Mafunzo chungu ya Kenya kupeleka polisi nchini Haiti
MWAKA mmoja umepita tangu Kenya itume maafisa wa polisi kushiriki katika Kikosi cha kukabili magenge nchini Haiti mnamo Juni 2024.
Hata hivyo, kufikia Oktoba 2, 2025, mamlaka ya kikosi hicho huenda yakafikia kikomo isipokuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liamuae vinginevyo.
Hii ilikuwa ni operesheni ambayo Umoja wa Mataifa na serikali ya Haiti zilitegemea kuwazima magenge ya wahalifu katika taifa hilo. Rais William Ruto aliahidi kutuma maafisa 1,000 wa Kenya kuongoza kikosi hicho.Kwa sasa, kundi la kwanza la maafisa hao linakamilisha muda wao wa kuhudumu mwezi huu.
Ni mafunzo yapi ambayo Kenya imejifunza kutokana na operesheni hiyo?
Kenya huenda ililazimisha operesheni hiyo iliyopingwa nyumbani, lakini nia kuu ilikuwa ni kupata heshima ya kimataifa na kuimarisha taswira ya nchi.
Rais Ruto alisema alikuwa akijitolea kwa ajili ya ubinadamu kuwalinda raia wa Haiti, japokuwa Wahaiti wengi hawakukubaliana naye.Ingawa operesheni hiyo iliidhinishwa rasmi Oktoba 2023, ilichelewa kwa miezi tisa.
Hapo awali, mahakama ilikuwa tayari imetangaza kuwa kutuma maafisa hao ilikuwa kinyume na Katiba.Wakili Ekuru Aukot mnamo Januari 2024 aliwasilisha kesi mahakamani kupinga hatua hiyo, akisema ni kinyume cha sheria kwa maafisa wa polisi kushiriki katika oparesheni za kijeshi nje ya nchi.
Mnamo Mei, serikali ilipojitayarisha kutuma maafisa, Aukot alirejea mahakamani akisema serikali ilikuwa inakiuka maagizo ya awali ya mahakama.
Hata hivyo, maafisa hao waliondoka, na mahakama baadaye ikaidhinisha hatua hiyo.Lakini upepo wa kisiasa ulibadilika nchini Amerika, mfadhili mkuu wa kikosi hicho, ambapo Joe Biden aliondoka madarakani na nafasi yake kuchukuliwa na Donald Trump, ambaye ana msimamo wa kupunguza ufadhili wa kimataifa.
Lengo la kikosi lilikuwa kuisaidia serikali ya mpito ya Haiti kukabiliana na magenge ya wahalifu. Lakini mambo hayakuenda kama ilivyotarajiwa.
Serikali ya mpito yenyewe ilichelewa kuundwa, huku Waziri Mkuu wa mpito Ariel Henry aliyekuwa ametia saini makubaliano na Kenya, akiondolewa madarakani baada ya machafuko kuongezeka.
Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa watu waliouawa au kufurushwa makwao nchini Haiti waliongezeka kwa kiasi kikubwa mwaka 2024 ikilinganishwa na 2023.Mwaka wa 2024, watu wapatao 5,600 waliuawa kutokana na machafuko ya magenge, ikilinganishwa na 1,000 waliouawa mwaka 2023.
Waliofurushwa makwao walikuwa 703,000 mwaka 2024 dhidi ya 240,000 mwaka 2023.Ingawa takwimu hizi haziwezi kuhusishwa moja kwa moja na kikosi hicho, zinaonyesha magenge yamekuwa katili zaidi huku mamlaka ya usalama ikizidi kudhoofika.
Mtaalamu wa usalama Pius Maasai alisema kuwa maafisa wa Kenya wamefanikiwa kwa kiasi kulinda maeneo muhimu, lakini changamoto zimekuwa nyingi.“Ninaunga mkono kuongeza muda wa operesheni na kuifanya iwe rasmi chini ya Umoja wa Mataifa. Tusitumie tu askari waliopo bali tuongoze kikamilifu,” alisema Maasai.
Aliongeza kuwa maafisa wa Kenya walikuwa na uwezo wa kitaaluma lakini walikosa vifaa vya kisasa na mafunzo ya kuendelea.Jambo moja la kuvutia kwa maafisa wa Kenya ni uungwaji mkono waliopokea kutoka kwa wananchi wa Haiti, licha ya pingamizi kutoka kwa baadhi ya wanasiasa na viongozi wa magenge.
Ndani ya kambi zao, walipokea wahisani waliotoa msaada wa tafsiri na huduma nyinginezo.Msemaji wa kikosi, Bw Jack Ombaka, alisema kuwa maafisa hao walipokelewa vyema na raia, kinyume na madai ya viongozi wa magenge.
Kamanda wake, Bw Godfrey Otunge, aliwahi kusema: “Kenya kama nchi inayoongoza kikosi cha mataifa mengi nchini Haiti inashukuru kwa mapokezi na imani ya watu wa Haiti pamoja na mashirika mbalimbali ya ndani na kimataifa. Tunajitahidi kutekeleza majukumu yetu chini ya Azimio la Baraza la Usalama la UN Na. 2699 la mwaka 2023.
Maafisa walioko Haiti ni miongoni mwa waliofunzwa zaidi katika polisi Kenya. Hata hivyo, tangu Juni 2024, afisa mmoja ameuawa na mwingine bado hajapatikana.Konstebo Samuel Kaetuai Tompoi aliuawa Februari 23, 2025 kwa kupigwa risasi na genge wakati wa operesheni katika eneo la Ségur-Savien.
Afisa mwingine, Benedict Kuria, bado hajulikani alipo tangu alipotekwa Machi 2025 katika shambulio la ghafla.
Mke wake, Miriam Watima, alisema: “Tumejaribu kupata habari kutoka kwa serikali mara kadhaa, lakini imekataa. Hatujui cha kufanya tena.”
Familia sasa imefungua kesi mahakamani kuishinikiza serikali kutoa taarifa rasmi kuhusu hali ya Kuria.Kutokana na hali mbaya ya hospitali nchini Haiti, baadhi ya maafisa waliojeruhiwa hupelekwa Jamhuri ya Dominica kwa matibabu ya dharura.
Mara kadhaa kikos kimeomba msaada wa vifaa. Wakati Rais Ruto alipotembelea Haiti mwaka jana, afisa mmoja alizungumzia wazi ukosefu wa vifaa.