Makala

MAPISHI: Biriani ya nyama ya mbuzi

October 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MARGARET MAINA

[email protected]

Muda wa kuandaa: Dakika 15

Muda wa mapishi: Dakika 40

Walaji: 5

Vinavyohitajika

  • Mchele wa Basmati kilo 1
  • Nyama ya mbuzi kilo 1
  • Tangawizi
  • Kitunguu saumu
  • Binzari
  • Pilipili manga
  • Vitunguu maji 6
  • Nyanya 4
  • Mafuta ya kupikia
  • Pilipili nyekundu kijiko 1
  • Giligilani vijiko 3
  • Chumvi
  • Hiliki

Maelekezo

Weka nyama iliyo kwenye sufuria hapo mekoni. Weka tangawizi, kitunguu saumu, binzari, pilipili manga na chumvi. Hakikisha nyama imeiva na haipotezi mchuzi. Epua.

Chukua vitunguu maji kisha vikate kwa umbo mviringo na nyanya zikate vipande vidogovidogo.

Bandika sufuria safi yenye mafuta mekoni kisha kaanga ile nyama mpaka iwe ya kahawia halafu iepue na uichuje mafuta. Weka pembeni.

Weka vitunguu – baadhi – kwenye yale mafuta na uvikaange kabla ya kutia binzari, unga wa pilipili nyekundu, giligilani, mbegu za hiliki na pilipili manga.

Changanya vizuri viungo upate mchanganyiko unaohitaji kisha mimina ule mchuzi wa nyama.

Weka nyanya kwenye ule mchanganyiko. Pika mpaka mchuzi wote ukauke.

Weka nyama halafu ongezea hapo chumvi kama unainyunyiza ikolee vizuri. Koroga vizuri na taratibu kwa muda wa dakika tano kisha epua.

Bandika sufuria nyingine; weka mafuta na vitunguu, weka majani ya giligilani, majani ya mint, funika kwa robo saa kisha weka wali wako.

Ongeza vikombe vitano vya maji na chumvi kisha funika chakula.

Punguza moto mpaka maji yakauke, halafu chukua ule mchanganyiko wenye nyama mwagia – nusu tu – juu ya wali kisha acha uive.

Baada ya dakika 10 funua chakula, geuza na upakue.