Makala

Makaa yatokanayo na kinyesi cha binadamu yaendelea kupata umaarufu Nakuru

July 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na PHYLLIS MUSASIA

KATIKA baadhi ya mikahawa eneo la Barut na maeneo mengine mjini Nakuru, makaa yatokanayo na kinyesi cha binadamu yameanza kupata umaarufu mkubwa.

Ni makaa ambayo waliowahi kutumia wanasema hayana harufu.

‘Makaa-dot-com’ kama vile yanavyojulikana Nakuru, ni makaa ya kipekee yanayotengenezwa na kampuni ya maji ya Nakuru (NAWASSCO) chini ya usimamizi wa kampuni ya NAWASSCOAL.

Kulingana na meneja mkurugenzi wa kampuni ya NAWASSCOAL Bw John Irungu, shughuli ya kutengeneza makaa hayo huanza kwa kuchota uchafu wa choo kutoka sehemu mbalimbali mjini na hata mashinani na kisha kuisafirisha hadi katika sehemu maalamu ambapo kampuni ya NAWASSCOAL huendesha shughuli zake.

“Kuna mashine spesheli ambazo hutumika katika shughuli nzima. Hii ni baada ya uchafu huo kukaushwa kwa muda wa wiki mbili au tatu hivi ndani ya greenhouse,” anaeleza Bw Irungu.

Viwango vya juu vya joto kwenye nyumba hizo huwa na uwezo wa kuondoa takribani asilimia 70 ya maji kutoka kwenye uchafu huo.

Wakati huo huo, uchafu huo huwa umeandaliwa tayari kwa mchakato wa kaboni.

Bw Kevin Ochieng akiwa katika sehemu ya kukausha kinyesi cha binadamu kabla ya kuwekwa kwenye mashine za kutengeneza makaa ya kisasa. Picha/ Phyllis Musasia

“Kwenye mchakato huu, uchafu uliokaushwa huwekwa katika viwango vingine vya joto kiasi cha nyuzijoto 700 hadi 800. Gesi zote mbovu huchomwa katika mchakato huu na kuondoa harufu mbaya,” anaeleza mhandisi Kelvin Ochieng ambaye ni afisa mzalishaji katika kampuni ya NAWASSCOAL.

Pia, wakati huo ndipo uchafu huo husagwa na kuwa laini kwa kutimia mashine kabla ya kuchanganywa na unga wa mbao ambao pia huwa umekaushwa na kuondolewa unyevu katika kiwango cha nyuzijoto 300.

Bw Ochieng anasema kuwa mchanganyiko huo huongezwa viwango sawia vya molasses na kuchanganywa kabisa.

Molasses hutumika kuunganisha chembechembe za mchanganyiko huo pamoja ili kuafikia shepu ya mvirongo kamili.

Baadaye huwekwa katika mashine iliyoundwa kwa mfano wa dramu.

“Mchanganyiko huu huzungushwa ndani ya mashine hii ambayo hutumia nguzu za umeme. ‘Molasses’ huendelea kuongezwa hadi shepu zinazohitajika kutoka kwenye mchanganyiko huo kuonekana,” akaeleza Bw Ochieng.

Kuanzishwa mradi

Mradi huu ulianzishwa mwaka wa 2017 chini ya mpango maalumu wa usafi katika kaunti ya Nakuru.

Baadaye, ulipigwa jeki na Muungano wa Mataifa ya Ulaya (EU).

Washirikishi wengine kwenye mradi huo ni pamoja na kaunti ya Nakuru, Umande Trust, Vitiens Evides International na shirika la maendeleo la Uholanzi.

Bi Rosemary Kilo, mkazi wa Nakuru anaeleza kwamba, mara ya kwanza aliponunua ‘makaa-dot-com’ na kupeleka nyumbani, kila mmoja akiwemo mumewe alikuwa na utata kuhusiana na matumizi ya makaa hayo.

“Walionekanaa kutoridhika nayo kwani walidhani yanatoa harufu mbaya yatakapo washwa,” akasema.

Lakini anasema alipowasha jiko na kupika chajio siku hiyo, alishangaa kuona kwamba kila mmoja ametulia huku wanawe wakiwa msitari wa mbele kutaka kujionea jinsi makaa hayo yanavyopika kwa haraka bila kutatiza.

Kulingana na Bw Irungu, mradi huo ulianzishwa ili kukabiliana na matatizo ya maswala ya usafi hasa katika maeneo ya mabanda wanapokaa maelfu ya wakazi wa Nakuru.

Nchi ya Keya ni mojawapo ya nchi ambazo zinajaribu sana kuzingatia hali salama ya usafi kwa raia wake kwa kubadilisha uchafu wa choo na kuwa bidhaa muhimu ya kutega uchumi.

Kulingana na Bw Ochieng’ haikuwa rahisi kwa kampuni hiyo kuanzisha shughuli zake.

Aidha idara ya afya ya kaunti ilizua maswali si haba kuhusu jinsi kampuni hiyo ingeweza kukusanya uchafu wa choo, kusafirisha na kisha kuibadilisha na kuwa bidhaa ya kutumia nyumbani bila kuvunja sheria.

Kuwashawishi wakazi kutumia bidhaa zake pia ilikuwa vigumu zana kwa kampuni ya NAWASSCOAL.

“Tujaribu kila tuwezalo kufanya uhamasisho kwa wakazi wa Nakuru na hata watu wa nje kuhusu ubora wa bidhaa zetu. Changamoto zilikuwepo lakini hatukufa moyo,” anaeleza.

Kilichochangia kupata wateja, Bw Ochieng anasema, ni kwamba ni marufuku yaliyowekwa na serikali kukata miti kiholela kwenye misitu kama vile Mau.

“Marufuku hayo yalisitisha uchomaji mwingi wa makaa ya kawaida na kutupa fursa ya kuingia kwenye soko,” anaongeza.

Kampuni hiyo sasa inazalisha takribani tani nane kila mwezi na kulingana na Bw Ochieng, kiwango hicho kinatazamia kuongezeka hadi tani 15 miezi kadhaa ijayo ikizingatiwa ukuaji wa soko ambalo limedhihirika siku za hivi majuzi.

Makaa hayo hutumika nyumbani, hotelini, shuleni na kwenye hospitali nyingi ndani na nje ya Kaunti ya Nakuru.

Kilo mbili za makaa-dot-com huuzwa kwa Sh60 huku kilo tano zikiuzwa kwa Sh150.

Kilo 25 zinauzwa kwa Sh750 na Sh1,500 kwa kilo 50.