Makala

MAKALA MAALUM: Masaibu tele kwa familia ambayo iliorodheshwa kama 'kundi la wahalifu'

August 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 5

Na WINNIE ATIENO na CHARLES LWANGA

WALIORODHESHWA miongoni mwa makundi ya wahalifu yaliyopigwa marufuku, kama vile Mungiki, lakini familia ya Charo Shutu haikuogopa wala kuvunjika moyo kwani imekuwa ikiendelea kutetea haki yao ya ardhi kwa bidii.

Familia hiyo yenye zaidi ya watoto 400, ambayo huenda ikawa ndiyo kubwa zaidi nchini, bado inajaribu kuuliza maswali kuhusu sababu iliyopelekea serikali kuiorodhesha miongoni mwa makundi haramu kwa miaka 10 sasa baada ya baba yao kufariki.

“Serikali imeendelea kutuchukulia kuwa wahalifu, wauaji na hata magaidi, kati ya majina mengine mabaya kwa sababu tunamiliki vipande vikubwa vya ardhi. Lakini hii ni kwa sababu kuna watu fulani waliotaka kunyakua vipande vyetu vya ardhi yetu ya ukubwa wa ekari 477 iliyoko Malindi, ambayo baba yetu alimiliki tangu enzi za ukoloni. Tulitetea ardhi yetu kwa machozi na vitisho vya kuuawa,” anasema msemaji wa familia hiyo Bw Japheth Noti Shutu.

Masaibu ya familia ya Shutu yalianza mnamo 2010 wakati aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani marehemu George Saitoti, kupitia notisi kwenye gazeti rasmi la serikali nambari 12585 ya Oktoba 18, 2010, alipiga marufuku makundi 33, ikiwemo Familia ya Charo Shutu, iliyoorodheshwa pamoja na kundi la kigaidi la al-Shabaab.

Hata hivyo, familia hiyo ikiongozwa na Bw Noti iliwasilisha kesi kortini kupinga notisi hiyo iliyoiorodhesha miongoni mwa makundi ya uhalifu kutokana na sababu kwamba walitetea ardhi yao. Walishinda kesi hiyo.

Hata hivyo, wakati huu, familia hiyo ingali na kesi 24 ambazo hazijaamuliwa katika mahakama ya Malindi kuhusu ardhi baada ya wao kuwashtaki watu waliodaiwa kunyakua ardhi zao.

“Hatua ya serikali kutuorodhesha miongoni mwa makundi haramu imepelekea baadhi yetu kukosa nafasi za ajira kwa kuwa na jina, Charo Shutu, anasema.

Anaeleza kuwa kufuatia hatua hiyo, watu wengi wa familia hiyo walikamatwa.

“Mwanangu kwa jina Eddy Fondo, 37 naye aliuawa,” anasema kwa machungu.

Bw Noti anaongeza kuwa, wakati mmoja maafisa 12 wa polisi walijaribu kumkamata kuhusiana na mzozo wa ardhi ya ekari 24, ambayo haikutumiwa “lakini ni mali yetu tangu zamani.”

Makundi haramu

Lakini Naibu Kamishna wa kaunti anayesimamia Malindi, Karung’o Kamau, anasema serikali iliorodhesha familia hiyo miongoni mwa makundi haramu kuanzia mwaka wa 2003 kwa sababu walikuwa wakiwaogofya wawekezaji.

“Wawekezaji waliokuwa wakinuia kuanzisha biashara Malindi walipata pingamizi kutoka kwa familia hii kwa sababu ilidai kumiliki ardhi iliyotarajiwa kutumiwa kwa ujenzi wa miradi,” akasema.

Kwenye mahojiano, Bw Kamau ambaye amehudumu Malindi kwa kipindi cha miaka mitatu baada ya taharuki ya serikali na familia ya Charo Shutu kutulia, alisema familia imekuwa ikidai kuwa inakinga ardhi ya akina babu zao dhidi ya wanyakuzi.

“Matukio haya yote yalitokea kabla ya kuzinduliwa kwa Katiba ya sasa mnamo 2010. Familia hiyo inamiliki vipande vikubwa vya ardhi Malindi na haikuamini idara ya mahakama hadi Katiba ya sasa ilipoanza kutekelezwa na shida yao ikaanza kushughulikiwa kupitia Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC),” afisa huyo alisema.

Bw Kamau, ambaye alianza kuhudumu Malindi mnamo 2016 alisema ni baada ya uchunguzi kuhusu umiliki wa ardhi hiyo kufanywa ukweli ulipobainika.

“Familia hiyo haikuwa na makosa kwani ilikuwa ikijaribu kuwasilisha malalamishi yake kuhusu unyakuzi wa ardhi. Walikuwa wakitetea ardhi yao na haikuwa sawa kwa serikali kuwaorodhesha miongoni mwa makundi haramu,” akasema.

Historia yao ilianza mapema mwaka wa 2000 wakati baba yao Charo Shutu Masha, ambaye alikuwa mwanamuziki shupavu, alikuwa mtu aliyeogopewa zaidi Malindi kwa kupinga unyakuzi wa ardhi.

Juzi, Taifa Jumapili ilikutana na watoto wa kiume wa marehemu Charo Shutu Masha katika chuo cha mafunzo ya kadri kilichojengwa katika ardhi yao.

Walijitambulisha kama Bw Japheth Noti Shutu na mkewe Cynthia, Joseph Patrick Charo, Samson Chula na Harrison Charo Shutu.

“Hii ni sehemu ndogo zaidi ya familia yetu; tuko wengi. Tukiitisha mkutano wa familia tunaweza kujaza uwanja wa michezo,” anasema Shutu (Harrison).

Bw Noti, 63, maarufu kama ‘Janja’ kwa machungu alielezea walivyoteswa, kuchapwa na kutiwa nguvuni kwa kutetea ardhi yao dhidi ya wanyakuzi.

“Baba yangu alikuwa na wake 48 na takriban watoto 420. Alikuwa mfanyakazi katika baraza la manispaa wakati wa enzi ya ukoloni. Aidha, alikuwa mwanamuziki wa haiba kubwa ambaye mara kadhaa aliwatumbuiza Rais Jomo Kenyatta na makamu wake Daniel Moi katika hafla mbalimbali,” asema.

Anasema babake alifuata nyayo (kuoa wake wengi) za Bw Kabwere Wanja ambaye alikuwa maarufu zaidi eneo zima la Pwani na ambaye alikuwa na wake 300. Nyakati hizo kuoa wake wengi kuliashiria kuwa mtu alikuwa tajiri.

Bw Noti anasema kuwa babake alithamini ardhi ambako waliendesha kilimo cha pamba, mahindi, sesame na korosho. Anafafanua kuwa baba yao alirithi ardhi kutoka kwa babu yake-Shutu Masha- ambaye alikuwa Chifu Mkuu katika enzi za ukoloni.

Alieleza jinsi babake alitoa ardhi kwa Idara ya Magereza Nchini (KPS) kuendeshea kilimo katika eneo la Ngala, kabla ya shamba hilo kuhamishwa hadi eneo la Mtangani.

“Idara ya Magereza iliomba ardhi kwa nia njema na babangu akaipatia. Lakini idara hiyo ilipopata ardhi katika eneo la Mtangani, baba alirejesha ardhi yake,” Bw Noti anasema.

“Lakini baada ya ardhi kurejeshwa kwetu watu fulani walitokea na kuinyakua wakati wa enzi ya utawala serikali za manisipaa,” anasema.

Bw Noti anaongeza kuwa aliweza kuwatambua watu walionyakua ardhi hiyo kwani walikuwa na wafanyabiashara wa asili ya Kiarabu na viongozi wa lililokuwa Baraza la Manisipaa ya Malindi.

“Nakumbuka kabisa enzi hiyo kana kwamba ni jana. Walikata miti ya minazi katika ardhi hiyo iliyoko katika eneo la Mbuzi Wengi. Na tulipigwa na kukamatwa na polisi tulipojaribu kuwapiga wanyakuzi hao,” anaeleza.

Anaongeza kuwa Chifu wa eneo hilo na Mkuu wa Wilaya walikuwa washirika katika njama hizo za unyakuzi wa ardhi yao.

Baadaye, Bw Noti anaongeza, Baraza la Manispaa pia lilianza kudai ardhi yao iliyoko eneo la Mbuzi Wengi, hatua ambayo ilizidisha vita vyao dhidi ya wanyakuzi wa ardhi.

“Tulipinga njama zote za kunyakuliwa kwa ardhi yetu bila woga. Tuna vyeti vyote vya umiliki wa ardhi hizo na ndipo tukawasilisha kesi mahakamani kuwashtaki wanyakuzi hao. Kwa bahati nzuri tulishinda kesi,” anasema.

Ilikuwa ni baada ya familia hiyo kushinda kesi ambapo aliyekuwa Meya wa Malindi Mzee Randu aliandika barua akithibitisha kuwa familia ya Charo Shutu ndio wamiliki halali wa ardhi hiyo.

UPINZANI

Bw Noti anasema juhudi za aliyekuwa OCPD wa Malindi King’ori Mwangi kuitetea familia hiyo ili isiorodheshwe miongoni mwa makundi haramu ya kihalifu ziligonga mwamba kutokana na upinzani aliopata kutoka baraza la Manispaa na Kamati ya Usalama, Malindi.

Anasema familia hiyo ilipatia Manispaa ya Malindi ardhi ya kujengea kituo cha zima moto, ambacho sasa kinajulikana kama “Epic Fire Station”, lakini ikauza kwa mstawishaji wa kibinafsi.

“Ardhi ya kituo cha zima moto ilitolewa na familia baadaye iliuziwa mfanyabiashara mmoja wa Malindi kwa Sh7 milioni kwani manispaa ilidai walihitaji pesa za kuwalipa madiwani na wafanyakazi,” akasema.

Maelezo ya Bw Noti yanaonekana na kuwasawiri viongozi wa iliyookuwa manisipaa wa Malindi kama wenye tamaa kwani ilidaiwa waliuza na kujigawia vipande fulani vya ardhi vya manisipaa hiyo.

“Tulichoshwa na tamaa ya viongozi hao ndipo tukachukua tena ardhi ya ukubwa wa ekari tatu katika eneo la Mbuzi Wengi iliyokuwa ikitumiwa kama Uwanja wa Maonyesho ya Kilimo. Hii ni licha ya kwamba sehemu fulani ya ardhi yote ya ekari 24 ilikuwa tayari imenyakuliwa. Wakati huu tunapambana na wanyakuzi hao kortini,” anasema.

Bw Noti anasema baada ya hapo uwanja wa Maonyesho ya Kilimo ulihamishwa hadi eneo la Sabaki eneo linalojulikana kama Kwa Moi. Lakini duru zinasema kuwa ardhi hiyo pia iliuziwa wastawishaji wa kibinafsi na Uwanja wa Michezo ukauziwa watu wa Jamii ya Bohora.

“Tumewasilisha kesi kortini na tukaweza kurejesha ardhi ya uwanja wa michezo. Sasa nimejenga vibanda vya kibiashara vya kukodiwa ili ardhi hiyo isikae tupu,” anasema.

Lakini inasikitisha kuwa licha ya familia hiyo kumiliki zaidi ya ekari 477 ya ardhi, anasema Bw Noti, takriban watu 350 wa familia hiyo sasa ni maskwota baada ya ardhi yao kunyakuliwa.

“Je, utakaa kitako huku ukiwaruhusu watu kunyakua ardhi yako? Lakini ukijitetea unakamatwa” anauliza Bw Noti

“Tunateswa kiasi hiki ilhali tumeipa serikali vipande kadha vya ardhi kutumia kwa ujenzi wa miradi kama vile kituo cha mabasi cha kisasa, Shule ya Upili ya Malindi, sehemu ya uwanja wa ndege wa Malindi, afisi za serikali kati ya miradi mingine,” anasema.