• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 7:02 PM
MALENGA WA WIKI: Alipata hamasa ya ushairi kwa kakake, akageuka gwiji

MALENGA WA WIKI: Alipata hamasa ya ushairi kwa kakake, akageuka gwiji

Na HASSAN MUCHAI

HASSAN Pojjo amekuwa mshiriki mkuu kwenye tasnia ya uandishi kwa miaka mingi na ni mshairi mshairi mtajika.

Pojjo ambaye huchangia safu mbali mbali katika gazeti hili, ni mzaliwa wa kijijini Dzirihini, eneobunge la Lunga Lunga, Kaunti ya Kwale.

Alitua duniani mapema mwaka wa 1969. Yeye ni mtoto wa nane kwenye familia ya watoto 10.

Alisomea katika shule ya msingi ya Mwena kuanzia chekechea hadi darasa la saba na badaye akajiunga na shule ya sekondari ya Mombasa High mnamo 1984 kwa masomo ya sekondari.

Utotoni, Pojjo alipenda sana mchezo wa soka na kushiriki mbio. Pia, alivutiwa mno na usomaji wa vitabu mbali mbali vya tamthilia za Kiswahili akiwa nyumbani.

Alipokuwa katika darasa la nne alipenda kuandika hadithi fupi fupi zilizowasisimua wanafunzi wenzake nyakati za mapumziko.

Hali hiyo iliweza kumjenga na hapo ndipo alianza kuajiamni katika uandishi wa lugha ya Kiswahili. Akiwa katika darasa la sita, alianza kuandika maoni na kuyatuma katika Taifa Leo. Bila shaka huu ulikuwa umri mdogo kwa mtoto kama huyu kupata bahati ya kuchapishiwa kazi zake.

Nyota ya ushairi ilimvaa kijana Pojjo akiwa katika darasa la saba. Hamasa ya uandishi wa fani hii ilimjia alipoona kazi za kakake Bw. Sakim Pojjo ambaye pia alikuwa mshairi wa haiba kubwa.

‘’Nikiwa darasa la saba, nilipata hamasa ya kuandika mashairi baada ya kuona madaftari ya mashairi ya kakangu mkubwa Salim Pojjo Babah ambaye ni daktari.’’ anasema Pojjo.

‘’Nilipopata muda, nilipitia madaftari hayo na hata kujaribu kuyaiba na kubadilisha baadhi ya mishororo ili yaonekane tofauti lakini maazimio yangu yaliniweka kwenye matatizo kwani mwenyewe alipogundua aliweza kunipa kichapo.’’ azidi kusimulia.

Mbali na kukwapua mashairi ya kakake,Pojjo alipenda kusikiza mashairi kutoka nchi jirani ya Tanzania hasa kwa mshairi Said Nyoka pamoja na Abdallah Mwasimba ambao kwa sasa ni marehemu.

Marehemu Nyoka alikuwa akimvutia kwa utunzi kutokana na jinsi alivyokuwa akighani mashairi yake. Hali hii ilimwongezea chachu ya kupenda ushairi na pia kujifunza.

Hapo ndipo alipoanza kuandika mashairi yake. Shairi lake la kwanza, “Kimya sikae Salimu” lilimpa ugumu sana kwani hakuwa na uzoefu wa kupanga vina.

Alipojiunga na shule ya upili ya Mombasa High alipatana na marehemu Said Karama aliyekuwa akifunza Kiswahili katika kidato cha kwanza.

Marehemu Karama ambaye anajulikana sana kwa utunzi wa vitabu vya Kiswahili, alimpa mkono wa tahania na kutabiri nyota ya Pojjo kwamba angekuwa msanii hodari siku za usoni. Alimpa mwongozo kuhusu lugha ya Kiswahili na jinsi ya kuandika mashairi.

Baada ya kumaliza Kidato cha Nne shuleni Pojjo aliingia jiji la Tanga nchini Tanzania. Tanga inajulikana sana kuwakuza washairi mahiri kama vile Sudi Kigamba, Malenga wa Mrima na hata Shaban Roberts. Ni mji wenye starehe za aina yake hasa kwa mahadhi ya nyimbo za taarabu.

Akiwa hapa alitangamana na waimbaji na washairi wa mji huu jambo ambalo lilipanua upeo wake kishairi.

Alikaa Tanga kwa mwaka mmoja na baadaye akarudi Kenya akiwa amejizolea ujuzi si haba. Alifululiza moja kwa moja hadi jijini Nairobi kujitafutia riziki na akabahatika kazi na kampuni ya Dental Laboratory Technology.

Akiwa Nairobi, alikutana ana kwa ana na washairi wenzake kama vile Nuhu Bakari,Mohammed Chatu,Said Mwangaluka, Hassan Muchai,Benson Matheka na wengineo. Kwa pamoja, walishirikiana kukuza vipawa vyao kwa kushiriki malumbano mengi yaliyokuwa yakiendelea wakati huo.

Itaendelea Jumapili ijayo.

You can share this post!

BI TAIFA OKTOBA 08, 2020

JAMVI: Raila alivyocheza reggae huku Uhuru akimtazama