Farasi Arsenal na Man City walivyonyolewa bila maji
ARSENAL wanaonekana hawajijui wala kujitambua msimu 2024-2025 baada ya kupoteza mechi ya pili mfululizo ya ugenini kwenye Ligi Kuu ya Uingereza kwa kupigwa 1-0 na Newcastle katika mechi ya raundi ya 10 ugani St James’ Park, Jumamosi.
Manchester City pia walikosa lao baada ya kupoteza mikononi mwa Bournemouth kwa mara ya kwanza kabisa ligini katika mechi yao ya 21.
Vijana wa kocha Pep Guardiola walikuwa wamezoa ushindi mara 18 dhidi ya Bournemouth ikiwemo 14 kwa jumla ya mabao 45-7 na kutoka sare mara mbili kabla ya kuzamishwa 2-1 na magoli kutoka kwa Antoine Semenyo na Evanilson.
City waliojifariji na bao kutoka kwa Josko Gvardiol hawakuwa wamepoteza mechi zao zote 28 ligini mwaka 2024 kabla ya kichapo cha Jumamosi.
Vijana wa kocha Mikel Arteta walifungwa goli chungu kutoka kwa Mswidi Alexander Isak lililopatikana kutokana na asisti ya Anthony Gordon katika kipindi cha kwanza.
Arsenal wanakamata nafasi ya tano kwa alama 18 tofauti na msimu 2023-2024 walipokuwa katika nafasi ya pili wakati kama huu wakiwa na alama 24.
Msimu jana wakati kama huu, Arsenal walikuwa wamezoa ushindi mara saba na kupiga sare tatu pamoja na kujaza kimiani mabao 23 na kufungwa manane.
Mara hii, Arsenal wameambulia ushindi mara tano, kutoka sare mara tatu na kupoteza michuano miwili. Wameonyesha kuvuja katika ngome yao kwani wamekubali nyavu zao kuchanwa mara 11 nao wakaona lango mara 17.
Kompyuta maalum ya kubashiri ligi hiyo ya klabu 20 itakavyotamatika mwezi Mei 2025 iliipa Arsenal asilimia 12.2 ya kuibuka washindi, mabingwa watetezi Manchester City (82.2) nao Liverpool (5.1). Inavyoonekana, Arsenal sasa hawawezi kuorodheshwa kama mmoja wa farasi.
Wanabunduki hao waliingia mechi dhidi ya Newcastle wakiuguza kipigo cha 2-0 kutoka kwa Bournemouth (Oktoba 19) na kutoka sare ya 2-2 dhidi ya Liverpool (Oktoba 27). Inamaanisha Arsenal hawana ushindi ligini katika mechi tatu mfululizo sasa.
Kabla ya vichapo kutoka kwa Newcastle na Bournemouth na sare dhidi ya Liverpool, Arsenal walikuwa wamepoteza mara moja ligini katika mechi 25 mwaka 2024. Viwango vyao vimeshuka, hii ikiwa pia ni mara yao ya kwanza kulimwa ugenini mara mbili mfululizo tangu Mei 2022.
Liverpool nao walirejea kileleni mwa jedwali baada ya kufuta bao la Ferdi Kadioglu dakika 14 kupitia kwa magoli Cody Gakpo (69) na Mohamed Salah (72).
Nottingham Forest waliendelea kutisha msimu huu baada ya kukung’uta West Ham 3-0 kupitia mabao ya Chris Wood, Callum Hudson-Odoi na Ola Aina nao Southampton wakaonja ushindi kwa mara ya kwanza ligini msimu huu kwa kunyamazisha Everton 1-0 kupitia goli la Adam Armstrong.
Naye Jordan Ayew alitoka kitini dakika za lala-salama na kuokoa Leicester kutoka kinywa cha mamba katika sare ya 1-1 dhidi ya wenyeji Ipswich Town. Leif Davis aliweka Ipswich kifua mbele dakika ya 55.
Ipswich walisalia wachezaji 10 uwanjani beki Kalvin Phillips alipolishwa kadi nyekundu dakika ya 77. Ayew alijaza nafasi ya Victor Kristiansen dakika ya 86 na kusawazisha 1-1 dakika ya 89.