jamii. Tumewasaidia kununua vifaa kama viti, mahema na vifaa vya upishi . Hii si siasa tupu bali ni mabadiliko ya kweli.”