Malezi kupita kiasi yana madhara kwa afya ya akili
KWA miaka mingi tafiti zimechunguza uhusiano kati ya malezi na afya ya akili.
Mada hii ni ngumu, na matokeo yamekuwa ya kukanganya.
Watafiti wengine wameripoti kwamba kumlea mtoto huchangia furaha na ustawi wa mzazi.
Wengine wanapendekeza kinyume chake.Utafiti wa hivi karibuni uliochapishwa katika jarida la Journal of Child and Family Studies unapendekeza kuwa si suala la wewe kuwa mzazi bali jinsi unalea ndilo jambo muhimu.
Kulingana na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Mary Washington huko Virginia, Amerika, wanawake wanaozama katika malezi mazito wana uwezekano mkubwa wa kupata matatizo ya afya ya akili kama vile msongo wa mawazo.
Watafiti wakuu katika utafiti huo walilenga wanawake kwa sababu wao ndio hushabikia zaidi mtindo huu wa ulezi.
Watafiti wanasema ni kauli ya wazazi, hasa akina mama, kwamba mzazi anapaswa kujitolea kwa kila kitu kwa ajili ya mtoto wake. Wazazi pia huamini furaha yao binafsi inategemea ufanisi wa watoto wao.
Wao hujitahidi kila mara kuwapa watoto wao shughuli za kuwachangamsha akili, bila wao wenyewe kutenga muda wa kupumzika au kujiburudisha.
Zaidi ya hayo, mara nyingi wazazi sampuli hii hujiona kuwa bora zaidi kuliko mzazi-mwenza katika suala la kulea mtoto wao; jambo linalowafanya kujitwika majukumu mengi ya malezi kila siku – hali inayoweza kusababisha uchovu kupita kiasi na hata kufadhaika.
Watafiti waligundua kuwa wanawake wanaodhani kuwa mama ndiye mzazi wa kimsingi waliripoti viwango vya chini vya kuridhika na maisha.
Aidha, wanawake waliodhani kuwa kulea ni kazi ngumu sana walipatwa na msongo wa mawazo na mfadhaiko. Takriban asilimia 23 ya washiriki walikuwa na dalili za mfadhaiko.
Kulingana na watafiti wa malezi dijitali, akina mama wengi wanaamini kuwa kujinyima mapumziko au kupuuza mahitaji yao binafsi kutawafanya kuwa mama bora zaidi, na hatimaye kunufaisha watoto wao.
Lakini cha kushangaza ni kwamba aina hii ya malezi inaweza kuleta madhara kwa pande zote mbili – mzazi na mtoto.
Bila shaka, watoto hustawi zaidi wanapokuwa na wazazi wenye furaha na afya bora. Nao wazazi hufurahia zaidi safari ya malezi wanapoafikia usawa kati ya malezi ya watoto na muda wao wa kujivinjari binafsi.
Katika familia zenye wazazi wawili, wataalamu wanapendekeza kuwa mgawane majukumu ya malezi ili kuimarisha ustawi wa kila mzazi na kurahisisha malezi ya mtoto.
Hata mapumziko mafupi kama kwenda matembezi, kunywa kahawa au kusoma jarida kutasaidia sana mzazi kupata nafuu ya kiakili na kumpunguzia msongo wa mawazo.