Makala

MAJI: Mabwanyenye wa maua wanavyotesa walalahoi Nakuru

May 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

NA RICHARD MAOSI

Mabwenyenye kutoka Kaunti ya Nakuru na Baringo wanaokuza maua, wamelaumiwa na wakazi kwa kugeuza mikondo ya maji, kuelekea kwenye mashamba yao huku wakiacha idadi kubwa ya walalahoi wakitaabika.

Maeneo yaliyopata pigo ni kuanzia Rongai, Kambi ya Moto, Emgwen, Kabarak na Kabarnet farm maeneo yanayopakana na mji wa Nakuru.

Ingawa msimu wa mvua umefika bado mito imekauka, huku raia wengi wakilazimika kubeba mitungi ya maji,hadi kwenye maeneo ya wawekezaji wa kibinafsi wanaomiliki visima vya kuunda maji.

Taifa Leo Dijitali ilizuru Eldama Ravine na kuzungumza na Joel Biwott, mwenyekiti anayesimamia mradi mpya wa maji ulioanzishwa na serikali kuu 2019.

Alisema muundo mpya wa Emgwen umewapatia wakazi matumaini,ikiwa ni kwenye hatua za mwisho.

Kwa upande mmoja matajiri wamekuwa wakijitetea kwa kudai, wanachangia nafasi nyingi za ajira miongoni mwa vijana na kuchangia uchumi wa nchi.

Mto Rongai ambao umefungiwa na mabwenyenye wanaokuza maua katika eneo la Emgwen. Picha/ Richard Maosi

“Wakati mwingine inalazimu wanyama wa mwituni kuzozana na wakazi ,tangu mto Rongai uanze kukauka,”alisema.

Wakulima wengi wamekadiria hasara kwa kupoteza mbuzi na ng’ombe, wanaoishia kuangamizwa na fisi wanaofika katika boma za watu.

Joel anasema kabla ya ghasia za uchaguzi 2007-2008 wakazi wa Kampi ya moto walichanga fedha za kununulia paipu za maji.

Aidha walipata ufadhili kutoka kanisa moja la kikatoliki hapo Rongai,na kuteremsha maji kutoka kwenye milima ya Kaptunga.

Walifanikiwa kuyaingiza maji kwenye tanki iliyoweza kuhimili lita 50,000, na baada ya muda mfupi maji yalikuwa yamejaa na kuwahudumia mahitaji ya watu.

Hili ni eneo la kuuzia maji linalofahamika kama Kambi ya Moto Eldama Ravine. Picha/ Richard Maosi

Lakini 2008 maji yalikatika ghafla baada ya matajiri kufungia mto Kiptunga uliokuwa ukielekeza maji ndani ya tanki hilo kongwe.

Baadaye kwa ushirikiano na kaunti ya Nakuru wakazi waliazimu kuunganisha maji ya Molo river,bila kupata mafanikio.

Fedha zilimalizika kilomita moja kabla ya mradi huo kukamilika.

Joel anasema serikali inafaa kuondoa sheria za mito zinazowapatia baadhi ya wakulima, uhuru wa kutekeleza kilimo kando ya mito.

“Wakulima wengine kwa sababu ya vibali kutoka kwa serikali,wamekuwa wakitumia maji ya mito vibaya kunyunyizia nyanya, hoho na matikiti ,” Joel akasema.

Awali tanki hili lilihifadhi lita 50,000 lakini wawekezaji wa kibinafsi walikatiza maji ya mto yaliyoingiza maji. Picha/ Richard Maosi

Anawalaumu wageni wanaokodisha mashamba kutoka kwenye kaunti jirani kwa kutoa hongo kwa serikali za kaunti ya Nakuru na Baringo,ndiposa wanachangia uharibifu wa vyanzo vya maji.

Kwa sababu ya uhaba wa maji viungani mwa mji wa Nakuru, serikali ya kitaifa imeanzisha mradi wa kujenga tanki litakalohifadhi lita milioni moja hivi karibuni.

Ujenzi wenyewe umefikia hatua za mwisho kabla ya jengo hilo kuwasilishwa rasmi kwa serikali ya kaunti itakayosimamia usambazaji wake.

Kabla ya kuanzisha mradi huu KENHA walidadisi miundo misingi, na tayari wapo kwenye harakati za kuunganisha paipu kutoka mto Chemususu.

Mkazi wa Rongai Junction akitumia baiskeli yake hadi eneo la Kabarak kilomita 10 akitafuta maji. Picha/ Richard Maosi

George Lagat anasema amekuwa akiishi eneo bunge la Rongai kwa zaidi ya miaka 43,lakini anashangaa kuona mto Rongai ukiwa umekauka msimu huu wa mvua.

Anasema vijana wa Rongai waliwahi kufanya maandamano kushinikiza mikondo ya maji ifunguliwe,lakini siku chache baadaye tena ikafungwa.

“Matajiri watatu hivi wanaojulikana ndio wamefungia maji ya mto Rongai unaopaswa kuwafaidi wakazi kwa matumizi ya nyumbani,” akasema.

Anasema washika dau hawajaitisha mkutano wa kuzungumzia swala hili.

Ikumbukwe eneo la Rongai halina maji ya mifereji hadi karne hii,ndiposa wakazi wengi wanategemea mito.

“Endapo tanki mpya itamalizika,bila shaka matatizo ya wakaziwa Emgwen yatatatuliwa,” akasema

George Lagat akionyesha ujenzi unaondelea kwenye mradi mpya wa kuhifadhi maji. Picha/ Richard Maosi

Maji yataelekezwa kutoka chemichemi za Chemususu hadi kwenye tanki mpya inayoweza kuhifadhi lita milioni moja ya maji.

Anaona ni afadhali serikali ianzishae miradi ya kukuza miti ya bamboo inayosaidia kuhifadhi kiasi kikubwa cha maji.

Alfred Keitany, mkazi wa Rongai Junction anasema amezoea kutumia baiskeli yake kila siku hadi Kabarak, kilomita 10 kununua maji.

Yeye ni mchuuzi wa maji na anasema tangu mto Rongai ufungiwe na mabwenyenye amelazimika kununua maji ili auzie mikahawa asipoteze wateja wake.

“Ingawa inachosha wakazi wa Emgwen tunatarajia mto Rongai utakuja kufunguliwa siku moja lau sivyo wakazi hatutakoma kupambana na serikali za kaunti zinazoshirikiana na mabwenyenye,”aliongezea.

Ingawa swala la uchafuzi wa maji limepungua, wakazi wanaamini mradi mpya ulioanzishwa na serikali utawasaidia wakazi wa mashinani.