Mahakama yaruhusu watumishi wa umma wauze pombe
SERIKALI imepata pigo baada ya mahakama kuu kuharamisha marufuku ya kuzuia watumishi wa umma wakiwemo maafisa wa polisi, watumishi katika Halmashauri ya Ukadiriaji Ubora wa Bidhaa (Kebs) na Mamlaka ya Mapato (KRA) kuwezekeza katika biashara ya pombe.
Katika uamuzi uliotolewa Jumatano –Aprili 15,2025 Jaji Roselyn Aburili alifutilia mbali maagizo yaliyotolewa na Naibu Rais Prof Kithure Kindiki mnamo Machi 6, 2024 alipokuwa Waziri wa Masuala ya Usalama kuhusu biashara ya kuuza pombe na wanaopasa kuiuza.
Jaji Aburili alisema maagizo hayo ya Prof Kindiki yanakinzana na Katiba kuhusu uwekezaji katika biashara ya pombe.
Maagizo 25 aliyotoa Prof Kindiki yalipiga marufuku watumishi wa umma kuwekeza katika biashara ya kuuza pombe.
Prof Kindiki alikuwa ametoa maagizo hayo katika jitihada za kuangamiza uuzaji pombe haramu ambayo madhara yake ni makubwa nchini.
Katika uamuzi wake, Jaji Aburili alisema amri hiyo ya Prof Kindiki inakinzana na Katiba na imepotoka katika maelekezo ya utoaji leseni za baa.
Marufuku hiyo ya Prof Kindiki ilizima Kebs na KRA kutoa idhini kwa wenye viwanda vya kutengeneza pombe wanaotengeneza pombe za bei nafuu.
Hatua nyingine ambayo Prof Kindiki aliyotoa ni uuzwaji wa pombe karibu na taasisi za elimu, makanisa na mitaa ya kuishi wakazi mijini.
Mahakama ilisema Prof Kindiki alitoa maagizo hayo kwa lengo la serikali kudhibiti uuzaji wa pombe.
Jaji Aburili alisema agizo hilo la Prof Kindiki lilitwaa mamlaka ya bunge la kutunga sheria na idara zinazopasa kudhibiti biashara ya pombe.
Mahakama ilisema maagizo ya Prof Kindiki yalivuruga mwongozo wa “utenganishwaji wa mamlaka na matumizi yake.”
Jaji Aburili Akasema, “Maagizo makuu hayawezi kuchukua mahala taasisi zilizopewa mamlaka ya kutunga sheria kama vile Bunge. Kwa kutoa agizo la kutwaliwa kwa bidhaa bila ya kufuata mwongozo uliowekwa ni ukiukaji wa sheria na mwongozo pamoja na utaratibu uliowekwa na Bunge.”
Prof Kindiki alitoa maagizo hayo baada ya mkutano wa maafisa wakuu serikalini ulioongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kujadili njia za kuangamiza pombe haramu yenye madhara makuu na inayoleta maafa katika jamii.
Wakati wa mkutano huo wa Machi 6 2024 Bw Gachagua alisema pombe hiyo haramu ilisababisha vifo vya wabugiaji 23 kaunti ya Kirinyaga.
Bw Gachagua alisema utekelezaji wa sheria za udhibiti wa pombe zilikumbwa na changamoto kadha wa kadha.
Katika uamuzi huo Jaji Aburili alisema washikadau katika biashara hiyo kama vile wenye mahoteli, wenye mabaa, wauzaji vileo na wanachama wa chama cha wenye hoteli na wauzao pombe nchini (HLTAK) hawakuulizwa maoni yao kabla ya maagizo hayo kutolewa.
Jaji Aburili alirejeshea kamati za kaunti kuhusu biashara ya pombe kutoa leseni na kudhibiti uuzaji pombe.