Mahakama yakataa kufuta jina la mume kutoka kitambulisho cha mke wa zamani
MAHAKAMA Kuu imetupilia mbali kesi iliyowasilishwa na mwanamume akitaka jina lake liondolewe kutoka kwa kitambulisho cha kitaifa cha mke wake wa zamani na vyeti vya kuzaliwa vya watoto wawili wa mwanamke huyo.
Jaji wa Mahakama Kuu Rhoda Rutto aliamua kuwa mahakama haina mamlaka ya kuamuru Msajili wa Uzazi na Vifo kufuta jina la mwanamume huyo kutoka kwa kitambulisho cha mke wa zamani na vyeti vya kuzaliwa vya watoto wake.
“Mlalamishi amejikita katika vifungu vya 12 na 28 vya Sheria ya Usajili wa Uzazi na Vifo. Vifungu hivyo havipatii mahakama hii mamlaka ya kutoa amri anazotaka. Mamlaka ya kufanya marekebisho imekabidhiwa Msajili,” alisema Jaji Rutto.
Aliongeza kuwa kutoa amri hizo kungekuwa ni kuingilia mamlaka ya Msajili ambaye, licha ya kutajwa kama mhusika katika kesi hiyo, hakukabidhiwa stakabadhi za kesi.
Katika ombi lake, mwanamume aliyetambuliwa kama JMM alisema alikutana na mpenzi wake wa zamani (CMM) mwaka wa 2013 na wakaanza kuishi pamoja. Alikuwa na mtoto mmoja kutoka ndoa ya awali, naye mwanamke alikuwa na watoto wawili.
Alisema alikubali kwa hiari jina lake liongezwe katika kitambulisho cha mwanamke huyo kama ishara ya upendo, na hivyo mwanamke akabadilisha jina lake kuwa CMM.
Vivyo hivyo, alikubali jina lake liwekwe katika vyeti vya kuzaliwa vya watoto wawili wa mwanamke huyo, aliozaa kutokana na uhusiano wa awali.
Vyeti hivyo vilitolewa Januari 2024 na Idara ya Usajili wa Uzazi na Vifo, Machakos.
Mahakama ilielezwa kuwa uhusiano huo ulianza kuvurugika pale mwanamke alipodaiwa kuwa katili dhidi ya binti wa JMM kutoka ndoa ya awali. Alisema alipomkabili, mwanamke huyo alimtusi na hata kumshambulia kimwili, hali iliyomlazimu kukimbia.
Aliporudi nyumbani, aligundua mwanamke huyo alikuwa ameondoka na watoto wake. Juhudi za kuleta upatanisho kupitia kwa wazazi wa mwanamke huyo hazikufaulu.
JMM alisema kuwa mwanamke huyo alianza kutishia wanawake wengine aliokuwa akijaribu kuanzisha uhusiano nao, akidai bado wao ni wanandoa halali – madai ambayo alihusisha na matumizi ya jina lake katika stakabadhi za kuwatambulisha.
Aliomba mahakama iamuru Msajili afute jina lake kutoka kwa kitambulisho cha mwanamke huyo na vyeti vya watoto ili aweze kuendelea na maisha yake.
Hata hivyo, mwanamke huyo hakuwasilisha jibu kwa ombi hilo. JMM alisisitiza kuwa hakuwahi kumuoa rasmi wala kuzaa watoto hao wawili.
Lakini Jaji Rutto alitupilia mbali ombi hilo, akisema halina msingi kwa kuwa JMM hakuthibitisha kuwa alijaribu kumshirikisha Msajili kutekeleza matakwa yake.
“Kuwasilisha kesi mahakamani kabla ya kujaribu njia za kiutawala kupitia Msajili ni kutumia vibaya mchakato wa mahakama,” alisema Jaji.
Aliongeza kuwa kwa kukwepa hatua hizo, mwanamume huyo alikuwa akijaribu kuruka utaratibu wa kisheria.
Mahakama pia ilibainisha kuwa JMM mwenyewe alikiri kuwa alikubali jina lake liongezwe kwenye stakabadhi hizo.