MAONI: Vita vya kijinsia viachiwe wajinga
HIVI umegundua kuwa watu wanaolialia eti Kawira Mwangaza ametupwa gizani si Wameru?
Inaonekana Wameru karibu wote wameridhika na wanafurahia kuondolewa mamlakani kwa gavana wao wa kike.
Niambie, Meru kumekolea taasubi ya kiume, au Kawira si mfano bora wa mwanamke bomba kwa viwango vya Kimeru?
Nenda katafute sababu nyinginezo, ila mwenzako nimejua tatizo ni taasubi ya kiume, yaani madume yamekataa kutawaliwa na mwanamke.
Na nina ushahidi: Hafla ya kuapishwa kwa gavana mpya, Mutuma M’Ethingia, ambaye ni mwanamume kwa taarifa yako, ilihudhuriwa na mibabe-dume inayojulikana kwa kuendesha siasa za Meru kama kinyago.
Huoni ajabu kwamba mahasimu wa kisiasa kama vile Kiraitu Murungi, Mithika Linturi, Peter Munya na wabunge wa janibu hizo walipatana na kuhudhuria hafla ile kwa kuwa adui yao mkuu, mwanamke, amezama?
Hakuna hata mmoja ambaye angeona haya kumlima mama wa watu kama shamba za miraa au ‘muguka’ mchana jua la utosi?
Meru kuna tatizo. Na mwanzo wa kusuluhisha tatizo ni kukiri kwamba lipo, kisha ukalifanyia kazi.
Hata hivyo, nawaomba mibabe-dume hao wasikubali kuna tatizo.
Hata wakijua lipo, ni heri wafiche vichwa vyao mchangani anavyofanya mbuni akiona upepo.
Katika nchi ambapo mambo mengi yanakwenda visivyo kama Kenya, tunahitaji burudani ya kila aina, hata ya watu ambao wamekwenda shule nzuri za kimataifa ila wakashindwa kutembea na majira.
Binafsi nahitaji watu wa kucheka na kupiga vijembe, kwa hivyo sote tukiwa wastaarabu nitakosa cha kuandikia.
Ukiwaona waambie wazidishe unoko dhidi ya wanawake, wakitaka waanzishe kampeni kote nchini ya kuwabadilisha wanaume wastaarabu, wakatae ‘kukaliwa chapati’, kulishwa limbwata wala mkate wa samli!
Hapo ndipo wanaharakati wa kike watakapokuja juu na kuwahimiza wenzao kote nchini wawawekee waume zao vikwazo fulani ambavyo sitaki kuandika hapa, lau sivyo hatutawahi kukutana tena kwenye ukurasa huu.
Utasikia wakiwahimiza wanawake wenzao wasiwapikie waume zao, ila najua mgomo huo hautafaulu.
Ama unataka kuniambia hujui wanawake wengi hupika chakula kwa ajili ya kujilisha na kuwalisha watoto wao, mijibaba inakuwa ‘mgeni asiyealikwa’ tu?
Kuna wanaume wengi ambao hula kwa bahati, kwa sababu wake zao wangali watu wazuri, wanafanya kazi ya Mungu ya kuwalisha wasio na chakula.
Mwanamume mwenzangu nisikilize; tangu hapo nikikwambia wajinga ndio waliwao. Ukiiga mfano wa mibabe hiyo tajiri kutoka Meru utaumia peke yako.
Wao wana hela za kuwalipa wapishi bora duniani, yaani wapishi wa vya kuliwa kwa vinywa na vinginevyo, ilhali wewe hata riziki ya Mungu kutia kinywani ni kwa hisani ya mkeo.
Danganywa uingie kiburi na jeuri, kiherehere chako kikuonyeshe eti sauti yako kama mwanamume inapaswa kusikika, utakufa njaa!
Sijaona wala kusikia kuwa Kasongo ana mpango wowote wa kutoa chakula cha msaada kwa wanaume wajeuri. Jifunze kuchagua vita.