Makala

Man United huenda ikakosa huduma za tegemeo Mazraoui dhidi ya Liverpool

Na MASHIRIKA October 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Manchester United huenda wakamkosa difenda Noussair Mazraoui kwenye mchezo muhimu dhidi ya mabingwa watetezi Liverpool ugani Anfield hapo Oktoba 19, 2025.

Vijana hao wa kocha Ruben Amorim walipepeta Sunderland 2-0 kabla ya mapumziko ya mechi za timu za taifa.

Amorim sasa analenga ushindi wa pili mfululizo tangu achukue mikoba ya ukocha. Hata hivyo, Mazraoui hajachezea mashetani wekundu tangu Septemba 20 kutokana na jeraha lisilofahamika, na Amorim amekiri kuwa hajui kama beki huyo atakuwa tayari kwa mpepetano huo.

Akitoa taarifa za majeruhi mnamo Oktoba 17, Amorim amesema: “Licha [Martinez] yuko karibu kurejea mazoezini na timu. Kuhusu Mazraoui, sijui.”

Martinez alipata jeraha kwenye goti alipokuwa akicheza dhidi ya Crystal Palace mwezi Februari, na kurejea kwake uwanjani bado hakutarajiwi hivi karibuni kwani benchi la ufundi halitaki kuhatarisha afya yake.

Amorim aliwaruhusu wachezaji waliokuwa na majukumu ya timu za taifa muda wa ziada wa kupumzika, lakini alithibitisha kuwa wote watakuwa tayari kwa mechi ya Jumapili. “Wale waliokuwa timu za taifa wako sawa,” akasema. “Lakini wengine walikuwa mbali, kama Japan, kwa hivyo tunahitaji kuwa waangalifu.”

Aliendelea kueleza kuwa Diogo Dalot hakucheza mechi ya mwisho na alikuwa kambini, huku Bruno Fernandes akicheza dakika 62 tu, kwa hivyo walijaribu kupanga ratiba ili wote wawe sawa.

Akizungumzia kipa chipukizi Senne Lammens, Amorim alisema, “Alifanya kazi nzuri dhidi ya Sunderland, na anaweza kuanza tena. Ameonyesha utulivu mkubwa, japo bado hajafika kiwango cha Peter Schmeichel.”

Imetafsiriwa na Geoffrey Anene