Manung'uniko katika ngome za Jubilee
Na MWANGI MUIRURI
SERIKALI ya Jubilee iliundwa mwaka wa 2013 kwa msingi wa muungano wa Rift Valley na Mlima Kenya kama wanahisa wakuu baada ya vyama vya United Republican Party chake William Ruto na The National Alliance (TNA) chake Rais Uhuru Kenyatta kuungana.
Kama kawaida, wenyeji wa ngome hizi mbili wamekuwa wakitarajia kutuzwa keki kubwa ya kitaifa kwa msingi kuwa “serikali ni yetu.”
Hii ni licha ya kuwa uchaguzi huwa sio wa kusaka wananchi wa kupakuliwa chakula kingi cha serikali kuliko wengine, bali huwa wa kutafuta serikali
ya kitaifa ya kutekeleza usawa wa kiutawala kwa wote.
Lakini baada ya uchaguzi wa urais wa mwaka 2017 ambao ulitekelezwa mara mbili baada ya mahakama kutupilia mbali matokeo ya kwanza, kuyumba kwa usalama kulishuhudiwa ambapo mrengo wa upinzani ukiongozwa na Raila Odinga uliishia kujiapisha kama ‘serikali ya pembeni’.
Ilibidi Rais Kenyatta amsake Odinga wasalimiane ili kuwe na maridhiano ya kuleta utulivu nchini.
Sasa, salamu hizi, baadhi ya viongozi na raia wananung’unika kuwa ziliingia kuondoa vipande vile vitamuvitamu vya keki ya kitaifa kutoka sahani ya ngome hizo mbili za Jubilee.
Kwa mujibu wa mbunge wa Bahati, Kimani Ngunjiri hizi salamu ziliingia kulazimisha maeneo yaliyo na ‘hisa nyingi’ ndani ya hii serikali kutengwa.
“Sisi ndio tulipambana kufa kupona kusaka idadi ya kura tosha za kumweka Rais Kenyatta mamlakani, tukitazamia kuunda serikali lakini leo hii sisi
ndio tumegeuzwa kuwa upinzani,” anasema Ngunjiri.
Wimbo ni uo huo katika ngome za Naibu Rais William Ruto ambapo wenyeji wanateta kuwa hakuna maendeleo wanapata kutoka kwa hii serikali “bali hela na macho ya serikali kwa sasa ni katika ngome za upinzani.”
Ni katika hali hiyo ambapo msanii Ng’ang’a wa Kabari ametunga wimbo ambao ujumbe wake umepakiwa kama radi ukielekezwa kwa serikali ya Jubilee.
Anasema kuwa taswira ya Jubilee kwa sasa kwa wenyeji wa Mlima Kenya na Rift Valley ni ile ya mtoto kuitisha mkate kwa babake lakini anakabidhiwa ‘mtu au mnyama mwingine tofauti’.
“Hii ni serikali ambayo haina haja na masikini. Wakubwa kwa wadogo wanalia serikali. Si wahudumu wa bodaboda, si wa matatu. Kila mtu anakonda na anateseka na kukambwa na njaa kwa sababu ya serikali,” anasema.
Anawaza ni kwa nini watu wa maeneo hayo waliamka asubuhi na mapema kwenda kupigia serikali ya Jubilee kura wakiimba “Tano tena.”
Analia: “Ni Tano Tena ya nini hata afadhali tungekaa nyumbani wengine wakapige kura.”
Anatoa mfano wa mfumkobei.
Analia kuwa umaskini ambao umekumba wengi wa waliopigia serikali hii kura hauna kifani, umaskini ambao umegeuza hata familia kukumbatia
kusambaratika kwa maadili kwa kiwango kikuu.
“Leo hii utapata kuwa baba mzazi ni muuzaji bangi, mama ni kahaba naye mwana wao wa kiume ndiye hupora watu mtaani. Tuliahidiwa kazi kama
vijana; kumbe hatukujua kuwa kazi ni kufungwa jela, kubomolewa vioski na kuhangaishwa tukiitwa wezi!” anatafakari.
Analia kuwa leo hii ni rahisi kwa mwizi wa kuku kufungwa huku wezi wakuu wakiwa serikalini.
“Wanjiku wa leo hii anamalizwa na kusukumwa hadi kwa kaburi. Na sasa wametuanza wakituambia kuhusu kura za mwaka 2022. Sioni tukitokea tena kupiga kura. Ni heri mjichague kwa kuwa tumechoka kudanganywa,” anateta.